Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kazi nzuri inayofanya Jeshi la Polisi, lakini kwa muda mrefu jeshi hili lina upungufu wa vituo vya Polisi kwenye maeneo yetu pamoja na vitendea kazi. Naomba Serikali itenge fedha za kutosha kwenye maeneo yetu na kuongeza vitendea kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kumekuwa na upungufu wa nyumba za Askari. Kila mmoja wetu anafahamu mazingira wanayoishi Askari hawa. Ni muda muafaka kwa Serikali kuja na mkakati kabambe wa kujenga nyumba za kutosha kwa ajili ya Askari wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa miaka ya hivi karibuni kumeripotiwa mauaji na kupotea kwa raia hapa nchini. Kuna maiti zinaokotwa kwenye fukwe za bahari, watu wanapotea na kutekwa, lakini kwa bahati mbaya mpaka sasa Jeshi la Polisi halijawakamata na kuwapeleka wahusika wa matukio haya Mahakamani. Ukimya huu unawatia wasiwasi wananchi, maana hawaoni hatua zozote zikichukuliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Nne ilihamasisha sana dhana ya Polisi Jamii na ulinzi shirikishi kwa maana kwamba suala la usalama ni suala la kushirikiana kati ya jamii na Jeshi la Polisi. Kwa siku za hivi karibuni, tumeshuhudia dhana hii kuanza kupoteza maana kutokana na matendo yanayofanywa na baadhi ya Askari Polisi yanawakatisha tamaa wananchi. Naomba Wizara iangalie upya mahusiano ya Jeshi la Polisi na wananchi ili kuhakikisha usalama wa raia wetu na mali zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2016 kulikuwa na kampeni kali ya kupambana na dawa za kulevya iliyoendeshwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam. Wote tulishuhudia orodha ndefu ya wafanyabiashara na watumiaji wa dawa za kulevya na wengine kuitwa Polisi kuhojiwa na kupimwa mikojo. Nataka kujua katika ile orodha, ni wangapi wamefikishwa Mahakamani? Utumiaji wa dawa za kulevya umepungua kwa kiasi gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Zimamoto halina magari na vifaa vya kutosha kukabiliana na majanga yanayotokea kwenye jamii yetu. Serikali ijitahidi kulipangia fedha za kutosha ili liwe na magari na vifaa vya kutosha vya uokozi.