Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Ali Hassan Omar King

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Jang'ombe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nakushukuru kunipa nafasi hii kuchangia bajeti hii ambayo ina mwelekeo mzuri sana katika nchi yetu hii, hususani katika miundombinu ambayo itatuondoa hapa tulipo na kusogea mbele zaidi. Pia napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai na uzima kuweza kusimama hapa kuzungumzia juu ya suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zamani kule ilikuwa mtu akitaka kubebesa ikiwa ile mistari ya kubebesea imemshinda basi huwa anatafuta maandiko matakatifu aidha aya za Quran au anaweza akatumia hata mistari ya Biblia ili kubebesea. Wakati mwingine ujue mtu kama huyu anakuwa ameshaishiwa. Kwa hiyo, wakati mwingine watu wanaotumia hizi aya inakuwa sivyo wanazitoa katika mantiki yake kwa sababu tu ya kutaka kuhalalisha neno analotaka kulisema, naomba hili tujaribu kuliangalia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali hasa kwa marekebisho ya bandari, ikiwemo Bandari za Dar es Salam, Mtwara lakini pia na mipango iliyopo kwa ajili ya Bandari ya Tanga. Bandari inachangia zaidi ya asilimia 70 ya pato letu au ya kodi zinazokusanywa, bidhaa nyingi sana zinapitia bandarini, kwa hiyo naipongeza Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa kuwa tunazifanya hizi bandari zifanye kazi vizuri na tunazirekebisha, tuzidi kufanya kazi katika miundombinu iliyobakia kama reli na barabara ili huo mzigo unaopokelewa ufikie vizuri. Huo ni ushauri wangu baada ya pongezi hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi nyingine ni katika kuimarisha Shirika la Ndege. Sawa ndege zetu zitakuja na zitakuwepo, lakini pia naipongeza Serikali kwa kuimarisha viwanja vya ndege, kuna viwanja vya ndege14 ukisoma katika hotuba ya miundombinu vitafanyiwa marekebisho na zaidi vitawekewa taa za kuongozea ndege. Hapa naishukuru Serikali lakini ilifanye hili kwa haraka kwa sababu wasipolifanya kwa haraka ina maana tutapoteza vitu vingi sana au mapato mengi sana kutokana na ndege zetu kulala jioni, ikifika jioni zinalala. Kwa hiyo, viwanja vya ndege tukiviimarisha ina maana hapa ndege zetu zitafanya kazi vizuri hata wakati wa usiku na itapunguza muda wa kulala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni hili ambalo limezungumzwa katika Wizara tano, suala la VAT ya bidhaa zinazokuwa manufactured Tanzania Mainland ambazo zitapelekwa Zanzibar. Tulifanya marekebisha mwaka 2016/ 2017 katika Finance Act tukaweka zero rate. Tumeweka zero rate lakini kwa mtu ambaye atanunua kwa manufacturer na zero rate kwa mtu ambaye ni VAT registered. Mheshimiwa Waziri hili suala analifahamu sana, tumelizungumza hapa siku ya Wizara ya Muungano ilikuwa kama ni changamoto, kama changamoto hii haijapatiwa ufumbuzi inageuka inakuwa kero.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Finance Bill ya safari hii hatujaona hili suala. Zanzibar kule watu wanatozwa VAT asilimia 36; asilimia 18 anatozwa original na asilimia 18 anatozwa kule kwenye destination. Tatizo hili lipo katika ile sheria, kwa nini tusiondoe utaratibu huu tukarudia ule utaratibu wa marejesho kama ilivyokuwa zamani? Kwa sababu tukisema tunataka tutumie destination principle ina maana kwamba tuendane na vitu vinafuatana navyo. Mheshimiwa Waziri ni mtaalam zaidi katika masuala haya, hili suala linawaudhi wananchi wetu wa Zanzibar. Zanzibar hakuna mashamba, Zanzibar kuna wafanyabiashara. Kwa hiyo, wafanyabiashara hawa ukawawekea kikwazo ina maana kwamba maisha ya watu yanakua mabaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili suala linakosesha mapato Zanzibar na Bara, pia linasababisha magendo yawe makubwa zaidi na wafanyabiashara na mitaji yao itakufa. Kwa hiyo, naomba hili suala lifuatiliwe na litolewe ufafanuzi. Mimi nimeuliza Zanzibar wamesema hawajatoa ushauri kabisa katika suala hili na lilishazungumzwa kama kero mpaka mbele ya Rais wetu Mtukufu na hapa tumelizungumza sana lakini halijafanyiwa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni Electronic Tax Stamp. Suala hili kidogo naona kwangu liko kinyume zaidi. Kwanza siyo economy, fedha za kukusanyia ni kubwa zaidi kuliko kodi inayoenda kukusanywa kwa lita. Yaani lita Excise Duty yake ni ndogo kuliko gharama za kukusanyia hizo fedha zenyewe, kwa hiyo siyo economy.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine, nimejaribuni kulinganisha jedwali tumeweka Excise Duty kwa bidhaa ambazo zitatoka nje za vinywaji, ukija ukapima moja kwa moja ukihesabu ile gharama itakayoongezeka ya hii Electronic Tax Stamp ni kubwa kuliko gharama ambayo tumemtoza yule ambaye atatoa hicho kinywaji nje. Tukitazama katika majedwali haya tutaona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala hilo pia tumesema kwamba kuna mkataba, huu mkataba haiwezekani ikawa ni kikwazo cha kutoondoa maamuzi haya. Kwa sababu mtu unaweza ukaozesha mtoto ikawa siyo wako. Kwa hiyo, ukiozesha mtoto siyo wako ina maana kwamba lazima mkataba huo ufe au cheti hicho cha ndoa hakikubaliki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nitolee mfano mwingine hata sumu mtu anapokunywa huwa anapewa maziwa. Kwa hiyo, kama tumeshaingia katika mkataba huu naomba tungejiondoa kwa sababu hauna maslahi kwa wananchi, walaji ndiyo watakaolipa gharama hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia huyu vendor ambaye tunataka kumtumia Kenya tayari amekuwa suspended, kwa nini tunataka kumtumia? Kingine, kuna regulation tayari zilishatengenezwa. Kwa hiyo, ni sawasawa na kwamba tuko katika hatua ya kuvalishana pete halafu mtoto anazaliwa ina maana mtoto alizaliwa kabla ya ndoa, sasa hiki kitu naomba kiangaliwe. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni tax amnesty ambayo Mheshimwa Waziri amepewa uwezo katika Tax Administration Act, section 70. Naomba mngeshauriana na mngeshauriana na Zanzibar, kwa sababu Zanzibar wanakusanya kodi income tax zinabakia kule kule. Ukisema Waziri wa huku unazisamehe na katika sheria Minister siyo Minister responsible for Finance wa Zanzibar inakuwa ni yule wa Tanzania. Kwa hiyo, naomba mngeshauriana nao kwa sababu mnaweza mkasamehe kitu huku lakini kule kikaleta impact katika mapato ambayo yanatakiwa yakusanywe katika penalties, interest na mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuhusu tozo ya maji ya Sh.50. Tumeona ugumu wake, tutumie ile bird in the hand fallacy, mwenzetu Waziri ni Mchumi, ndege mmoja aliye mkononi ana thamani zaidi kuliko mia ambao wanaoruka katika mbuga au katika msitu au sehemu nyingine yoyote. Waswahili wanasema moja shika, siyo kumi nenda uje. Kweli Serikali imesaini mikopo hata juzi tumeona katika TV kutoka Ufaransa, lakini sasa hii ni ya kwetu, tukikusanya tutapata pesa yetu, hii ndiyo ile moja ya kwetu, moja shika siyo kumi nenda uje. Ndege huyu yuko mkononi ana thamani zaidi. Naomba hilo tulijali na tuweze kulisisitiza liwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe hongera kwa Serikali kuhusu taulo za kike. Ni sawa tunaipa hongera Serikali lakini taulo hizi za kike pia kuna baadhi ya bidhaa zinafungamana nazo navyo vingeweza kusamehewa. Kuna equipment’s na materials pengine yanakuwa imported,hivi navyo pia tungejaribu kutizama ili tukapata uwanja mpana ili hili jambo likawa zuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo napenda kulizungumzia ni kupunguza Income Tax kwa kampuni za wazalishaji wapya wa madawa. Naomba pia ingekuwa ni busara mkawashauri na wale wa Zanzibar kwa sababu makusanyo ya Zanzibar yanakusanywa Zanzibar na yanabakia Zanzibar. Kwa hiyo, ukisema huku ushasamehe hivyo watu wanatafuta loophole na anaweza akapenya na pengine inaweza ikaja ikaathiri. Kwa hiyo, namuomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja ajaribu kutueleza, je, makubaliano yapi yalifikiwa katika suala hili? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo napenda kulizungumzia ni makusanyo ambayo Serikali Kuu itakuwa inakusanya kila kitu. Kusema kweli hapa kidogo inaweza ikatupelekea katika nafasi mbaya sana ya kiuchumi. Ina maana kwamba ukifeli upande mmoja kila kitu kinaharibika. Kila kitu kikiharibika ina maana lawama zote zitakwenda Serikali Kuu. Tujaribu kutazama hii diversification inasaidia, tukiwa na portfolio ya kukusanya mahali na kutumia katika maeneo mengine atleast inapunguza zile risk za kukwamakwama. Kuna vitu vingine utendaji wake utakuwa unakwama kwa sababu mapato yote yanakusanywa upande mmoja. Kwa mujibu wa sheria hii inayotaka kutumika sasa hivi, imewekwa baada ya siku moja kama fedha hazijatumika fedha zitarudi. Je, zitarudishwa tena kwa muda gani au ziombwe tena vipi? Kwa hiyo, hili naomba Serikali ijaribu kulitazama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuhusu korosho, asilimia 65 ya korosho katika export levy. Hili at least lingekuwa linafanyika kama lilivyopangwa, kwamba zirudi kwa wakati vinginevyo, jamaa zangu wa Kimakonde wana msemo mmoja wanasema kwamba, ‘Channumbile Nnungu Cha Kumemena’, ina maana kwamba kila kilichoumbwa na Mungu kinaliwa tu. Hizi asilimia 65 ikiwa haturudishi tukamemena hukuhuku tutawapa taabu na hili zao halitakuja kustawi tena. Tumetanua wigo wa zao, tumeongeza mikoa, sasa hivi hatuko Kusini peke yake tunakuja Kanda ya Kati, tunakwenda na Magharibi, kwa hiyo, tutazame kwamba hili jambo linaendaje katika huu ushuru wa korosho ambao unakusanywa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja na Serikali ijaribu kuangalia ushauri ambao tunaipa. Nashukuru.