Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Rashid Ali Abdallah

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Tumbe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. RASHID ALI ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiisikiliza kwa makini taarifa ya Kamati ya Bajeti na ukawasikiliza kwa makini wachangiaji mbalimbali utaona kwamba wanatilia mashaka bajeti yetu hii. Mimi nasema kwamba nina mashaka makubwa sana kuhusiana na bajeti yetu hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia bajeti hii vipaumbele vyake havitoshelezi. Nasema hivi kwa sababu Mheshimiwa Waziri wakati akiwasilisha hotuba yake alisema uchumi umepanda kwa asilimia 7, jambo ambalo ni mashaka makubwa sana. Kama uchumi umepanda, tukija kwenye kilimo, kilimo kimekua kwa asilimia 3.7, ambapo ili uweze kupunguza umaskini kwa wakulima ni lazima kilimo kipande angalau kwa asilimia 8 hadi asilimia 10. Sasa tuna asilimia 3.7 kwa miaka kumi, Mheshimiwa Waziri anasema uchumi umepanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna barabara kilometa 86,472 lakini barabara za lami ni asilimia 9.7 tu, lakini tunaambiwa bado uchumi wetu umepanda. Tunahitaji megawati 3,000 lakini tangu nchi hii ipate uhuru tuna megawati 1,424.6, bado tunahitaji megawati 1,575.4 ili tufikie mahitaji yetu. Sijui ni miaka mingapi tunahitaji ili tufikie lengo hili kwa sababu hizi megawati 1,400 tumechukua miaka 57, sasa megawati 1,500 tutachukua miaka mingapi? Sidhani kwamba katika Bunge hili tutakuwepo na sidhani kwamba CCM itakuwepo katika madaraka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali Kuu ilitakiwa ikusanye shilingi trilioni 19 lakini imekusanya shilingi trilioni 14, huu uchumi umepanda vipi? Halmashauri zetu zinatakiwa zikusanye Sh.687,304,000,000, zimekusanya Sh.437,607,000,000 ambapo tofauti ni shilingi bilioni 249.699, ni nusu yake. Sidhani hawa wataalam ambao wanafanya tathmini za makusanyo wako sawasawa na wanazijua halmashauri zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu chochote kinaathiriwa na idadi ya watu. Kila mwaka idadi ya watu inaongezeka asilimia 3.1, katika miaka mitano kuna watu milioni 7.6 kwa hivyo kwa muda wa miaka 10 tutakusanya watu milioni 15.2. Hawa watu wanataka matibabu, madawa, shule na wana mahitaji mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine ambacho nakieleza, kila mwaka deni linapanda, kwa hiyo, kwa mwaka huu deni limepanda mara mbili ya mwaka uliopita. Kila mwaka wahitimu wetu wanaomaliza shule ni 800,000 lakini Serikali ina uwezo wa kuajiri 40,000, kwa hivyo, kuna watu 760,000 kwa kila mwaka wanakosa ajira. Kwa hivyo, tukifanya miaka mitano tuna watu milioni 3,800,000 wako bench wanasubiri ajira, leo tunaambiwa uchumi umepanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma ukurasa wa 79 wa kitabu cha Mheshimiwa Dkt. Mpango katika hitimisho lake anasema:-

“Naomba Waheshimiwa Wabunge na wananchi kwa ujumla tuunganishe nguvu zetu, vipaji vya wananchi wetu na biashara zetu ili kufikia malengo tunayoyakusudia. Hivyo, tunahitaji uzalendo na nidhamu ya kazi ya hali ya juu tukikusudia kuondoa umasikini”.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri hapa amesema Wabunge na wananchi wote kwa jumla, hii ni kusema kwamba uchumi wa Taifa unategemea wananchi wote. Hata hivyo kwa sasa wapinzani katika Taifa hili wanaonekana ni maadui wakubwa na nusu ya wananchi ni
wapinzani na uchumi unahitaji mshikamano wa umoja katika Taifa kwa mwendo huo uchumi huu utakua kwa kaisi gani?

Mheshimiwa Naibu Spika, ni lazima kuwe na uhusiano wa kimataifa kwani umeporomoka, haupo. Ni lazima tuwe na demokrasia, demokrasia haipo. Ni lazima tuwe na utawala wa sheria, utawala wa sheria haupo. Ni lazima tuwe na utawala bora, utawala bora unanuka kabisa katika nchi hii. Katika hali hii, vipi tutaweza kujenga uchumi wetu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hayo, nitoe ushauri kwamba turejee nyuma tuweze kuimarisha kilimo. Sijaona msukumo wa Serikali katika kilimo.

T A A R I F A . . .

MHE. RASHID ALI ABDALLAH: Mheshimiwa naibu Spika, taarifa hiyo siipokei, tuna ushahidi wa kutosha, mauaji yanayotokea katika nchi hii, watu wanafungwa hovyo katika nchi hii, maonevu yanayotokea katika nchi hii na ushahidi upo. Hawezi Mheshimiwa Waziri akafananisha Tanzania na nchi ile ya Rwanda na Burundi, zile ni nchi ndogo sana (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema malengo makuu katika Taifa hili ni lazima tuwekeze kwenye kilimo. Adui mkubwa wa nchi hii ni yule ambaye anashindwa kuwekeza katika kilimo, anashindwa kutoa misaada katika kilimo kwa sababu asilimia kubwa ya wananchi wake wako kwenye kilimo. Serikali bado haijaamua kuwekeza kwenye kilimo. Nchi moja ya Rwanda imewekeza kwenye kilimo takribani shilingi trilioni 7 lakini leo Tanzania wametoa pesa za maendeleo asilimia 11.