Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mafinga Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia. Naomba moja kwa moja nianze kwanza kwa kushukuru Mamlaka ya TRA hususani Kamishna Mkuu na Kamishna wa Kodi za Ndani, lakini pia na Waziri kwa sababu wakati fulani niliwasilisha kwao malalamiko, licha ya kuwa niliwasilisha kwa meseji juu ya wananchi wangu wanaofanya biashara ya mbao na matatizo wanayokutana nayo. Kwa kweli hatua zilichukuliwa, Kamishana wa Kodi za Ndani akaja Mafinga akafanya mkutano karibu saa sita kuwasikiliza wale wadau. Kwa sababu ilifika wakati ilikuwa kama vile kufanya biashara ya mbao ni laana. Ukipakia mzigo mtu mwenye lori anaulizwa mashine ya EFD aliyokulipa mwenye mzigo ya transport iko wapi, hana, faini milioni nne. Kwa hiyo, tulikuwa tuna paralyse sekta ya mazao ya misitu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa hili napenda kupongeza lakini pia napenda kushauri. Kumekuwa na malalamiko sana ya wafanyabiashara hususani wafanyabiashara wadogo wa Mji wa Mafinga. Ushauri wangu kwa Serikali na kwa TRA, naomba kupitia Idara ya Elimu kwa Mlipa Kodi kwa mwaka walau mara mbili iwe inatoa elimu lakini pia ikutane na wafanyabiashara na kujua ni changamoto gani wanakutana nazo ili kwa pamoja waweze kuwa on the same boat. Kwa sababu tunachotaka watu walipe kodi sustainably siyo mwaka huu mtu alipe kodi Sh.1,000,000, mwaka unaofuatia Sh.800,000, mwaka unaofuata Sh.500,000, mwaka unaofuatia ame-collapse. Lazima tuwekeane mazingira Serikali ipate chake lakini pia na wafanyabiashara wa-survive progressively. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili, mimi nilishika shilingi hapa wakati wa bajeti ya Wizara kuhusiana na fedha za miradi viporo. Mheshimiwa Jitu jana amezungumza, kwamba fedha hizi Serikali imekubali itatoa kwa awamu nne, itaanza na shilingi bilioni 32 kwa 29 kwa miradi ya elimu na afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu mimi kwa Serikali fedha hizi Mheshimiwa Waziri ni muhimu sana zikawa ni reflected kwenye hiki kitabu cha matumizi. Naiamini Serikali yangu lakini wasiwasi wangu Waheshimiwa kama tutapewa hizi fedha awamu hii ya mwezi wa sita na ambazo Mheshimiwa Waziri nikuombe, tumebakisha siku tisa kumaliza mwaka wa fedha, ni matarajio yangu kwamba ya kufanya majumuisho fedha hizi zitakuwa zimeshaenda kwenye halmashauri ili michakato ya manunuzi kupitia force account iweze kuanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini nasema zile reflected humu Waheshimiwa Wabunge, tukianza mwaka 2018/2019 kama hazipo humu, pamoja na kuwa naiamini Serikali yangu tunaweza tukapigwa changa la macho. Kwa sababu baadaye tutaambiwa haipo katika vitabu. Nawaomba sana muangalie suala hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, Serikali hapa imesema kuhusu asilimia kumi ya wanawake na vijana na kwa mujibu wa Kamati imependekeza kuwa iwe 4, 4, 2 kwa maana wanawake, vijana na walemavu. Hata hivyo, lazima tukubaliane, halmashauri hazifafani uwezo. Mimi napendekeza hii asilimia kumi ilenge maeneo ambayo ni majiji au manispaa. Kuna halmashauri baada ya Serikali ku- centralize vyanzo vingi hii ten per cent inakuwa kama maigizo unless otherwise tunafanya politics.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama tuko serious kabisa tumehamasisha wananchi wajiunge katika vikundi Serikali itusaidie katika baadhi ya maeneo ambako vyanzo viko chini iweze kupeleka asilimia kumi ya vikundi kama ruzuku. Otherwise kama halmashauri kwa vyanzo vya ndani inakusanya shilingi milioni 500 asilimia kumi unazungumzia shilingi milioni 50, hivi ukiwapa vikundi Sh.100,000 na vikundi viko vingi tumewasaidia au tumefanya politics?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, usahuri mimi kwa Serikali kwenye ten percent hii katika baadhi ya maeneo tusifanye unform. Majiji kama Arusha, Dar es Salam, Mwanza na Manispaa unaweza ukasema waende kwa utaratibu huo, lakini kuna maeneo kwa kweli vyanzo ni dhoofu. Kwa hiyo, Serikali iangalie uwezekano wa kupeleka ruzuku ili hamasa tuliyowapa wananchi kwamba wajiunge katika vikundi iwe ni kweli kwa vitendo isiwe tu katika makaratasi ten percent. Ten percent yenyewe imekuwa ngumu kwa sababu hata OC haiendi ipasavyo; halmashauri zinajikuta kwamba zinachukua fedha matokeo yake inakua ten percent katika makaratasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie pia challenge mbalimbali ambazo Serikali imesema inakabiliana nazo katika masuala ya kuongeza makusanyo. Mheshimiwa Waziri tuna fedha tunapoteza kwenye suala la fuel levy kwa sababu hatujui mpaka leo mafuta kiasi gani yanaingia katika Taifa hili. Ameenda Mheshimiwa Rais pale bandarini, ameenda Waziri Mkuu tena Waziri Mkuu nadhani ameenda hata tatu kuhusiana na suala la flow meter lakini mpaka leo hatufahamu suala la flow meter limefikia wapi. Flow meter yenyewe iliyopo watu wana tamper nayo wakati mwingine wanacheza nayo isipige alamu lakini hata ule mchakato wa kupata flow meter nyingine hatujui umeishia wapi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kama Waziri anataka pesa, kuna pesa zingine ziko nje nje lakini tutaweza kuzipata kama tutadhibiti baadhi ya mianya moja wapo likiwa ni suala zima la kudhibiti tuweze kujua idadi ya mafuta yanayoingia katika taifa letu. Otherwise tutawakamua Wamachinga, tutawapa sijui hiyo TIN namba that’s is very peanut, kuna pesa mamilioni kwa mabilioni katika suala zima la mafuta.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hili suala la ETS, yaani I am very layman linapokuja suala la mambo ya uchumi lakini na u-layman wangu nashindwa kuelewa hivi sisi kweli Mheshimiwa Mpango katika zama hizi za digital tunashindwa kuwa na control mechanism ya sisi kama sisi ili kuokoa yale mabilioni badala ya kwenda kwenye kampuni tu bora kampuni yakabaki hapa yakatusaidia na tumesomesha vijana. Nadhani Mheshimiwa Waziri hili jambo kama Serikali mnatakiwa mlitafakari mara mbili. Hatuwezi tukawa tunahangaika kwamba hatuna vyanzo lakini kuna pesa tunazipoteza tu. Naamini katika mifumo ya kisasa Serikali ina uwezo kabisa wa kujua na ku-cotrol uzalishaji uwe wa maji, soda au wa vinywaji vyovyote hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala la Mheshimiwa Waziri kurejeshewa mamlaka ya kusamehe, kuna watu wengine hapa tunapata miradi ambayo ni misaada kutoka kwa wafadhili marafiki, kutoka kwa NGO’s na Balozi mbalimbali, niombe sehemu ile ya msamaha Mheshimiwa Waziri hebu iwe extended iende mpaka kwenye miradi ya namna hii ambayo tunaipata katika kuangaika kwa ajili ya wananchi wetu. Mimi nina mradi pale Ubalozi wa Japan unatujengea theater ya kisasa, Halmashauri imelazimika kulipa zaidi ya shilingi milioni 30 kama sehemu ya VAT. Niombe pamoja na mipango hii ambayo umeileta hebu huo msamaha tukupe nguvu uweze kusamehe hata misamaha ambayo sisi tumehangaika kwa marafiki zetu mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni ukurasa 59 wa hotuba na Waheshimiwa Wabunge naomba mnisikilize sana, amekuja hapa na hizi HS Codes kwa ajili ya makaratasi ya kuzalishia madaftari na vitabu. Mheshimiwa Waziri hizi HS Codes, unless ama mmejua au hamjajua, Waheshimiwa Wabunge niwafahamishe kilichosamehewa kwenye daftari kwa mujibu wa hizi HS Codes ni cover, hili hapa, kama ni kitabu ni cover. Hizi HS Codes Mheshimiwa Waziri ni za makaratasi magumu. Kama kweli tunataka tusamehe kwa ajili ya uzalishaji wa madaftari, muende mkazi-review hizi HS Codes. Niwaombe Waheshimiwa Wabunge tujitahidi kujifahamisha na kuhabarishana. Kwa sababu ukienda tu ukiona hizi HS Codes hapa tumepiga makofi; lakini sisi kama Wabunge wa Bunge Tukufu tupigie makofi hii cover? Katika daftari cover na hiki cha ndani kipi kingi? Kina Mwalimu Mulugo wanajua mambo ya madaftari. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri muende mka-review kitu hiki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha za LGDG, mimi naendelea kuomba mmesema kuna miradi mikakati; siyo kila halmashauri inaweza kuwa na mradi mkakati, hapa ndiyo sisi pakutokea kama Wabunge na kama halmashauri. Kwa hiyo, mimi naomba tusijifiche kwenye kichaka cha miradi mikakati, fedha hizi zinazokwenda kwenye maendeleo na ku-stimulate wananchi kuchangia na kuhamasisha na kufyatua matofali kwa kutumia nguvu zao Serikali iendelee kuzitenga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, sports betting, hatuwezi kukwepa duniani sasa hivi hicho ni chanzo kikubwa sana cha mapato. Sheria imetoka asilimia 6 mpaka 10 ya mauzo ghafi, napendekeza na kushauri ili kuleta fairness kwa mchezaji na mchezeshaji na ili kuvutia wachezaji wengi wasikwepe waendee kwenye online sports betting, Serikali iweze kuangalia kusudi tupanue wigo wa mapato. Kwa sababu ukiweka mazingira ambayo yanavutia kwa mchezaji na mchezeshaji maana yake tutapata fedha nyingi lakini sehemu ya fedha tutenge iende kwenye michezo. Kama ni kugharamia timu ya taifa, timu za riadha , kuboresha viwanja kwa sababu michezo nayo ni sehemu ya kiwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.