Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Kiza Hussein Mayeye

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. KIZA H. MAYEYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema na kuweza kuchangia kwa maandishi siku hii ya leo. Pia niipongeze Wizara kwa jitihada inazozifanya lakini, pamoja na jitihada za Serikali bado katika nchi yetu kuna changamoto nyingi zifuatazo ambazo napenda kuiomba sana Serikali izifanyie kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Maslahi ya Polisi, Polisi ni watu muhimu sana katika nchi yetu kwani ndiyo wanaotulinda raia na mali zetu, lakini kulinda hata amani ya nchi yetu, lakini polisi hawa hawana maslahi mazuri ya mishahara yao. Hii imekuwa ni changamoto kubwa sana kwa polisi kupelekea kuishi kwa shida, hii ni hatari kwani inaweza pelekea wao kuingia katika vitendo vya kiuhalifu kama unyang’anyi wa silaha, upokeaji wa rushwa ili wajiongezee kipato. Niiombe sana Serikali kuboresha mishahara ya Polisi kwa haraka, hii i tawaongezea munkari ya kufanya kazi kwa umakini zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nyumba za Polisi, maeneo mengi ya nchi yetu makazi ya polisi kiukweli ni duni sana na hayaridhishi kabisa. Polisi wanaishi katika mabanda yaliyojengwa kwa mabati. Hii siyo sawa, polisi wapatiwe nyumba nzuri za kudumu na wao waishi kwa heshima. Leo Mkoani kwangu Kigoma polisi wanaishi katika nyumba duni sana humo humo baba, mama na familia hakuna usiri. Kiukweli hali si nzuri kabisa. Niiombe sana Serikali ijenge nyumba za kudumu na nzuri katika mikoa na wilaya zote nao polisi waishi vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uchakavu wa vituo vya polisi, vituo vingi vya polisi vina hali mbaya sana hasa mikoani. Unaweza jiuliza hiki ni kituo cha polisi au ni kitu gani? Kituo chakavu sana, hawa polisi nao ni binadamu wanahitaji kufanya kazi katika mazingira mazuri na hata raia wanaokwenda kupata huduma pale wahudumiwe katika mazingira mazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matukio ya upoteaji wa watu, sasa hivi hali inatisha sana. Kumejitokeza matukio makubwa na ya kuhuzunisha sana, watu wanapotea na kuuawa mara kwa mara na watu ambao hawajulikani. Hali hii imezua taharuki sana kwa wananchi. Serikali niiombe sana kuhakikisha watu hawa wanaofanya vitendo hivi wanakamatwa kwa haraka na kuchukuliwa hatua kali mara moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, raia kubambikiziwa kesi na polisi. Baadhi ya polisi wamekuwa si waadilifu na kupelekea kulichafua Jeshi la Polisi kwani kumekuwa na malalamiko mengi sana toka kwa wananchi hasa vijijini. Wanabambikiziwa kesi na baadhi ya polisi wasio waadilifu kwa lengo la kujipatia pesa. Niiombe sana Serikali kuliangalia suala hili kwa jicho la pili kwani wananchi wengi wanateseka sana, mtu anapewa kesi kubwa wakati hahusiki. Hasa tuliopo mipakani kama Kigoma, wafugaji, wavuvi wamekuwa wakibambikiziwa sana kesi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Polisi kujichukulia hatua dhidi ya raia wanapowakamata. Ninavyofahamu mimi kazi ya polisi ni kulinda raia na mali zake. Polisi anatakiwa kuhakikisha anamlinda raia asipate tatizo lolote lile hata anapomkamata amefanya kosa lolote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni jukumu la polisi kumlinda mhalifu (raia) na kumfikisha kituoni akiwa salama pamoja na mali zake. Hata hivyo, polisi wamekuwa wanaua raia kwa kuwapiga mpaka kupoteza maisha. Hii ni hatari sana sana kupita maelezo. Hata kama raia amekosea ni jukumu la polisi kumlinda na kuhakikisha anafika kituoni salama. Tumeona Musoma Polisi kamchoma kisu raia, kweli polisi wanafikia huku? Hii ni hatari kubwa na inasikitisha sana. Niiombe Serikali hii sikivu polisi hawa wachukuliwe hatua kali mara moja iwe fundisho kwa wengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado kuna changamoto kubwa sana katika Jeshi la Zima Moto, maeneo ya Wilayani hakuna vifaa vya zima moto vipo mikoani tu. Hii ni hatari sana lakini hata maeneo ambayo yanazima moto bado changamoto ni kubwa, vifaa wanavyotumia kwani inategemea ukubwa wa moto. Niombe sana Serikali iweke vikosi hivi vya zima moto katika maeneo yote ya Wilayani na mijini pia, majengo yawepo ya kutosha. Niombe sana Serikali ijenge majengo ya kutosha, vifaa vya zimamoto vya kutosha katika maeneo yote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uhamiaji maeneo mengi hayana ofisi. Niombe Serikali ijenge ofisi za uhamiaji za kisasa hasa katika Mikoa iliyopo mpakani kama Kigoma, Kagera, Tunduma, lakini utoaji passport umekuwa wa shida sana na bei ya kupata passport ni kubwa kwa raia.