Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Deogratias Francis Ngalawa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ludewa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. DEO F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nyumba za Askari Polisi; Serikali ichukue hatua stahiki za kukarabati na kuendeleza nyumba za Askari Polisi hususani Wilaya ya Ludewa. Kuna nyumba za Polisi zilianza kujengwa toka mwaka 2012, lakini mpaka sasa hazijakwisha wakati askari wanaishi uraiani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa kituo cha Polisi cha Wilaya ya Ludewa; Serikali ione sasa kuna haja ya kujenga kituo cha Polisi cha Wilaya kwani Wilaya hii ni ya siku nyingi toka tarehe Mosi Julai,1975. Tuiombe sasa Serikali kufikiria kujenga kituo cha Polisi kwani ongezeko la watu na uhalifu unaongezeka kadri muda unavyokwenda. Ni tumaini la wana Ludewa kuwa suala hili litapewa kipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu majengo ya Magereza; Majengo mengi ya Gereza la Ibihi lililopo Ludewa yamechakaa mno kiasi ambacho yanahitaji kufanyiwa ukarabati mkubwa sana, naomba Serikali kuliona hilo. Pia gereza hili la Ibihi ni gereza la kilimo ambalo lina ekari nyingi sana lakini lina changamoto kubwa ya kutopata trekta kwa ajili ya kulimia na kuleta ufanisi. Tayari gereza hili lilishaomba kupewa mkopo wa trekta jambo ambalo mpaka sasa hawajafanikiwa. Niiombe Serikali kuliona hilo na wapewe trekta ili ifanye kazi kwa tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia uchakavu wa sare za Askari Magereza na wafungwa. Sare zao zimechaka mno, tunaomba Jeshi la Magereza kuliona hili kwani linaaibisha taasisi hii nyeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Idara ya Uhamiaji; Serikali ijaribu kuiangalia Idara hii hasa katika upande wa ofisi na watumishi. Wilaya ya Ludewa haina ofisi ya Uhamiaji na pia watumishi ni wachache mno. Ludewa ipo mpakani mwa nchi hivyo kuwa na watumishi wa kutosha ni jambo muhimu kwani zipo dalili za kuwa na wahamiaji haramu. Pia idara hii ipewe vitendea kazi kwani Ludewa ina eneo kubwa la mpaka kuliko Wilaya ya Nyasa na Kyela. Wapewe magari, maboti, pikipiki na kadhalika kwani miundombinu ya eneo hili ni migumu mno.