Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Maftaha Abdallah Nachuma

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mtwara Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mwenyezi Mungu na naomba kuchangia kwa maandishi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kuongelea kuhusu mauaji ya raia Abilah Abdureheman wa Mtwara Mjini. Kijana huyu aliuawa na Jeshi la Polisi tangu tarehe 25 Machi, 2018 ufukweni/pwani ya Mtwara Mjini Kianga. Nimeongea sana kuhusu suala hili ila bado sijapata majibu ya Serikali na hatua kwa wahusika ni zipi maana Waziri aliahidi kuunda tume mpaka sasa hakuna majibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali (Waziri) atoe majibu stahiki juu ya mauaji haya kwa kijana ambaye hakuwa na hatia kwa kisingizio kuwa alikuwa mvuvi haramu. Suala hili limeleta taharuki kubwa sana Mtwara Mjini, Serikali lazima ifanye uchunguzi wa kweli na wahusika wachukuliwe hatua na mimi kama mwakilishi wa wananchi nipate majibu ya kina.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, napenda kuongelea Kituo cha Polisi Mtwara (Wilaya) ambacho kiko mbioni kubomoka. Kituo cha Polisi Wilaya ya Mtwara ni kibovu sana, zege inakatika na siku yoyote itabomoka. Naiomba Serikali ikarabati haraka kituo hiki kwani askari wetu watapoteza maisha muda wowote baada ya kuwabomokea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, niongelee kuhusu kukosekana kwa samani katika Kituo cha Wilaya ya Mtwara. Kituo hiki hakina meza na viti ambavyo vinaweza kukidhi mahitaji ya polisi wanapotoa huduma. Polisi wanasimama muda wote wanapohudumia wananchi. Naomba ziletwe meza na viti katika kituo hiki cha Polisi Wilaya kwani hali ni mbaya sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nne nitaongelea kuhusu nyumba za bati za Polisi wa Mtwara. Nyumba za bati kwa polisi ni hatari sana. Mtwara Mjini zipo nyumba nyingi za bati mpaka leo. Hali hii inatisha sana kwani umeme unaweza kuangamiza maisha ya askari wetu mara moja. Naomba pesa ziletwe Mtwara Mjini kwa ajili ya kujenga nyumba bora za polisi badala ya hizi za bati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tano, niongelee kuhusu bodaboda na polisi. Mtwara Mjini wahalifu wengi wameingia kwenye kazi ya bodaboda na uhalifu umepungua sana Mtwara Mjini kwa kuwa wahalifu wana kazi ya kufanya. Jambo la ajabu askari wetu ambao hawaitakii mema amani yetu wanawasumbua sana bodaboda tena bila sababu. Askari wanawafukuza kana kwamba wameua, wanakamata pikipiki hovyo na kutoza fine ovyo tena bila sababu. Bodaboda anatakiwa apeleke Sh.40,000 kwa tajiri wake kwa wiki lakini anashikwa na polisi anatozwa Sh.120,000 au Sh.90,000 kwa kisingizio kuwa amefanya makosa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Polisi zimejaa pikipiki nyingi sana. Polisi hawatoi elimu, wananyang’anya pikipiki za maskini, wanaziacha zinaoza katika vituo vya polisi. Hali hii haikubaliki hata kidogo. Naitaka Serikali iangalie suala hili kwa jicho la kipekee kabisa.