Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CUF
Constituent
Mwanakwerekwe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ALI SALIM KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Awali ya yote, nimshukuru Mwenyezi Mungu kunijalia leo hii kusimama hapa kwa ajili ya kuchangia bajeti hii. Leo mimi nitakuwa zaidi na maswali na nina mambo matatu tu ya kuchangia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimuulize Waziri wa Fedha, makusanyo yote ambayo yamekusanywa ndani ya nchi ni shilingi trilioni 21, matumizi yake ni shilingi trilioni 21, wapi imewahi kutokea makusanyo yaliyokusanywa na matumizi yakaenda sawasawa? Yaani hata shilingi haibaki, 21 trillion mmekusanya, 21 trillion mmetumia. Hebu mtuambie ninyi wachumi na watu wa bajeti hii imekaaje? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili ni kwamba ukiacha hayo hizi shilingi trilioni 21 zimekwenda kwenye matumizi ya kawaida tu, deni, mishahara, hizi fedha za maendeleo hapa ziko wapi?
T A A R I F A . . .
MHE. ALI SALIM KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba niendelee kwa sababu jana yeye mwenyewe alikiri kwamba siyo mchumi, wapo wachumi hapa watasema kwamba unapokusanya unatumia 100% hakuna hata senti ambayo inabakia unatumia kama ilivyo, watatuambia hapa wachumi wapo, tuna madaktari wawili hapa watatueleza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuonyesha kwamba hizi taarifa ni za kutengeneza tuje katika pato la Taifa. Pato la Taifa Mheshimiwa Waziri wa Fedha amesema kwenye kitabu chake kwamba ni shilingi trilioni 50. Sasa hivi Tanzania current population ni watu milioni 59, sasa milioni 59 ukigawa kwa shilingi trilioni 50 unapataje 2,275,000 kuwa pato la mtu wa kawaida kwa kila Mtanzania?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba wakija hapa watusaidie hizi hesabu zimekaaje kwa sababu ukifanya hesabu hapa, kama ukifanya kwa hiyo milioni 50 maana yake pato la kila Mtanzania ni wastani wa 1,063,000. Sasa hapa Waziri wa Fedha anatuambia kwamba pato la Mtanzania limeongezeka na ni 2,275,000 kwa mwaka wakati yeye mwenyewe amekiri hapa pato la Taifa ni shilingi trilioni 50. Kawaida katika kujua pato la mwananchi unagawa pato la Taifa kwa idadi ya watu ambao unao. Sasa Mheshimiwa Waziri akija hapa atuambie hii hesabu imekaaje. Nasema haya kuonyesha kwamba haya ni mambo ya kutengeneza. Sasa tukisema hii ni bajeti hewa tunakosea? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikitoka hapo tuje kwenye masuala ya uwekezaji. Serikali ya Awamu ya Tano ilisema kwamba inafufua Shirika la Ndege kwa ajili ya kukuza uchumi wa nchi hii. Ukichukua taarifa hii ya CAG anasema wazi kwamba taratibu za manunuzi ya umma hazikufanyika na Serikali imekiuka Kanuni ya 10(4), Kanuni ya Manunuzi ya Umma katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyopitishwa mwaka 2013. Sasa ikiwa leo utaratibu tu tunaukosea, tunakwendaje kuwekeza na mradi huu uweze kuwa na tija kwa wananchi wa Tanzania? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa zinakinzana, ukiangalia kitabu cha Mheshimiwa Dkt. Mpango anasema kwamba mwanzo waliomba shilingi bilioni 500 kununua ndege na mwaka 2017/2018 wakaomba tena shilingi bilioni 500 kumalizia kulipia ndege na sasa wameshaomba tena pesa nyingine kwa ajili ya kukamilisha malipo kwa baadhi ya ndege na utaratibu wa kufanya operesheni lakini inatofautiana na kitabu cha Waziri wa Uchukuzi. Waziri wa Uchukuzi anasema mwaka jana wameomba kwenda kukamilisha malipo ya ndege sita lakini leo humu Waziri Mheshimiwa Dkt. Mpango kwenye kitabu chake anasema wametenga shilingi bilioni 495.6 na kuwa wamekamilisha malipo ya asilimia 30 ya ndege mbili za CS3100 wakati huku walisema wanakamilisha malipo, sasa hii biashara mnaifanyaje?
Mheshimia Naibu Spika, nimuombe Waziri akija hapa atupe sera ya ufufuaji wa hili Shirika la Ndege, atuambie hapa sera ni hii kwa sababu ikiwa sera ya shirika imekosekana unatengenezaje business plan? Unalifanyaje Shirika lijiendeshe kwa faida? Ukiangalia kuna mashirika kadhaa ambayo yana hali mbaya kwa sababu hapa tatizo siyo kununua ndege, tatizo ni utaratibu wa kuendesha shirika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Shirika la Alitalia, wanazo ndege lakini sasa hivi linatafutiwa wabia ili waweze kuliendesha shirika. Kuna Shirika la British Airways sasa hivi Qatar ndiyo wanakwenda kulihuisha lina-suffer. Kuna Shirika la Air Rwanda limeshafilisika tayari. Kuna Shirika la South Africa sasa hivi linaomba watu wakalisaidie ili lifufuke. Sasa sisi tukisema hapa hatusemi kwa sababu tunaichukia Serikali, tunataka hili shirika liendeshwe kwa faida. Kama tunaendesha shirika kwa kupitia safari zetu za ndani basi tungeanzia hapa halafu baadaye tukaenda sehemu nyingine lakini huku tunakoelekea na ndege ambazo mmenunua inaonekana wazi ndege hizi mnakwenda kuzikodisha kwa mashirika mengine kwa sababu mtakuwa hamuwezi kuzihudumia na wala hamtaweza kufanya ushindani wa kibiashara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapoyasema haya tunayasema kwa sababu nchi hii ni yetu sote. Ikiwa hamtaki ushauri huu ambao tunawapa matokeo yake mtakuja kuona. Kwa sababu Serikali ya Awamu ya Tano mnakataa kujibu maswali ya Serikali ya Awamu ya Nne, mnasema Serikali ya Awamu ya Tano imejipambanua, imeamua, inafanya, sasa hii yenu nyie mkimaliza anakuja kujibu nani? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimalizie kwa kusema kwamba tatizo kubwa linaloonekana ni kwamba Rais amewaamini watu wake lakini wanapomrejeshea taarifa hawamrejeshei taarifa sahihi. (Makofi)