Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
ACT
Constituent
Kigoma Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia hoja zifuatazo:-
(i) Uchunguzi wa mauaji ya raia (MKIRU - Mkuranga, Kibiti na Rufiji);
(ii) Suala la uraia wa watu wa Kigoma;
(iii) Kupotea kwa Ben Saanane, Azory Gwanda na Simon Kanguye bila taarifa yotote ya polisi kuhusu uchunguzi wa kupotea kwao. Pia uchunguzi kuhusu kupigwa risasi Tundu Lissu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi ya Watanzania 380 wanatajwa kupotezwa ‘MKIRU’, Bunge lichunguze kama lilivyochunguza Operesheni Tokomeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, 12 Juni, 2017 mchana Bi, Ziada Salum wa kitongoji cha Maparoni Wilayani Kibiti alikuwa nyumbani kwake akipika chakula cha familia yake, wakati ambao Jeshi la Polisi lilifika na kumchukua kwa ajili ya kwenda kumhoji. Ni Miezi 11 leo tangu Bi. Ziada Salum achukuliwe, hajarudishwa mpaka leo, familia yake haijaarifiwa chochote, bado imekaa na matarajio kuwa ipo siku atarudi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwezi huo wa Juni, 2017, si Bi Ziada tu aliyechukuliwa na kutokurudishwa mpaka leo, kwa staili ya namna hiyo ni wengi mno. Wakiwemo kina mama wa familia moja, Rukia, Muhohi na Tatu, Muhohi wa kitongoji cha Msala, hapo hapo Wilayani Kibiti, wao wakichukuliwa kwenda kuhojiwa na Jeshi la Polisi 26 Juni, 2017 na mpaka leo hawajarudishwa. Kaka yao Nassoro Muhohi yeye alichukuliwa 27 Juni, 2017 kisha kuachiwa (najua kwa kumtaja hapa Bungeni anaweza kuchukuliwa tena na mara hii kupotea kabisa).
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitongoji hiki cha Msala kimewapoteza wengi, akiwemo Jumanne Rashid Pango, aliyechukuliwa naye siku moja pamoja na Rukia na Tatu Mhohi. Ni miezi zaidi ya 10 leo, watu hawa wote Jeshi la Polisi halijawarudisha, lakini pia halijatoa maelezo yoyote kwa ndugu zao juu ya walipo na lini watawarudisha?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kina Muhohi si ndugu pekee waliochukuliwa na Jeshi letu la Polisi na kutokurudishwa mpaka leo, katika Kata ya Mjawa, Wilayani Kibiti ndugu watatu wa familia moja nao walichukuliwa 2 Juni, 2017, hao ni Hamisi Omari Nyumba na mwanawe, Sadam Hamisi Nyumba pamoja na nduguye, Juma Omari Nyumba. Nao Jeshi la Polisi limebaki nao mpaka leo, halijawarudisha, hatujui kama bado wako hai ama ni sehemu ya miili iliyookotwa kwenye fukwe zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sio hao tu, 10 Julai, 2017, katika Kitongoji cha Nyantimba, Wilayani Rufiji, Jeshi la Polisi liliwachukua watu watatu, bwana Hamis Mketo, Bi Tabia Nyarwamba na Bi. Pili Mkali nao wakielezwa wanakwenda kuhojiwa, kama ilivyo kwa hao wengine, nao hawajarudishwa mpaka leo, zaidi ya miezi tisa sasa. Orodha niliyonayo hapa ni kadhia 68 za namna hii, kadhia 62 zikiwa zimezithibitisha, kadhia nane nikiwa naendelea na uchunguzi. Kwa sababu ya muda niishie kutaja hao tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kadhia za namna hii ni nyingi mno na yeyote kati yetu, akipata wasaa tu wa kwenda MKIRU (Mkuranga, Kibiti na Rufiji) ataelezwa mambo haya kwa undani, makadirio ni kuwa zipo kesi zaidi ya 380 za namna hii za watu kuchukuliwa na kutorudishwa kwa zaidi ya miezi 10 sasa, hizo ni tofauti na zile za watu waliokamatwa, kuteswa na kisha kuachiwa au wale waliojeruhiwa kwa kupigwa risasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo MKIRU tu, bali ukanda wote wa Kusini, wiki mbili zilizopita, Mbunge wa Kilwa Kusini Mheshimiwa Suleiman Bungara ‘Bwege’ (CUF) naye alieleza kadhia za watu 10 wa Jimboni kwake Kilwa, kuchukuliwa Msikitini na Jeshi letu la Polisi, kupigwa risasi wengine kutokurudishwa mpaka leo na kuhisiwa kuwa wameuawa, wengine kurudishwa wakiwa na vilema vya kukatwa masikio, kuchomwa ndevu kwa moto na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua haja ya kudhibiti hali mbaya ya usalama iliyojitokeza mwaka jana. Mauaji yale ya Askari Polisi na raia yaliyokuwa yakiendelea MKIRU yalipaswa kukomeshwa, lakini bado ukomeshwaji husika ulipaswa kufanyika ndani ya utaratibu wa kisheria tuliojiwekea kama Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haya yanayoripotiwa sasa kutoka MKIRU, ni dhahiri kuwa utaratibu wa kisheria ulikiukwa, haki za binadamu zilivunjwa, raia wema na wasio na hatia waliuawa na jeshi ambalo lilipaswa kuwalinda na wananchi wengi wakiwa wamepotea tangu wachukuliwe kwenda kuhojiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo ya namna hii si mapya hapa nchini mwetu, hayana nia nzuri ya kudhibiti jambo baya, bali hutumika kuwaumiza wananchi. Mwaka 2013 nchi yetu ilikumbwa na janga kubwa la ujangili, tembo na faru wetu wakiuawa na magenge ya wahalifu. Kwa nia njema ya kudhibiti ujangili huo, Serikali kwa kutumia majeshi yetu, ilianzisha Operesheni ya kutokomeza Ujangili huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipindi kifupi cha Operesheni husika, malalamiko juu ya wananchi kubakwa, kuteswa, kuuawa, kuporwa mali zao na mengine mengi mabaya ya unyanyasaji wa raia yaliripotiwa. Unyanyasaji na ukiukwaji huo wa haki za binaadam wa wananchi wetu uliripotiwa Wilayani Babati, Mkoani Manyara; Tarime, Mkoani Mara; Kasulu, Mkoani Kigoma; Meatu, Mkoani Simiyu; Ulanga, Mkoani Morogoro; Urambo na Kaliua, Mkoani Tabora; pamoja na maeneo mengine ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, malalamiko ya wananchi yaliletwa hapa Bungeni. Bunge letu lilichukua hatua juu ya malalamiko hayo. Kwanza kwa kuitaka Serikali kusitisha Operesheni Tokemeza na kisha kwa kuunda Kamati Teule ya Bunge, kuchunguza juu ya utekelezwaji wa Operesheni Tokomeza. Kamati Teule ilithibitisha ukweli wa madai ya wananchi kunyanyaswa, kuuawa, haki zao kubinywa na kadhalika na hatua kadhaa njema zilichukuliwa ili kurekebisha jambo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, malalamiko ya MKIRU ni makubwa mno, unyama unaoripotiwa kufanywa huko na vyombo vyetu vya ulinzi na usalalma hata hauelezeki, umehusisha kupotezwa kwa watoto, akinamama na wazee, haukujali jinsia wala rika, kadhia chache nilizozielezea hapa zimeonesha taswira ya maumivu na ukubwa wa jambo hilo, zaidi taarifa juu ya kupotea kwa watu zaidi ya 380 zikishtusha na kuamsha hisia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mkutano Mkuu wa CCM wa mwaka 1987, Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere alisema yafuatayo:-
“Panapokuwa hapana haki, wala imani na matumaini ya kupata haki, hapawezi kuwa na amani wala utulivu wa kisiasa. Hatima yake patazuka fujo, utengano na mapambano”.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu hawa wa MKIRU na Kusini kwa ujumla ni ndugu zetu, kaka na dada zetu, ni Watanzania wenzetu ambao tuko humu Bungeni kuwawakilisha. Unyama huu unaosemwa kufanywa dhidi yao umewaondolea kabisa Haki yao ya uhai, umewaondolea Imani ya kupata ulinzi wa Vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama, Bunge letu lichunguze jambo hili kuwapa Matumaini ya kupata haki, ili wasibaki na vinyongo na ili wasichague fujo, utengano na mapambano kama njia ya kuponya majeraha yao na kudai Haki zao zilizominywa. Sisi Bunge tunao wajibu huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo basi, kwa maelezo hayo niliyoyatoa, kwa mujibu wa Kanuni ya 120(2) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, naomba kutoa taarifa kwamba nitatoa hoja binafsi kutaka Bunge lako Tukufu Kamati Teule kufanya uchunguzi kuhusu kadhia za Mauaji, kupotea, kupigwa Risasi, kuteswa watu wa MKIRU na Kusini kwa ujumla. Ni imani yangu kuwa Wabunge wenzangu wataunga mkono jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wa kigoma si Watanzania? Uhamiaji na NIDA watueleze tukatafute nchi yetu? Jambo la pili ninalotaka kulizungumzia ni juu ya suala la uraia kwa watu wa mikoa ya mipakani mwa nchi, zaidi kwetu sisi watu wa Mkoa wa Kigoma. Nchi yetu inapakana na nchi majirani nane, zikiwemo nchi za Kenya na Uganda upande wa kaskazini; Msumbiji, Malawi na Zambia upande wa kusini; na Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa upande wa magharibi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wa upande wa magharibi, hasa tunaopakana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Burundi ndio tunaosumbuka na haya masuala ya uraia kwa kiasi kikubwa kuliko watu wengine wa mikoa ya mipakani. Kiasi kwa sasa limekuwa ni jambo la kawaida kabisa kwa mtu yeyote mwenye asili ya Mkoa wa Kigoma, aliyekwaruzana au kusigana na Serikali kuitwa na kuhojiwa na Idara ya Uhamiaji au kutakiwa kuthibitisha uraia wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, orodha ya matukio ya namna hiyo ndefu sana, sina haja ya kuisema hapa, lakini wahanga wa karibuni wa kadhia za namna hiyo ni Abdul Nondo, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, UDSM na kiongozi wa Mtandao wa wanafunzi nchini, TSNP; pamoja na Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), ndugu Zacharia Kakobe, ambao wote waliitwa kuhojiwa na Idara ya Uhamiaji kwa sababu ya misigano waliyonayo na Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiacha hilo la watu wengi wenye asili ya Mkoa wa Kigoma, wenye mikwaruzano na Serikali kuitwa kuhojiwa na Idara ya Uhamiaji, sasa limeibuka tatizo kubwa zaidi na hili linatuhusu karibu wananchi wote wa Mkoa wa Kigoma, ugumu katika upatikanaji wa vitambulisho vya Taifa kutoka NIDA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wa Kigoma tunasumbuliwa mno kupata vitambulisho, katika wakati ambao ni 13.4% tu ya Watanzania wote ndio wana vyeti vya kuzaliwa, haitegemewi kuwa hicho kitumike kuwa kikwazo cha sisi kunyimwa vitambulisho. Zaidi hata wananchi wanaokwenda na viapo nao wanasumbuliwa, wakati wanatumia gharama kubwa kuvipata viapo husika, wakivifuata mjini kwenye huduma ya Mawakili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wa Kigoma ni maskini, mkoa wetu ni moja ya mikoa masikini zaidi nchini, ni mkoa pekee hapa Tanzania ambao haujaunganika kwa mtandao wa barabara za lami na mikoa mingine nchini, haya pekee yalitosha kuifanya Serikali kututazama kwa jicho la huruma. Lakini sivyo, hata Utanzania wetu, uraia wa nchi yetu tunahojiwa, tukinyanyaswa na kutendewa kama watu wa daraja la pili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuyaoni haya kwa Wadigo wa kule Horohoro, au Wamasai wa Longido, kama ambavyo hatuyaoni haya tunayotendewa watu wa Kigoma, kwa watu wa Nachingwea na Nanyumbu, au Nyasa na Tunduma. Kwa nini sisi tu watu wa Kigoma tunasumbuliwa zaidi kuhusu masuala ya uhamiaji? Kwa nini sisi watu wa Kigoma ndio tunapata zaidi tabu kupata vitambulisho vya Uraia kutoka NIDA? Kwa nini ni sisi tu? Naamini Waziri atakuja na majibu juu ya suala hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge tulipuuza kupotea kwa Saanane, tusipuuze kuchunguza kupotea kwa Azory na Kanguye. Mwaka jana Aprili, 11 nilizungumza humu Bungeni wakati nikichangia Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, juu ya kupotea kwa ndugu Ben Saanane, kijana wa Kitanzania, kupotea ambako kulihusishwa na Idara ya Usalama wa Taifa, ikielezwa kwamba alishikiliwa na kisha ‘kupotezwa’ na watu wanaohisiwa kuwa ni Maafisa wa Idara ya Usalama wa Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maelezo yangu yale, nilitoa wito kwa Bunge lichukue hatua kufanya uchunguzi juu ya jambo hilo, kwanza ili kupata ukweli juu ya matukio yaliyokuwa yameanza ya watu kupotea tu bila maelezo ya kina, pamoja na kulinda hadhi ya Idara ya Usalama wa Taifa ambayo ilitajwa kuhusika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni bahati mbaya kuwa wito wangu wa Bunge kufanya uchunguzi haukupata uungwaji mkono. Wakati natoa hotuba ile, ilkuwa ni miezi sita tangu ndugu Saanane apotezwe, leo ni mwaka mmoja na nusu, familia yake, ndugu na wazazi, wamebaki na simanzi ya kutojua nini kimetokea kwa kijana wao. Idara yetu ya Usalama wa Taifa imebaki na doa la kuhusishwa na kupotea kwake na nchi yetu imechafuka, kwa taswira yake kuwa ni nchi ya usalama na amani kupotea na Bunge letu likionekana dhaifu kwa kutokuchukua hatua ya kuchunguza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi ndani ya Bunge hili tunayo dhima na wajibu, tumekasimishwa na Watanzania wenzetu mamlaka na madaraka ya kuwasemea, kuisimamia Serikali kwa niaba yao, kuhakikisha juu ya usalama wao. Kwenye jambo hili la ndugu Saanane tumeshindwa kutimiza wajibu wetu, tumeshindwa kuhoji juu ya usalama wake, hasa ikiwa Idara yetu ya Usalama wa Taifa ndiyo inayotajwa juu ya kupotea kwake, hatujafanya kazi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kushindwa kwetu kuhakikisha tunachunguza suala la ndugu Saanane kumetoa mwanya wa matukio ya namna hiyo ya watu kupotezwa tu kuendelea bila kukoma, sasa karibu yataonekana ni matukio ya kawaida. Labda kwa kuwa Saanane ni kijana wa upinzani tuliona tu kuchunguza juu ya kupotea kwake, tukidhani ni jambo lingeishia tu kwa watu wa upinzani, lakini kupuuza kwetu kumepelekea kupotea kwa ndugu Simon Kanguye, huyu ni Diwani wa CCM na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kibondo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mazingira ya kupotea kwa ndugu Kanguye hayana tofauti na mazingira ya kupotea kwa ndugu Saanane, yeye aliitwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo, kukutana na DSO(Afisa Usalama wa Wilaya) wa Kibondo, tangu hapo hajaonekana, akiwa amepotea siku moja kabla ya ziara ya Rais na Mwenyekiti wa CCM Taifa hapo kwenye Hamashauri ya Kibondo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kanguye amepotea tangu Julai, 2017, miezi miwili na siku10 tangu Bunge likatae wito wangu wa kuchunguza kupotea kwa Ben Saanane. Naamini sisi Bunge tungechunguza juu ya kupotea kwa Ben labda asingepotea, labda angekuwa na familia yake, au barazani na Madiwani wenzake kule Kibondo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ni miezi tisa na nusu tangu Kanguye apotee, mkewe na wanawe wamekwenda kila mahali kutaka msaada wa kupatikana kwake, mie huyu ni mjumbe mwenzangu wa RCC, nimehoji huko, sijapata majibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miezi minne tangu kupotea kwa Kanguye, akapotea Azory Gwanda, baba, mume na Mwandishi wa Habari za Uchunguzi, akiandikia hasa Magazeti ya Kampuni ya Mwananchi, kupotea kwake kumehusishwa na habari za Kibiti ambazo amechunguza na kuandika mno. Kama ilivyo kwa Saanane na Kanguye, maelezo ya kupotea kwa Azory (kwa mujibu wa mkewe) yamehusisha tena watu wetu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama, waliomchukua 21 Novemba, 2017 nyumbani kwake na kutokuonekana mpaka leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ni miezi mitano na nusu tangu Azory apotee, mkewe, dada yetu Anna Pinoni aliyekuwa mjamzito,amejifungua Februari mwaka huu, binti yao sasa ana miezi mitatu, mnaweza kuwaza huzuni, upweke, mfadhaiko na msongo wa mawazo aliyonayo mama huyu. Kuachwa mjane, kuachwa na ujauzito na sasa kulea mtoto akiwa mpweke bila ya mzazi mwenzake. Mimi nikiwaza jambo hili naumia sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Bunge letu haliwezi kuwa msaada kwa Anna Pinoni, kuibana Serikali ieleze alipo mumewe, kuhakikisha anarudishwa kwake salama ili asibaki mjane binti yake asibaki yatima, basi litapoteza maana na uhalali wake kwa wananchi wanyonge. Hali ya mke wa Azory ndiyo aliyonayo mke wa Kanguye pamoja na watoto wao, ndiyo waliyonayo wazazi wa Ben Saanane.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Wabunge hatukutimiza wajibu wakati wa suala la Ben Saanane, tuutimize sasa kwa kuchunguza matukio haya ya watu kupotezwa huku vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama vikihusishwa. Narudia wito wangu kwenu Wabunge wenzangu, kwa heshima na taadhima, tuunde Kamati Teule ya Bunge kuchunguza mambo haya, huu ni wajibu wetu kwa wananchi wenzetu. Tuutimize.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Kanuni ya 120(2) ya Kanuni za Bunge natoa taarifa kwamba nitatoa hoja binafsi kutaka Bunge lako Tukufu kuunda Kamati Teule kufanya uchunguzi kuhusu vitendo vya utekaji, upotezwaji na mauaji dhidi ya raia (likiwemo suala la Ben Saanane, Simon Kanguye na Azory Gwanda).
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini Waheshimiwa Wabunge wenzangu wataniunga mkono kwenye jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mauaji, utekaji na uteswaji unaendelea kwenye Wilaya za Kusini Pwani (Mkuranga, Kibiti, Rufiji – MKIRU). Natambua umuhimu wa kudhibiti usalama wa ndani yetu lakini nalaani mauaji ya raia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nalitaka Bunge kuunda Kamati Teule kuchunguza vifo vya raia Wilaya za MKIRU na Kilwa. Watu takribani 348 wamepotea/kufa ndani ya mwaka mmoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi za inayoitwa Task Force inayoteka, kutesa na kuua watu ni lazima ichunguzwe na Kamati Teule ya Bunge. Bunge haliwezi kuacha raia wake wanauawa hovyo kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi.