Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nominated
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Awali ya yote nichukue fursa hii kuwapongeza ndugu zangu walioko Wizara ya Mambo ya Ndani Mheshimiwa Mwigulu, Naibu wake Mheshimiwa Masauni, Katibu Mkuu Wasaidizi wao wote, Makamishna Jenerali walioko hapo juu, Ma-RPC, Maafisa Uhamiaji katika Mikoa. Wizara nzima nawapongeza sana kwa kazi kubwa mnayoifanya kutulinda katika nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na hili la ulinzi hasa polisi, wachangiaji wengi wamesema nani halindwi, nani kafanyiwa hivi, nani kafanyiwa hivi, mimi nataka niende Kibiti tu kidogo. Polisi walifanya kazi kubwa sana Kibiti inatakiwa tuwapongeze wote tuliomo humu ndani. Kazi yao waliofanya ni kubwa, ilifika mahali mtu ukitaka kwenda Kibiti inabidi utafute polisi wa kukusindikiza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ndani wengine walimaliza kusema kwamba sisi Serikali haitutaki, haiwi hivi nataka kuuliza swali moja hasa kwa Wabunge, askari polisi mmoja anapokufa ni kwamba alikuwa vitani, Kibiti wamekufa askari kama sikosei kati ya 20 mpaka 25 haikutugusa, haionekani kama walikuwa vitani, wakapata shida na wala hata humu ndani hatukuitana kuchangiana hata elfu kumi kumi ya kusaidia familia zao. Ni watoto wetu wale! Ni wapiganaji wa nchi hii ndiyo kiapo chao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunakaa hapa kuna watu wanabeza polisi. Hata ukiwa na Mmasai anakulinda huwezi kubeza polisi. Wasemaji wamesema polisi ni professional, haiwezekani kila mtu anaweza kwenda nyumbani akavaa akaitwa polisi. Kwa nini tunawafanya watu wa kawaida polisi? Naomba Waheshimiwa Wabunge polisi pamoja wanalipwa kwa kodi zetu hata nyie Wabunge humu mnalipwa kwa kodi ambapo hata polisi anakatwa makato yake, si ndiyo? Maana yake leo mtu anasema kodi yetu, nani halipwi kwa kodi? hata sisi mshahara tunaopata ni kodi ya polisi ipo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, suala hili ni letu sisi wote, lakini wachangiaji wanasema polisi kwa kodi zetu, kodi ni yetu sisi wote kama polisi anavyolipwa mshahara, kama wewe unavyolipwa posho, tuna haki ya kuthamini polisi. Naendelea kusema tukitoka nje hapa tunalindwa na polisi, popote unalindwa na polisi, lakini polisi hawa hatuwathamini wala hatuwapi value. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kwamba, napenda niwapongeze matrafiki wote Tanzania wanaofanya kazi ya usalama barabarani. Sisi Wabunge tukienda na magari yetu traffic akikusimamisha, unasema naitwa Mbunge, kwani ukiitwa Mbunge ndio uvunje sheria? Nani amekwambia kuna mahali imeandikwa Mbunge avunje sheria? Tunawadharau wale watu hatuwapi haki, hata kama wewe ni Mbunge una haki nayo, basi simamisha gari msikilise jieleze mpe thamani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa Mheshimiwa IGP Sirro, hawa Wabunge wanaofanya makosa barabarani wakienda wawapeleke mahakamani. Ndiyo, kwa kuwa hakuna mahali mtu ameambiwa avunje sheria, sheria hii inatuhusu sisi wote. Unaona watu wanafanya vitu vya ajabu eti kwa sababu wanatumia nembo ya Ubunge, Ubunge siyo certificate ya kwenda kufanya makosa kwa kuwadhalilisha wenzetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niingie sehemu ya pili upande wa polisi, polisi kuna ile kitu wanaita Police General Order kwa maaskari wetu, wanakaa miaka 12 ndio wanaingia kwenye ajira, hii nyingine ni mkataba mkataba. Nafikiri wangefanya utarabu tulete sheria huku au tufanye marekebisho tuwape nafasi yao. Kwa sababu kama tunafanya hivyo hapa katikati wakiondoka kuna mambo mengi wanayapoteza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye upande wa polisi niende suala lingine ambalo ni gumu. Kwenye kitabu cha bajeti cha Waziri hapa nilipoangalia kwenye eneo la maendeleo kwenye ukurasa wa 51, polisi wamewapa hela kidogo. Pale Makao Makuu ya Polisi kuna jengo fulani pale linajengwa miaka mingi forensic bureau haliishi, kwa nini Mheshimiwa Mwigulu jengo hili haliishi? Kwa nini kwenye bajeti hii hatulioni? Jengo hili ni muhimu sana kwa nchi za wenzetu kwa sababu gani, mtu akipata ajali, mtu akiuawa usiku kuna mahali anapelekwa ajue, mitandao ipo, tutakwenda kuangalia wapi, kwa nini jengo hatulipi bajeti? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo matatizo mengi katika nchi hii watu wanauawa, watu wanaonewa, watu wananyang’anywa mali zao, lakini hawana mahali pa kwenda. Naomba Mheshimiwa Mwigulu wakati akija hapa anijibu forensic bureau ya Makao Makuu pale inakwisha lini? Huo mradi ni mkubwa sana katika nchi za wenzetu, huwezi kutambua jambo mpaka uende kuazima kwa rafiki yako itakuaje. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba sana, inawezekana hatuoni umuhimu, lakini nina uhakika eneo hili ni muhimu. Hawa watu wenu wa Kibiti wangekuwa wanapatikana, mitandao ya simu ingekuwa inapatikana polisi wajitegemee wenyewe, kwa nini wawe na mawazo ya kupiga hodi kwa watu wengine? Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri akija nafikiri majibu yake yatakuwa mazuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee Uhamiaji. Kwanza nichukue fursa hii kumpongeza sana Kamishina wa Uhamiaji, hongera sana mama, ameonesha mabadiliko, anafanya kazi. Pia katika pongezi hizo nimpongeze tena Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani niliuliza hoja hapa Bungeni kuna vijana wetu walifukuzwa pale polisi kwa kufoji viza, yule aliyesababisha wafoji viza akapigwa PI Uhamiaji wakawa bado wanamshikilia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nampongeza Naibu Waziri na Jenerali wa Uhamiaji, yule mtu baadaye walikamilisha utaratibu akarudi kwao, basi watoto wetu wamefukuzwa na yeye ameenda kwao. Kwa hiyo, nawapongeza sana kwa usikivu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini uhamiaji kuna tatizo, tena si dogo kubwa sana. Namwomba Kamishna atoke Ofisini, atembelee Mikoa ya Tanzania yote ajue pamekaaje. Kwenye border kuna shida, kuna shida sana ukienda Namanga, ukienda Mtukula, ukienda Songwe pale kuna shida kubwa. Pamoja na hayo kila siku tunawakamata Waethiopia, tunawakamata Wasomali, lakini humu ndani kuna watu wanaishi bila utaratibu na wako wanalindwa na Uhamiaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliuliza swali hapa nikasema kuna mtu amekuja hapa nchini anaitwa Mhasibu, leo ni group Meneja miaka 20, anaitwa Vedagiri yuko kwenye kampuni ya Alpha Group. Mtu yule anaishi kwa utarabu gani lakini niliposema neno lile kuna Wabunge humu niliwagusa wenye matakwa na watu kwa sababu ni wafanyabiashara wakubwa nafikiri wana mambo yao pale wanayoyafanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoongelea ni Utanzania kwenye uhamiaji. Baada ya kumtaja huyo nimeletewa wengine zaidi ya 20, wanaishi humu wanaonekana kama Watanzania, lakini hatuwafuatilii! Ukienda kwenye Idara ya Uvuvi, Mheshimiwa Mwigulu nimewaambia waanzie Mtwara mpaka waje Singida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi kweli Watanzania hawana uwezo wa kuuza bucha za samaki? Hawa Wahindi wanaouza bucha za samaki wanawapa vibali gani? Uhamiaji wanawaona? Ni Wizara ya kazi ndiyo wanashirikiana na Wizara hizi ni mtambuka, lakini kazi haiwezi kuwapa kibali mpaka uhamiaji waseme anatakiwa kuwepo nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa eneo la Uhamiaji kwa nini wanashughulikiwa Waethiopia, Wasomali, ndiyo wanaguswa huku, lakini hawa wengine tunaoishi nao nchini kwa sababu wana mapesa, wamekaa zaidi ya miaka 20 mpaka wanaingia kwenye siasa zetu nani awe CCM, nani awe CHADEMA, wanawaangalia tu hawasemi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili sasa namkabidhi Mheshimiwa Waziri, Kamishna Jenerali hajashindwa inawezekana alikuwa hajui wakae mezani wanipe majibu. Bahati mbaya nikilisema nitaenda nalo mpaka mwisho kwa sababu sitaliacha kama sitapa majibu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanawalinda Wahindi humu, hawana vibali, hawana nini, wanakamata Wasomali akina Bashe waliozaliwa nchini, ndiyo wanahangaika nao. Akiguswa mtu wewe njoo, wewe njoo, lakini hawa wanaotoka nje hawafanyi nao kazi kwa nini? Uhamiaji ni pazuri, siwezi kumsema Jenerali huyu mpya ana siku chache, lakini pale kuna mizizi mibaya, ukienda sehemu ambako kuna wakimbizi, ukienda sehemu ambazo zina mipaka watu wa Uhamiaji wale ni hatari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niulize kati ya Uhamiaji na Polisi; nimeona IGP Sirro mwili wake mzuri, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji mzuri, Magereza mzuri, hawa wenye vitambi vikubwa vinakaa kwenye meza kuliko vyetu ni mapolisi kweli au…
(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)