Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Hassan Elias Masala

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nachingwea

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia hotuba ya bajeti. Nami niungane na Wabunge wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na wasaidizi wake kwa kutuletea yale mambo ambayo tunafikiri yana manufaa makubwa kwa wananchi wetu lakini kwa Taifa letu kwa ujumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na pongezi hizo, naomba nijielekeze kwenye eneo moja linalohusu kilimo. Kabla sijazungumza lolote, naomba nijaribu kumpitisha kidogo Mheshimiwa Waziri na timu yake ili waweze kujua wapi tumetoka. Toka mwaka 2015 wakati tunaingia hapa kwa mara ya kwanza tulitoa mapendekezo kadhaa kwa ajili ya kuboresha mazao yetu makubwa ambayo yamekuwa yanaliingizia Taifa letu kipato. Katika mazao haya lipo zao kubwa la korosho ambalo limekuwa linalimwa kwenye baadhi ya maeneo au kwenye baadhi ya mikoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, jitihada ambazo zimefanywa na Wizara ya Fedha kwa kutondoa tozo tano ambazo zilikuwa kikwazo zimepelekea kuongeza tija lakini pia kiasi kikubwa cha fedha katika mzunguko mzima, kwanza kwa wakulima wetu lakini pia kwa Taifa zima. Kama mwakilishi wa wananchi, nitakuwa mtovu wa fadhila kama sitatoa shukurani kwa sababu ni Mheshimiwa Mpango ndiye aliyefanya kazi ya kuondoa zile tozo za usafiri, unyaufu, kulipa wale viongozi wa vyama vikuu na maeneo yale yote ambayo nafikiri yalipelekea kwa mara ya kwanza kuanza kuuza korosho kwa bei kubwa na wananchi wameweza kunufaika.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na kumpa pongezi hizi kidogo nimepata mashaka kupitia pendekezo la bajeti ambayo iko mbele yetu. Nilikuwa nasoma katika ukurasa wa 69 juu ya azma ya kuleta mabadiliko kwa ajili ya kuhakikisha fedha zinazotokana na mazao ambayo yako chini ya Bodi za Mazao kufikiria kuziingiza katika Mfuko Mkuu. Jambo hili Mheshimiwa Dkt. Mpango na Serikali yangu naomba niseme kwetu sisi kama wakulima hamtakuwa mmetusaidia kwa namna ambavyo mmefikiria. Nimwombe Mheshimiwa Dkt. Mpango wazo hili ambalo analileta hebu afikirie kuliondoa kwa sababu atakwenda kutugombanisha na wakulima wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nina hoja kwa nini nasema hivi lakini yako mapendekezo ambayo napenda kwa umakini ayachukue na akayafanyie kazi. Asipofanya hivyo, nafikiri jana amemsikia Mbunge mwenzetu mmoja alikuwa anazungumza kwa utani lakini alichokuwa anakizungumza ndicho kitu ambacho kipo kwa wakulima ambao wametutuma kuwepo hapa ndani. Sisi Wabunge ambao ni wenye Serikali hii tusingependa kuona jitihada kubwa zilizofanywa na Serikali zinaenda kuharibika kwa ajili ya kufanya yale ambayo tunaona hayatatusaidia na wala hayatawasaidia wakulima wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya yale mapendekezo ambayo nataka kuyasema, Mheshimiwa Mbunge mwenzetu wa Mtama wiki mbili zilizopita alikuja hapa na hoja ambayo kimsingi iko pending mpaka leo na ilikuwa pending kwa sababu Mheshimiwa Dkt. Mpango wakati tunamuita kwenye kikao cha bajeti aje atuambie liko wapi rejesho la fedha za wakulima ambazo zinafika takribani bilioni 81 bahati mbaya sana hakutokea kwenye vile vikao. Sasa leo anapokuja na mapendekezo ya kutaka kuchukua asilimia 100 ya fedha yote ambayo kimsingi ukisoma hiyo Finance Act ya mwaka 2010 inaeleza asilimia 35 itaingia Hazina, asilimia 64 itarudi kwa ajili ya kuboresha zao hili la korosho.

Mheshimiwa Naibu Spika, zao la korosho linaboreshwa kwa kununua mbegu, mbegu hizi zinapandwa kwa maana ya miche, wako watu mpaka leo tunazungumza hawajalipwa fedha zao za kazi ambayo wamefanya ya ku-supply miche. Pia tunatakiwa tujenge maghala mpaka sasa hivi hatujajenga kwa sababu fedha haijarudi. Mbaya zaidi napozungumza leo wananchi wanagawana mifuko ya sulphur kitu ambacho siyo cha kawaida na kitakwenda kuondoa kabisa uzalishaji mkubwa ambao tumeufanya kwa miaka hii mitatu kutokana na mabadaliko tuliyoyafanya. Sasa ukifikiria kuchukua asilimia 100 ya fedha hii kutoka kwenye sheria hii ambayo nimeitaja, Mheshimiwa Dkt. Mpango anakwenda moja kwa moja kudidimiza na kuua zao la korosho. Pia nimhakikishie kwamba anaenda kuwagombanisha wananchi wa mikoa inayolima korosho pamoja na Chama chao cha Mapinduzi kitu ambacho tusingependa kitokee. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tunampenda sana Rais wetu na tunaamini Rais wetu anatupenda sana sisi wananchi na ndiyo maana alisikiliza kilio chetu, naomba Waziri asirudishe nyuma jitihada za Mheshimiwa Rais katika hili. Waziri akifanya hivi, hata mimi Mbunge wa CCM nakwenda kuungana na wananchi wangu kupinga hicho ambacho anakwenda kukifikiria kukifanya lakini tunakwenda kusimama na wakulima wetu moja kwa moja kuhakikisha maazimio haya ya kwenda kuchukua asilimia 100 ya fedha hii hayawezi kufanikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ambalo nafikiri ni vizuri nikashauri na nimwombe Mheshimiwa Waziri kama nilivyomuomba kwanza aende kwenye takwimu. Bajeti tuliyomaliza au tunayomaliza 2016/2017 kwenye bajeti ya kilimo zaidi ya asilimia 10 tu ya fedha ambayo imeidhinishwa ilikwenda. Leo anaposema anaenda kuchukua asilimia 100 ya makusanyo ya korosho au ya mazao yote yaliyoko kwenye bodi na wakati asilimia 90 ya bajeti nzima haijaitekelezwa, ndiyo kusema kwamba hata hizi asilimia ambazo wanataka kuzichukua na kwamba zao hili litagharamiwa na Serikali Kuu tunaenda kufeli. Kwa sababu bajeti ya jumla peke yake tayari tumesha-prove failure, tumeshindwa kutoa fedha na hivyo leo kilimo tunachozungumza ambacho ndiyo uti wa mgongo wakulima wetu hawajaweza kunufaika nacho. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe sana Waziri kwamba zoezi la kwenda kuichukua hii fedha halitakuwa na tija kwa sababu hata hiyo bajeti kuu ya Wizara nzima tumeshindwa hata kufikia asilimia 50 ya utekelezaji wake. Tukichukua hii maana yake unaenda kuondoa moja kwa moja uzalishaji na unaenda kutudidimiza moja kwa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ambalo nilitaka pia nijaribu kumpitisha Mheshimiwa Waziri ni namna gani ambavyo ataenda kutueleza na ataenda kuwaeleza wakulima. Kwa miaka mitatu kuanzia mwaka 2005/2006, 2006/2007, 2007/2008 tuna zaidi ya shilingi bilioni 201 imekwama katika Wizara yake. Hela hii haijarudishwa na mpaka sasa hivi tunavyozungumza shilingi bilioni 10 tu pekee yake ndiyo imetolewa, tena yenyewe imetolewa kama mkopo kutoka NMB, kama ni mkopo maana yake ni nini? Wananchi wetu wanapaswa kulipia riba ya mkopo huu wakati fedha yetu ya ruzuku ambayo yeye ameshaichukua hajaturudishia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo anapoenda kuleta mabadiliko ya sheria na kutaka tubadilishe ili fedha iende Mfuko Mkuu atueleze fedha yetu ya miaka mitatu iko wapi na inaenda kufanya nini? Inafutwa au ndiyo sisi wakulima tayari tumeshadhulumiwa? Kitu ambacho kwa kweli narudia kusema, tena nasema nikiwa na utulivu wa hali ya juu Mheshimiwa Dkt. Mpango asitulazimishe, asitake kututia majaribuni kati ya sisi na wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hebu tuendelee kuwa watiifu kwa Taifa letu na kwa Rais wetu kwa sababu tunampenda na tunataka awatumikie wananchi. Katika hili Mheshimiwa Dkt. Mpango tunaomba sitisha mara moja zoezi la kwenda kuchukua fedha ya wakulima ambayo nyingine mpaka leo hujairudisha na majibu hujatoa leo unakuja na mapendekezo mengine ambayo kwetu sisi hayana tija na hayatatusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la lingine ambalo nataka nilizungumzie ni kuona namna gani ambavyo mapungufu ambayo wao wameyaona kama Wizara juu ya hoja walizozitoa wakati wanajibu kwamba kuna matumizi mabaya kwenye Mfuko wa Uendelezaji wa Zao la Korosho lakini solution haiwezi kuwa kwenda kuufuta ule. Nafikiri solution ilikuwa ni kufanya maboresho. Fedha ambazo wamezizuia maelezo yanayotolewa ni kwamba kuna matumizi mabaya ya honorarium na matumizi mengine, sisi hatuna tatizo katika hilo na tutaendelea kuunga mkono jitihada za Serikali kupinga matumizi mabaya yasiyokuwa na tija lakini hatuwezi kuzuia na kuua zao zima kwa ajili tu ya eneo moja ambalo tungeweza kulibana kwa maana ya kuwabana watu wa Bodi ya Korosho na wale watumishi ambao wanatumia fedha hii. Yale yanayohusu kununua miche, kufanya utafiti, leo Chuo cha Naliendele hakifanyi kazi yoyote, magonjwa yameanza kuvamia zao la korosho watu hawana fedha za kulipia kwa sababu fedha yote imeingia kwenye Mfuko Mkuu na hairudishwi. Sheria ambayo imetungwa ni ambayo sisi kama Wabunge tunapaswa kuisimamia na tunapaswa pia kuiheshimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikuombe sana lakini nimwombe Mheshimiwa Waziri Mpango hebu hapa tunapokwenda kuhitimisha zoezi hili binafsi sitamuunga mkono na naenda kupinga moja kwa moja wazo hili kwa niaba ya wananchi wangu ili tuhakikishe haki na hatima ya zao la korosho inaenda kuimarishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho atuambie, najua mapendekezo aliyoyatoa siyo kwa zao la korosho peke yake yako mazao mengine kama pamba, kahawa na mazao mengine. Hebu atoe takwimu ndani ya miaka mitatu kila zao ambalo amefikiria na lina bodi ni kwa kiasi gani mazao hayo yameingiza fedha katika Taifa letu? Kwenye kitabu chake kinaeleza pamba tumepata hasara, hapa anachoelekea kukifanya ni kwenda kuua pia zao la korosho ambalo linafanya vizuri kwa kisingizio cha kutaka kuchukua mazao ya Bodi nzima.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba niseme siungi mkono hoja mpaka pale jambo hili litakapokwenda kukamilika, ahsante sana.