Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kinondoni
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MAULID S. MTULIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema kwa kunijalia uzima na kuweza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii, lakini nianze kabisa kwa kuwashukuru Watendaji Wakuu wa Wizara hii, kaka yangu Mheshimiwa Mwigulu Nchemba na kaka yangu Yussuf Masauni kwa kazi nzuri wanayofanya ya kuhakikisha nchi yetu bado ipo na ulinzi na usalama na amani ya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Kamanda Sirro, Kamanda wangu wa Mkoa wa Kanda ya Dar es Salaam, Mambo Sasa na Kamanda wangu wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Kamanda Jumanne. Kwa sisi ambao tumetoka kwenye hekaheka za chaguzi muda siyo mrefu tunajua umuhimu na thamani ya kazi za Watendaji wetu wa Ulinzi na Usalama. Kwa kweli nawapeni pongezi nyingi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuwa mkweli. Nimefurahishwa sana na nimejifunza kitu kikubwa sana kutoka kwa kiongozi wangu, Mbunge mwenzangu Mheshimiwa Mchungaji Msigwa alipokuwa anaongea mbele ya Mheshimiwa Rais. Kwa kweli nimejifunza kwamba sisi kama Wabunge, kama Wanasiasa pamoja na hitilafu zetu za Vyama, pamoja na tofauti zetu bado tunahitaji kuheshimiana. Nam-promise kwamba kwa kuwa amemheshimu kiongozi wetu wa nchi, amemheshimu ni kiongozi wangu wa Chama nami nam-promise nitamheshimu kiongozi wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na mchango wangu katika Jeshi la Polisi. Pamoja na kazi nzuri wanayotufanyia Polisi wetu, bado wana changamoto nyingi. Kwetu pale Dar es Salaam bado tuna changamoto ya vituo chakavu vya ofisi za vituo vidogo vya Polisi, tuna changamoto ya samani za Watendaji wetu wa Polisi na changamoto ya usafiri. Polisi pamoja na Magereza wote wana changamoto ya usafiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaambie wenzangu, bajeti hii sitegemei upande ule kule kwamba wataikataa kwa sababu itaenda kutatua matatizo ya kuongeza magari. Tuliona lilitokea tatizo hapa, kiongozi wetu na wale baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wenzetu watuhumiwa walicheleweshwa kwenda Mahakamani wakakosa dhamana ikabidi walale ndani kwa sababu ya kukosa magari na mafuta.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namna nzuri ya kuondoa tatizo lile ni kupitisha hii bajeti ikawa ni bajeti ambayo inaenda kufanya kazi badala ya kwenda kwenye Balozi za watu wengine na kuomba labda watusaidie, kwa sababu hapa ndiyo mahali pake. Nategemea kwamba bajeti yetu itapita bila shida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Polisi wetu walikuwa wanapata ration na wanaendelea kupata lakini wanapata mwisho mwezi na majeshi yetu mengine haya. Ni vizuri kwa sisi ambao tunafanya nao kazi, tunazungumza nao, wanaomba sana hii ration itolewe kati ya mwezi na isiwe mwisho wa mwezi, kwa sababu ikitolewa katikati ya mwezi ina manufaa makubwa sana kwao. Kwa hiyo, namwomba kaka yangu Mheshimiwa Mwigulu alichukue hili kwamba ni hitaji la vijana wetu wa ulinzi na usalama, wanaomba ration zao zipatikane katikati ya mwezi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kama Mbunge, vijana wangu wa Dar es Salaam pale wengi wanaendesha bodaboda. Hivi sasa imekuwa bodaboda na Jeshi letu la Polisi wanawindana kama chui na paka. Namwomba kiongozi wetu wa Jeshi la Polisi badala ya kuwatazama vijana wale kama maadui na badala ya kuwawinda kama chui anavyowinda mnyama, wawafundishe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua vijana damu inachemka kuna makosa mengi wanakosea, wakati mwingine wanashindwa kufuata sheria, kuvaa kofia ngumu, kuendesha wakiwa na ndala, natambua na hata mimi mwenyewe najitahidi sana kuwaelimisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Jeshi la Polisi lichukue hili kama ni task maalum, kwa sababu wale vijana ni wetu, wamejiajiri, wanatoa service na wanahudumia watu wetu. Huu upungufu wao basi, Jeshi la Polisi kama walivyoanza kufanya kuandaa baadhi ya semina mbalimbali, kuanza kuwaelimisha kuhusu Sheria ya Usalama Barabarani; pili, kuwafundisha maadili ya usafirishaji; na tatu, kuwaeleza kwamba watakapofanya kinyume na utaratibu, watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria ili vijana wale wapate kujifunza. Naamini wakijifunza wanaweza kukafanya vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami natambua kwamba Jeshi la Polisi limefanya kazi kubwa sana katika operation mbalimbali. Nakumbuka kuna kipindi Panya Road walisumbua pale siku moja tu mji mzima uliharibikiwa. Hata wale ambao wanatazama hii dhana ya ulinzi na usalama na kutazama Polisi kama ni watu ambao hawana faida sana, nawashangaa kwa kweli. Nawashangaa kwa sababu naamini Polisi kama wangepata kupumzika siku moja tu na wahalifu wangeijua siku hiyo moja wanayopumzika Polisi, nafikiri tungeijua thamani ya Polisi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka tulipokuwa kwenye kampeni, wakati tunamaliza pale Polisi walitusaidia sana. Wakati mwingine wakijua kwamba chama fulani wanapita njia fulani wanakuja kutuzuia sisi wengine tusiingie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati mbaya sana siku lilipotokea tukio lililotokea laiti sisi vyama tungekutana pale, kwa kweli lingetokea jambo moja kubwa sana. Nafikiri tusingesema tunayosema sasa. Kwa juhudi zao Jeshi letu la Polisi wamefanya kazi kubwa, nami nasema waendelee kufanya kazi kubwa. Huu upungufu unaotokea, siupuuzi na wao wasiupuuze, wautazame kwa jicho kubwa, waondoe upungufu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Wajumbe wenzangu wengine wamesema kwamba watu waliokufa wakaokotwa beach wamefika 1,000 na wengine wanaamini wale walikufa Tanzania, wengine tunaamini sio Watanzania kwa sababu mahali wanapokufa watu 1,000 Tanzania hii wenye ndugu zao wangeonekana. Haiwezekani leo tunazungumzia mfano suala la Benny Saanane, tunazungumzia mfano suala yule mwandishi aliyepotea, halafu tukaacha kuzungumzia watu 1,000 waliopotea, kwa kweli haiwezekani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachoonekana, tukubaliane na kama tulivyopewa taarifa, hawa ni watu wahamiaji haramu wanaotupana, watu wanasafirishwa kwenye malori, wakishakufa wanatafuta mahali pa kuwa- dump. Haiwezekani kwamba wale wawe Watanzania halafu ndugu na jamaa wasionekane.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni jambo ambalo kwa kweli siyo sahihi. Tusije tukalipaka tope Jeshi letu kwa ajili tu ya kutaka kutia uzito wa jambo. Kimsingi tuzungumzie hoja iliyopo, kuna watu wamepotea na watu wakipotea Polisi wanashirikiana nasi kutafuta, haina maana kila aliyepotea kafichwa na Polisi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo hapa limesemwa, jambo kubwa sana.