Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Rehema Juma Migilla

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ulyankulu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. REHEMA JUMA MIGILLA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi hii nami niweze kuchangia kidogo katika hotuba ya bajeti ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimepitia vitabu hivi na kuvisoma kwa umakini sana, kimaandishi vitabu hivi vina maelezo mazuri sana, lakini kwenye utekelezaji napata ukakasi. Kiukweli bajeti ya mwaka huu haiakisi maisha halisi ya Mtanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivyo kutokana na sababu kwamba leo hii ukiangalia maisha ya kila Mtanzania ni magumu sana. Bado kuna Watanzania wanakula mlo mmoja kwa siku, lakini sokoni mfumuko wa bei ni mkubwa sana, vitu vinauzwa kwa bei kubwa sana. Sambamba na hilo, hata mzunguko wa pesa huko mitaani haupo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii wafanyakazi wanalia, hawana pesa; wakulima wanalia, hawana pesa; wafanyabiashara wanalia hawana pesa, halafu tunasema ni bajeti nzuri, huu ni uwongo. Bado katika vitabu hivi tunasema kwamba, eti bajeti hii ina lengo la kuondoa umaskini na kupeleka nchi kwenye nchi ya viwanda ilhali hatuyapi kipaumbele maeneo muhimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na matatizo hayo ambayo yanaikumba hii bajeti yetu, naomba Serikali sasa ifanye yafuatayo ili kuhakikisha maisha ya Mtanzania ambayo tunalenga yamwondolee umasikini yanafanyiwa kazi. Kwanza Serikali idhibiti mfumuko wa bei, bei ni kubwa sana, lakini pia kupunguza riba kwenye mikopo. Suala lingine kuwepo basi na nidhamu kwenye matumizi ya mapato yetu. Leo hii tunachokipanga siyo ambacho tunakitekeleza. Bajeti ya mwaka 2017 haijatekelezeka kwa asilimia zinazotakiwa, halafu leo tunaleta bajeti nyingine ambayo ni kubwa zaidi kuliko ya mwaka 2017. Naomba haya masuala yafuatiliwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo nataka kuongelea leo ni kutoongezwa kwa mishahara kwa wafanyakazi na kulipa madeni ya wafanyakazi. Suala la kuongezewa mishahara kwa hawa wafanyakazi siyo suala la mtu kupenda, ni la kisheria. Annual increment iko kisheria, lakini leo hii uongezaji wa mishahara kwa wafanyakazi imekuwa mpaka mtu apende. Jamani kwa nini tunakwenda kinyume na utaratibu wa sheria inavyotaka? Tunataka sasa pindi anapo-wind up atuambie hii sheria ambayo iliruhusu annual increment iwepo na mliitunga humu Bungeni inafanyiwa kazi kwa kiasi gani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni ulipaji wa madeni. Wafanyakazi wa Tanzania especially walimu, wana madeni mengi sana. Wana madeni ya arreas, likizo, tofauti na mshahara, lakini madeni haya hayalipiki kwa kigezo cha uhakiki. Hivi ni uhakiki gani ambao hauna kikomo? Serikali inatumia upenyo wa uhakiki kutowalipa watu stahiki zao. Tunaomba huu uhakiki uwe na kikomo, watu walipwe stahiki zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni ajira kwa vijana. Naipongeza Serikali kwa kutoa riba kwenye hii 10% ya maendeleo ya vijana na wanawake. Hata hivyo, kutoa riba haimaanishi kwamba ndiyo hawa vijana watakuwa wamekomboka kwenye suala la ajira.

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivyo, nikiwa na sababu kwamba Halmashauri zetu tumezinyang’anya vyanzo vikubwa vya mapato kiasi kwamba mapato yanayobakia yanakuwa ni madogo hali inayosababisha ile 10% iwe ndogo. Wanapoenda kwenye vile vikundi vyao wanapatiwa hela ndogo sana kiasi kwamba watu wanaamua kuacha pesa ile. Kwa hiyo, naomba sasa Halmashauri zirejeshewe vile vyanzo vyao vya mapato ili watu waweze kusaidiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine tujikite katika maeneo ya kipaumbele. Malengo ya bajeti hii yanalenga kuifikisha Tanzania katika uchumi wa viwanda, lakini tunaufikishaje uchumi wa viwanda ilhali maeneo ya kipaumbele kama kwenye kilimo, afya, elimu, tunayapelekea bajeti ndogo mno ambayo haitekelezeki? Naomba kilimo lipewe kipaumbele kwa sababu kwanza kinaajiri Watanzania walio wengi lakini pia kipelekewe pesa kwa wakati ili wakulima waweze kuwa na tija na kilimo chao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni TRA. TRA na wenyewe ni another disaster. TRA tunaamini ndiyo chombo chetu cha kutukusanyia mapato lakini wamekuwa ni mwiba kwa wafanyabiashara na kwa kila kitu. Leo TRA anakwenda kukagua na wanatembea na makufuli muda wote. Sasa kama wanatembea na makufuli muda wote, wafanyabiashara wataogopa kufanya biashara na wakiogopa, watafunga biashara zao. Wakifunga biashara hatuwezi kupata mapato ambayo tunayatarajia. TRA wanatembea mpaka kwenye ma-guest usiku, kweli! Mtawatisha hadi wawekezaji, tuiangalie TRA. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni kwenye kuboresha viwanda vyetu. Tuko kwenye nchi ya viwanda na tunaelekea kwenye Serikali ya viwanda. Viwanda tunavyo vingi sana lakini mpaka dakika hii havifanyi kazi, vimekufa. Tunaiomba Serikali yetu, kabla ya kuanzisha viwanda vingine iviboreshe vile vilivyopo na kama kuna wawekezaji ambao wanashindwa kuviendesha basi wapewe wazawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kodi ndogo ndogo ambazo ni kero kwa wawekezaji zipunguzwe. Mfano Mkoa wa Tabora kuna Kiwanda cha Nyuzi, kipo siku nyingi sana, kilikuwa kinatoa ajira kwa wakazi wengi sana wa Tabora. Kiwanda kile kimekufa na walipewa Wahindi na bado kuna wananchi wa Tabora wanadai pesa ambazo zilizotokana na kiwanda hiki. Kama kweli, tunataka tuboreshe ajira na tufikie uchumi wa viwanda, basi hivi vilivyopo kwanza vihakikishwe vinaboreshwa na hao wawekezaji wanapunguziwa adha ndogo ndogo ili waweze kuwekeza kwa umakini sana. (Makofi)

T A A R I F A . . .

MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Naibu Spika, siipokei. Naomba niendelee, nilindie muda wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mheshimiwa Waziri hawezi kutuambia kwamba eti tuanzishe viwanda vingine ilhali kuna vingine ambavyo vimekufa. Kwa nini tusifufue hivi kwanza? Leo uanze mradi mwingine wakati wa kwanza haujaukamilisha, ndiyo maana tuna-fail katika mambo yetu mengi kwa sababu ya kuanzisha miradi ambayo haitekelezeki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee. Suala lingine ni elimu bure. Elimu bure ina faida nyingi sana lakini hatukujiandaa. Tumeanzisha elimu bure ilhali hatujaandaa miundombinu ya kuhakikisha tunaenda sambamba na hii elimu bure.