Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Rwegasira Mukasa Oscar

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Biharamulo Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Kwanza kabisa, namshukuru Mungu lakini nampongeza Mheshimiwa Dkt. Mpango, Mheshimiwa Naibu Waziri na wataalam wake wote kwa kuandaa bajeti lakini kwa kufanya kazi nzuri. Kuna maeneo yenye upungufu, lakini natambua kuna kazi imefanyika vinginevyo Taifa lingekuwa limesisimama kabisa. Kwa hiyo, nawapongeza kwa kazi iliyofanyika lakini nitasema maeneo yale ambayo hayako vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, langu la kwanza mahsusi ni wigo wa walipa kodi, ndipo tatizo langu lilipo. Mwaka 2004, kama siyo 2005, Fernando de Soto’s ambaye Waziri anamfahamu vizuri kuliko hata mimi, alishiriki kuandika MKURABITA, alisema zaidi ya asilimia 90 ya shughuli za kiuchumi kwenye nchi hii zinafanya kazi nje ya sheria na shughuli za kijasiriamali asilimia 98 zinafanya kazi nje ya sheria na mbili tu ndiyo ziko ndani ya sheria. Alisema pia mali zetu kama ardhi na vinginevyo, asilimia 11 pekee ndiyo ziko ndani ya mfumo, kwa hiyo, ndiyo zinalipa kodi. Kwa hiyo, tuna wigo mkubwa sana wa mali na shughuli za uchumi ambazo ziko nje ya sheria hazilipi kodi. Kwa wakati huo alithamanisha shughuli za kiuchumi na mali ambazo ziko nje ya uchumi na hazilipi kodi, ilikuwa ni karibu mara kumi zaidi ya pesa yote ya nje, Direct Foreign Investment inayoingia nchi hii toka tumepata uhuru mpaka mwaka huo. Unaona kwamba ni uchumi mkubwa sana uko nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukilileta hili kwa muktadha wa sasa, nakumbuka tarehe 25 Machi, kama sikosei, Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli akiwa Morogoro, moja ya kauli zake alikuwa anawakemea TRA kufanya kazi kwa kuwa- harass wafanyabiashara. Naamini kabisa na ni wazi hakuwa anazungumza hivyo kwa maana ya kwamba tusikusanye kodi, lakini ukitafsiri hiyo ni kutafuta namna gani watu walipe kodi lakini wigo uwe mpana, tutafute kupanua ili watu walipe kiwango ambacho kila mtu anakimudu na kwa sababu ni wengi, tutapata tija zaidi kwa maana ya kodi na hakutakuwa na haja ya kukimbizana. Hiyo ndiyo tafsiri rahisi kabisa ya alichokuwa anakisema Mheshimiwa Rais. Sasa nikawa nafikiri hebu tujikite kwenye kutanua wigo wa kodi, ndiyo moja ya matatizo makubwa yaliyopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mmoja umetokea juzi hapa, mimi nimetafakari sana hii habari ya kupima samaki kwa rula. Nikawa nafikiri hivi habari ya samaki, ni kweli tunahitaji kusimamia sheria kwamba samaki wavuliwe pale ambapo wana viwango lakini hii habari ya kutanua wigo wa kodi na kusimamia sheria kwenye sekta mbalimbali tunahitaji kuviweka kwenye muktadha sahihi wa kila sekta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, nafikiri njia rahisi ni kutafuta namna ya ku- balance kati ya ufugaji wa samaki ili isaidie, watu wasijikite zaidi kuvua kwenye maziwa na bahari, wavue huko wanakofuga. Hii itakuwa imetibu mambo mawili; amezuia kila mtu kwenda kule lakini ameanzisha ajira ambako tutapata kodi, watu familia zao maisha yatakwenda na tutapata kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata habari ya mifugo, tumepiga kelele sana watu wa Kanda ya Ziwa. Nilisema na ninasema tena. Mimi sio mmoja kati ya watu wanaotetea mifugo wakae hifadhini lakini ni mmoja wa watu ambao sielewi kuwaondoa tu hifadhini ili kukidhi sheria, lakini hatutumii hiyo fursa kubadilisha hii mifugo ikawa ya kibiashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka kuna habari hapa imesemwa ya kugonga wale ng’ombe mihuri, nafikiri Mheshimiwa Rais wakati anatoa agizo hilo alikuwa analenga ni namna gani tujipange. Siyo lazima tukae kwenye kugonga mihuri, kwanza tunaharibu ile ngozi, tunapunguza thamani. Teknolojia sasa hivi iko juu, tena hapa hapa Tanzania, ukienda Sokoine tu hapo, Chuo Kikuu cha Kilimo, ng’ombe anamezeshwa chip, anatembea na chip yake, ukikaa kwenye kompyuta unamwona, unawahesabu ng’ombe 8,000 wako Biharamulo, akifa au akichinjwa unaona taa imezimika, unampa Afisa Ugani wako namna ya kudhibiti wa kwake, unajua nani kachinjwa, nani hajachinjwa, ni rahisi. Hebu tutafute ubunifu ambao utadhibiti watu wasiwe na ng’ombe wengi, lakini umedhibiti na umeweza kurasimisha na kutengeneza ajira na wigo wa kodi. Tupanue wigo wa kodi Mheshimiwa Dkt. Mpango, tatizo langu liko hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kwenye habari ya upangaji wa mipango yetu, haikai vizuri sana hapa, ingekaa kwenye Wizara ile ya Mipango, lakini ngoja niiseme ataona atakavyoiunganisha, ni habari ya sensa. Sensa yetu ndiyo inayotupa idadi ya watu ili kujipanga. Inafahamika duniani na hata sisi tunafahamu na Waziri anafahamu sensa ina upungufu, tena hasa ya kwetu ambayo mara nyingi kuna watu wanakimbia kwa sababu tofauti tofauti, tunashindwa kupata idadi kamili. Sensa iliyopita inasema Dar es Salaam ni watu milioni tano, lakini kwa hesabu ya kawaida tu, hata ukikaa ukiangalia, pale siyo milioni tano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano, watu wa NIDA wanaoandikisha vitambulisho vya Taifa, ukiangalia idadi ya namba waliyoandikisha mpaka sasa Wilaya ya Temeke peke yake ambayo wanaanzia umri wa miaka 18 kwenda juu na tukikumbuka demografia inasema kwamba umri wa miaka 18 kwenda chini ndiyo watu wengi, ndiyo base, ukilinganisha idadi hiyo ya umri wa miaka 18 kwenda juu na idadi ya sensa inayosema kwa Temeke, ni vitu viwili tofauti. Tutafute tuwe na idadi sahihi ili tuweze kutekeleza mipango yetu na majibu yapo hapa hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwezi Machi, 2018 nilikwenda Mkoa wa Songwe kwa Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa pale. Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe ametengeneza Daftari la Wakazi la kielektroniki, mnaweza ku-check hata kesho, akikaa mezani anaweza akabonyeza button anakwambia leo wanafunzi ambao hawakwenda shule watoro ni wangapi, siku hiyo hiyo real time. Mkoa wa Songwe, nchi hii, siyo nchi nyingine. Hebu tutafute namna gani twende tujifunze pale, watu wa NBS wakae watazame…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.