Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Maryam Salum Msabaha

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia kusimama katika Bunge lako hili Tukufu na leo ikiwa ni siku Al-jumaa kwa hiyo Insha Allah Mwenyezi Mungu atasimama na mimi, nitakayoyaongea, Serikali itayachukua wayafanyie kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote niwape pole viongozi wangu wote ambao wamepitia misukosuko kwenye Jeshi la Polisi na ambao hata wengine sasa hivi wapo magerezani wanatumikia vifungo na wengine ambao wapo kwa mashtaka mbalimbali ndani ya magereza. Niliwahi kusema hapa ndani ya Bunge hili, nikasema sheria za wafungwa na magereza na haki zao zifuatiliwe na wapate faragha ya kukutana na wapenzi wao, sasa viongozi wote tunaelekea huko huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia suala la haki za raia na vifo vinavyotokana na ukatili wa Jeshi la Polisi. Si vibaya ndugu zangu kuwasema kidogo na kuwakosoa kidogo, polisi unavyoenda kupambana na raia, raia hana silaha na najua Jeshi la Polisi wamefundishwa namna ya kupambana na raia ambaye hana silaha na ambaye hawezi kukuhujumu wewe na kuna viungo maalum ambavyo wamefundishwa namna ya kupambana na hawa raia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi naona wanakokwenda si kuzuri, wanakamata watu, wahalifu, wahalifu hawana silaha, mhalifu hana chochote, hana hata sindano, lakini kinachofuatia anapata kipigo ambacho ni kitakatifu. Akishapata kipigo kile ambacho kimemsababishia maumivu, wanampeleka wanaenda kumweka lockup au rumande, kokote kunakostahili kuwapeleka watu wale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sasa hakuna matibabu, hapa wanakiuka haki za binadamu na sitaki muende huko. Raia, askari huwezi kufanya kazi, hasa Kitengo cha Upelelezi bila kuwa na rafiki raia ambaye ni mwananchi, ndiyo na wewe unapata uafueni wako wa kufanya kazi. Taarifa utazipata wapi? Taarifa lazima uzipate kwa kupitia kwa raia na ndiyo maana tunasema polisi wasijenge uhasama na wananchi wasiokuwa na silaha, wasiokuwa na mbinu za kutumia silaha, ni lazima wajenge urafiki ambapo na wao wapate wepesi wenu wa kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, askari wetu wana changamoto, kuna wengine wana vyeo lakini stahiki zao hazilingani na vyeo vyao. Niiombe Serikali iongeze mishahara na iangalie namna gani wanavyopandisha madaraja ya maaskari hawa nao wapate stahiki zao, sio kuwatumia kwa matukio tu mbalimbali bali nao wapate stahiki zao ili wapate kufanya kazi kwa weledi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo waende labda Marekani waangalie askari wanavyofanya kazi. Waende japo hata Kenya wakaangalie askari wanavyofanya kazi, wanafanya kazi kwa kuipenda, kwa hiyo askari wetu wasifanye kazi kwa kulazimishwa kuifanya ile kazi na sidhani kama kuna wanasiasa ambao watawafundisha kufanya kazi zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanavyokamata wahalifu, wale wahalifu wakishawakamata, ambaye labda kesi hii kaifanya kweli kweli, mpe ile kesi ambaye anastahili kupewa kesi ile, wasimbambikizie kesi. Haya mambo ya kuwabambikizia wananchi kesi, wananchi sasa wanafika mahali wanajenga hofu na Jeshi la Polisi. Wakumbuke bado askari wengi hawajajengewa nyumba, wanaishi uraiani, watoto wao wanasoma uraiani. Tunajuana Watanzania, kwa hiyo, wakijenga mazingira yale, kinafika kipindi sasa na Watanzania nao watakosa uvumilivu kwa sababu wataona, kwa nini mzee wangu kafanyiwa kitendo hiki? Kwa hiyo, mtoto anakuwa anajenga chuki na Jeshi la Polisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mahabusu; mahabusu wana haki kama binadamu wengine, lakini sasa mahabusu hawa wanavyopelekwa huko mahabusu, unakuta kwa kweli mahabusu wanakaa dirisha lile ni dogo sana, japo wamefanya makosa. Wengine nimesema wanakuwa wanabambikiziwa makosa, wote wanaokwenda kule mahabusu sio wote wana hatia, sasa unakuta kule mtu analetewa chakula, choo chake kiko pale pale, mazingira sio rafiki na mahabusu. Mlo wake anapata mara moja, hao wengine pia hawana ndugu wa kwenda kuwaangalia kule kuwapelekea chochote. Wale askari ambao wanakaa na wale mahabusu, hawana fungu la kuhudumia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niiombe Serikali ihakikishe sasa wanatenga bajeti ya kutosha. Hii bajeti ambayo tunaisimamia ndani ya Serikali tuhakikishe inapelekwa kwa wakati muafaka ili angalau sasa Serikali na askari hawa ambao wanahusika na mahabusu, mahabusu nao wapate haki zao, kwa sababu unavyomkamata mhalifu sio wahalifu wote wanandugu, wahalifu wengine hawana ndugu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuangalie, kuna wale watu ambao wanakamatwa na makosa madogo madogo. Yale makosa madogo madogo tunaweza kuangalia sasa wale ambao wanapelekwa magerezani, wanajazwa magerezani tukaangalie zile kesi za kuku, kesi sijui za nazi, hawa wapewe adhabu ndogo ndogo ili kupunguza msongamano wa magerezani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nitaongelea kuhusu Chuo cha Mafunzo Ziwani. Hiki Chuo cha Mafunzo Ziwani ni chuo kizuri sana na ni chuo cha zamani na wengi wanatambua. Hiki chuo jamani naona wamekisahau kwa sababu wako askari wengi nao wanatoka huku bara wanapangiwa kwenda Zanzibar. Hata hivyo, sasa hivi hiki chuo kinapoteza hadhi, chuo hiki kiko tangu enzi za mkoloni, tangu enzi za muasisi wa Taifa lile, Mzee Karume lakini zile nyumba ni za siku nyingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale kuna hospitali, hospitali ile sio inahudumia tu polisi na familia zao, hapana! Hospitali zile zinahudumia mpaka raia ambao wanatoka pembezoni ambao ni majirani wa chuo hiki. Sasa naomba Serikali wahakikishe wanavyotenga bajeti, bajeti hii wahakikishe na upande wa pili inavuka ili kutatua zile kero ambazo zinakabili chuo hiki cha Ziwani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Polisi Mikese, kiko barabarani. Nimshukuru afande ambaye ni Mkuu wa Kituo hiki, amekuwa msaada mkubwa sana, wangeangalia ni namna gani hata waweze kumwongeza angalau chochote. Mheshimiwa Mwigulu, huyu askari amekuwa hana itikadi ya kazi, anafanya kazi yake kwa weledi mzuri sana, lakini kituo hiki ni cha tangu enzi za Mjerumani. Pale hakuna gari na pale pamekuwa panatokea ajali mara kwa mara na hata viongozi wengi wamekuwa wanapata ajali sana pale ile barabara ya Mikese, si usiku, si mchana. Sasa kituo hiki hakina nyenzo, kituo hiki ukiangala kinavuja, waende siku za mvua waangalie pale panavyovuja, panavuja, majengo yote yanavuja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Askari wanafanya kazi katika wakati mgumu, hakuna magari ambapo utasikia ajali imetokea labda Morogoro kwa mbele kule, wanatakiwa watoke pale kituoni, wafuate majeruhi, au kuna wengine wamegongana na pikipiki, lakini gari hakuna, mafuta hakuna, nyenzo hakuna. Unakuta sasa wengine wanatoa pesa zao mfukoni, tusifike huko.