Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Abdallah Majurah Bulembo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. ALHAJ ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Niungane na wenzangu lakini awali ya yote nimpongeze Mheshimiwa Mpango, hongera sana, unajua mishale hii inavyopigwa ndiyo maana amekalia kiti hicho. Kwa hiyo, awe mvumilivu maana asingekikalia asingepigwa. Nimpongeze shemeji yangu Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kijaji, Ndugu Dotto, Manaibu wake wote, Makamishna wa TRA na wengine wote, hongereni kwa kufanya kazi katika eneo ambalo kila mtu anaangalia maana ni maeneo ya pesa hayo, hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa kwanza ni katika eneo la bima. Mwaka jana tulipitisha sheria hapa kwa ajili ya NIC lakini ndani ya bima hii kuna watu watatu. Kuna huyu mkubwa NIC, broker na agent. Mheshimiwa Mpango mbona broker hawa mnawaua? Kwa nini mnatoa maelekezo watu waende direct kwa insurer, hawa broker waende wapi? Leseni mnachukua, sheria iliyowaunda ipo, hamuwasaidii, kwa nini tunaiua hii industry? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Serikali inatakiwa ifanye kazi na mashirika mbalimbali lakini broker mmemuweka ninyi. Kama hafai basi naomba tulete sheria ya kumfuta na tukimfuta mniambie kama NIC ana rasilimali watu wa kuweza kuhudumia maeneo yote haya, hawezi. Nakuombeni sana, kama kuna waraka mmeutoa ule kwenye bima, huyu bwana mgeni wa bima huyu mwambieni aanze kusoma upya kidogo kwamba hawa broker bila kuwepo yeye hawezi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii ina miradi mingi mikubwa. Tuna ndege, standard gauge, tuna madude makubwa sana, kwa nini hamuweki kwenye clause za procurement zenu kwamba mwekezaji yeyote atakayekuja insurer atakuwa NIC? NIC kama hawezi ata-syndicate na watu wa nje lakini atapata pesa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri wakati anakuja kwenye ushauri wangu hebu walindeni brokers na agents. Kwa nini agent wanakuwepo, huwezi kukata insurance mahala popote, lakini mnaposema mtu aende direct hawa watu mnawaua.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ni ushuru wa stamp, dakika 10 ni kidogo. Sipingani na ushuru wa stamp nakubaliana nao lakini nina maswali. Kwanza miaka mitano ni mingi kwa mujibu wa hesabu, Waziri akija hapa atuambie kama ni mwaka mmoja au miwili tutamuelewa. Pili, tatizo ninalolipata huyu mtu akitengeneza lita moja na nusu analipa Sh.13,500, lakini chupa moja na nusu ile ina mia tano mara tatu, ukipiga hesabu yake Sh.13,500 ni Sh.40,500 na hawa wanywa maji ndio wengi zaidi kuliko hii lita moja na nusu, hesabu mbona haikubali? Tunapiga hesabu gani? Unaenda kwa mtu wa soft drinks unataka alipe Sh.13,500 kama anauza 150 haiwezi tena kuendelea kuwa Sh.13,500 itakuwa Sh.13,200. Kwa nini huyu mtu wa chini ndiyo tunamuumiza zaidi? Kwa nini tusielekee kwenye bia? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza hakuna soda ulishasikia ni forgery, hakuna soda ya kutengeneza mtaani, lakini hizi pombe kali hizi ndiyo zinatengenezwa magarasha mengi huku mtaani, kwa nini bei kubwa hii tusingeipeleka kwenye pombe kali? Kwenye mapendekezo yenu pombe kali mnaiweka mbali kidogo. Naomba tuelekee hapa ili tumsaidie mtu wa kawaida anayekunywa maji na soda aendelee ku-relax. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatukatai, kwenye Kamati ya Bajeti tumeangalia mtu huyu atapata hii hela kwa mwaka mmoja tu, hata tufanyeje capital anayoitumia na faida yake mwaka mmoja inamtosha, tunampa miaka mingi ya nini? Waheshimiwa Wabunge nawaombeni tuweke mguu chini, apewe mwaka mmoja au miwili, stamp hatuikatai baada ya hapo hii iwe shughuli ya TRA kiwe chanzo chao. Kwa nini tumtajirishe mtu mpaka mwisho na hizi hela anapeleka nje, hazikai nchini. Mheshimiwa Waziri tusaidie hapo.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nahamia kwa wakwe zangu kule Mtwara na Lindi kuhusu korosho. Hivi hii hela ya korosho ni yetu kwani? Serikali hii hela ni yetu? Tunaitaka ya nini? Kwa nini tutunge sheria kwa sababu tumeona kuna mapato? Hiki ni chanzo chao wapeni. Mkienda kwenye pamba chanzo chao wapeni, mkienda kwenye kahawa wapeni. Kwa nini Serikali tunaingia kwenye ugomvi ambao hauna msingi, msingi wa hizi hela ni nini? Kwa nini tuliue zao hili? Kwa nini tuue kahawa na pamba? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pesa hii siyo chanzo cha Mheshimiwa Dkt. Mpango, pesa hii inatoka kwa mkulima mwenyewe, sasa unaipangiaje bajeti, unaiwekaje kwenye Mfuko wa Pamoja? Jamani sisi tunakaa jukwaani kuomba kura, msitupe tabu kabisa. Yaliyotokea Mtwara tunayajua, tusijifanye kuna pamba masikioni. Tumefanyaje Mtwara kupata amani mnajua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kasema Mheshimiwa Bwege hapa mkaona kawaida, siyo maneno madogo hayo kwenye siasa, ni maneno makubwa sana. Lazima muende mbele mrudi nyuma, hela hizi kwa nini zitupe kero zinatusaidia nini? Nawaombeni Serikali sikivu mpo mnasikia, wote mpo hapa, nendeni mjadiliane, achaneni na hela ya korosho msituletee balaa, wapeni hela zao tuendelee na vyanzo vingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeletewa Sheria ya Serikali za Mita, nataka kuunganisha mambo yote lakini sasa nataka kuongelea asilimia 10. Tumeondoa vyanzo vingi kwenye Local Government, kuna Halmashauri haziwezi kuwalipa Madiwani posho zao na kuweka mafuta lakini hapa tunasema asilimia 10 wakipata tunaiundia sheria, nakuja na wazo jipya nini tufanye. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, twende kwenye Municipality za Dar es Salaam, Ilala, Arusha, Mbeya na Ilemela Mwanza hawa walipe asilimia 10 lakini zile Halmashauri ambazo zinashindwa kununua mafuta, Serikali kwa sababu mmechukua vyanzo m-top up pale asilimia 10 muipeleke kama ruzuku kule chini ili akina mama na vijana wakope. Haiwezekani Halmashauri inakusanya shilingi milioni 100 posho za Madiwani na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa haziwezekani halafu tunawaruhusu kwamba kweli kila Halmashauri itoe asilimia 10 kwenye chanzo gani? Kuna vyanzo gani mmebakiza huko? TARURA, mabango na property tax mmeondoa, hakuna kitu kule. Kwenye Municipality na Majiji kwa sababu kuna watu wengi inawezekana lakini huku chini siyo, naomba mrudi nyuma muangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naongea hapa nikiamini mwaka kesho ni mwaka wa uchaguzi, tusipate tabu za lazima hapa kwa sababu ya bajeti. Halmashauri hazijiwezi, hazijiendeshi wapelekeeni ruzuku ya 10% ili mikoa, wananchi na halmashauri zote wawe na uwezo wa kukopa asilimia
10. Tusitoe mfano wa Kinondoni au Ilala ukafananisha na Katavi na Tunduru, havifanani! Nchi hii iko tofauti na mapato yapo tofauti. Kwa hiyo, hiyo asilimia 10 huko juu muiangalie tuwapelekee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye michezo ya kubahatisha kuna Bahati Nasibu ya Taifa haipo katika nchi yetu, ipo hatujui inafanya kazi wapi. Kwa nini Bahati Nasibu ya Taifa tunaitoa 6 kuipeleka 10, tunataka nini? Bahati Nasibu ya Taifa sehemu nyingi zilizoendelea ukienda Ghana, Nigeria na sehemu nyingine chanzo hiki ni cha Serikali Kuu kwa maana ya Wizara ya Fedha. Ninyi mnatakiwa mtafute anayeweza mkae naye lakini huyu akipatikana atatengeneza nchi nzima kwa sababu ata-invest mtaji wake. Kwa nini mnamzuia kabla hajaja, tunaweka hiki chanzo cha nini, kwa nini tunaongeza hela hapa? Tutakosa watu wa kuja kufanya kazi hii na hii hela ni ya Serikali. Chanzo hiki kingekuwa kinafanya kazi vizuri mngepata hela nyingi za bure pale zipo, lakini mkiongeza kodi wawekezaji watajikata, itakuwa shida. Kwa nini msikubaliane katika hili?

Mheshimiwa Mwenyekiti, namalizia kwa kusema ninyi watu wa Mifugo muende pale Masaka Uganda ukifika Lukaya wanafuga bycatch, mjifunze wenzenu wanafanyaje muache kutembea na rula.