Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JOYCE J. MUKYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia kwa maandishi katika hoja hii kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu haki ya kuishi; kama Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inavyoeleza kwa kila binadamu, Mtanzania ana haki ya kuishi. Nasikitika kuona Jeshi la Polisi Tanzania limekuwa linakiuka Katiba ya nchi ambayo ni Katiba Mama au mwongozo ambao umewekwa na Bunge letu Tukufu ili tuweze kutekeleza majukumu yetu kwa haki na bila kuvunja sheria za nchi yetu ya Tanzania. Polisi wamekuwa wakivunja sheria za nchi mara nyingi sana kwa kukatiza maisha ya watu kwa kutumia silaha za moto, vitu vyenye ncha kali na mambo mengine kama vipigo kwa kutumia nguvu za ziada.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano wa matukio haya ni Ndugu Aquilina Aquiline wa Chuo cha Usafirishaji yaliyotokea mwezi Februari, 2018 Jijini Dar es Salaam. Pia mauaji yaliyotokea kwa mdogo wa Mheshimiwa John Heche, Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, lakini nashukuru kuwa Polisi aliyehusika Tarime ameshafikishwa Mahakamani na naamini haki itatendeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Polisi wafuate sheria zitokanazo na Katiba ya nchi ambayo ndiyo mwongozo wetu na Polisi wenyewe wamekuwa wakikamata raia yeyote anayekiuka sheria ya nchi, lakini wao wenyewe ndio wamekuwa mstari wa mbele kutotii sheria za nchi kupitia Katiba ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haki ya usalama wa mtu na faragha; Jeshi la Polisi pia limekuwa na tabia mbaya sana ya kuingilia haki ya faragha na usalama wa mtu. Ni sawa Askari Polisi anaweza kukagua simu ya raia mara anapomtilia mashaka, lakini kwa siku za hivi karibuni imezidi, kwani Polisi baada ya kukagua simu au laptop ya mtu anabaki nayo kwa muda mrefu sana huku akiwa anafahamu password ya kifaa hicho. Hii ni hatari sana kwani simu au laptop inakuwa haina usalama tena kwa maana ya mambo yaliyopo ndani ya simu na kama inavyofahamika simu na mawasiliano yaliyopo kwenye simu ni siri ya mtumiaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Jeshi la Polisi likague simu hizi na laptop na kuzikabidhi kwa mhusika mara tu wanapomaliza ukaguzi.