Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, naomba kumpongeza Waziri wa Mambo ya Ndani pamoja na Naibu wake, lakini kwa Wizara yote kwa ujumla wake kwa kazi kubwa wanayoendelea kuifanya. Nami nasema hivyo nikijua wazi kwamba suala la kulinda amani ni jambo lenye changamoto kubwa. Ni Wizara ambayo kwa kweli niwapongeze wamefanya kazi kubwa sana na wanaendelea kufanya kazi kubwa. Mwenyezi Mungu aendelee kuwapa nguvu ya kutosha kuhakikisha kwamba suala la amani ni jambo la msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakika nafahamu kwamba hakuna mbadala wa amani. Kwa hiyo, suala la usalama wa watu ni jambo la msingi sana. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mwigulu na timu yake nawapongeza sana kwa kazi kubwa wanayoendelea kuifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nita-reserve muda kwa wenzangu wengine, nitaongea kwa ufupi sana. Kulikuwa na hoja ambayo ilikuwa ikijitokeza hapa kuhusu suala zima la Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kwa utaratibu ambao imeonekana kuna kesi mbalimbali zimejitokeza kuwaweka watu katika ule utaratibu wa masaa 48.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sheria Na. 9 ya Tawala za Mikoa ya Mwaka 1997, Wakuu wa Mikoa wamepewa mamlaka mbalimbali katika kifungu cha (7) na Wakuu wa Wilaya ni kifungu cha 15, kwamba pale ambapo saa nyingine wanaenda katika tukio, au kuna jambo limeonekana kwamba kuna uvunjifu wa amani na suala la kijinai, basi Wakuu wa Mikoa au Wakuu wa Wilaya inawapa nafasi. Lengo kubwa ni kumweka yule mtu chini ya usimamizi fulani kwa ajili ya kuepusha madhara hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa michango ya Waheshimiwa Wabunge mbalimbali hapa, inaonekana sheria ile inatumika visivyo. Hata hivyo, jambo hili limejitokeza katika maeneo mbalimbali ndiyo maana ofisi yetu iliamua kuchukua jukumu maalum kwa ajili ya kutoa maelekezo maalum hasa kwa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kwamba sheria ile iendelee kutumika kwa kadri maudhui yake yalivyokusudiwaa, lakini tusi-over do kinyume cha taratibu. Tuliweza kutoa maelekezo hayo kwa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya, lakini hata hivyo tumeamua kuanzisha zile session maalum kwa ajili ya mafunzo mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua hata humu Bungeni, sote sisi ni Wabunge, lakini wote hatu-act kwa kufanana. Kuna style mbalimbali za utendaji wetu wa kazi, ndiyo maana kati ya Wabunge tuliokuwepo humu kila mtu ana sarakasi zake za utendaji wake wa kazi. Kwa hiyo, katika njia moja au nyingine, wakati mwingine kuna upungufu wa kibinadamu kwa baadhi ya viongozi inawezekana, lakini siyo kwamba ndiyo jambo la kila kiongozi afanye hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa jambo hili najua sheria ipo, lakini tumeendelea kutoa maelekezo mbalimbali hasa pale tunapoona kwamba kuna taratibu kidogo za kisheria zinakiukwa tunatoa maelekezo haya. Kwa kuwa sasa hivi tuko katika mchakato wa kumaliza mafunzo kwa Wakuu wa Mikoa ambapo tumemaliza kwa Wakuu wa Wilaya hapa katikati na tunaenda katika session kwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa, ni imani yangu kwamba utafika muda katika haya mambo ambayo tunaona kipindi kirefu wakati mwingine kuna utaratibu kidogo umekiukwa, naamini wote tutakuwa katika mstari mmoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, napenda kuwasihi hasa Watanzania wote kwa ujumla wetu kwamba mara nyingi sana tutii utaratibu wa sheria ambapo naamini haya yote tukiyafanya kwa umoja wetu, tutaweza kuepuka migogoro mingi sana ambayo inatokea katika jamii yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yangu yalikuwa ni hayo tu, kuweza kutoa ufafanuzi katika maeneo hayo. Kubwa kama nilivyosema mwanzo ni kwamba niwasihi sana hasa Wabunge wenzangu na viongozi wengine, kwamba mara nyingi sana katika utendaji wetu wa uongozi na maisha yetu tuweke suala zima la ustaarabu na maisha ya kawaida na kuheshimiana. Naamini kama viongozi wa Kitaifa na watu wa aina mbalimbali kila mtu akijua mipaka ya kanuni ile ambayo nasema siku zote STK - Sheria, Taratibu na Kanuni itakuwa imetuwezesha sana kuishi katika Taifa letu tukiwa katika hali ya usalama na amani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii. Niseme kwamba naunga mkono hoja hii asilimia zote mia moja.