Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Maftaha Abdallah Nachuma

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mtwara Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuchangia hotuba hizi mbili za Ofisi ya Rais, TAMISEMI na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunijalia, kunipa afya njema na leo hii niweze kuchangia Wizara hizi ipasavyo. Naomba nianze moja kwa moja na Wizara hii ya TAMISEMI na hasa katika eneo hili la Mipango Miji, kumekuwa na matatizo makubwa sana kwenye suala la upangaji miji. Leo hii tunapopita kwenye Halmashauri zetu na hasa kwenye miji midogo na miji mikubwa katika suala la kupanga ardhi ni changamoto kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo baya ambalo naweza kulisema hapa, watu ambao wanashughulika na upangaji wa ardhi, wanafanya mambo ya ajabu sana kwa wananchi wetu wa Tanzania. Unaweza ukakuta wakati wanaenda kupima ardhi, wanapima kwa bei kubwa sana, wananchi wa kawaida hawapati ahueni ya kupimiwa viwanja vyao mpaka uweze kuwa na pesa za kutosha. Hii ni kwa sababu gharama zimekuwa kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Mheshimiwa Waziri Mheshimiwa Jafo kwa kazi nzuri anayoifanya, ahakikishe kwamba Halmashauri zetu hizi zinapewa vifaa vya kupima ardhi na maeneo yaweze kupimwa kwa viwango ambavyo vinastahiki, lakini mwisho wa siku, kiwango kinachotumika kupimia ardhi, basi hata unapotoa fidia, iweze kulingana na viwango halisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine kuna maeneo yanaweza yakapimwa, lakini kukawa na double allocation yaani leo hii kiwanja kimoja kinapewa watu zaidi ya watatu, maeneo mengine kiwanja kimoja watu wanne. Hili ni jambo kubwa sana na kuna changamoto kubwa na migogoro mingi ya ardhi kwenye miji yetu kutokana na sekta hii ya ardhi kwenye Halmashauri, lakini hasa kwenye miji yetu midogo na mikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze kidogo suala la elimu. Elimu ni jambo ambalo tumekuwa tunazunguza sana kwenye bajeti zetu zote hapa, kwamba maeneo mengi, shule nyingi za mijini na vijijini hazina madarasa ya kutosha. Mheshimiwa Waziri amezungumza hapa kwamba enrolment ya wanafunzi wa darasa la kwanza sasa hivi imefikia asilimia 101. Enrolment imekuwa ni kubwa sana, kwa hiyo, madarasa hayatoshi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, ukifika Mtwara Mjini unaweza ukashangaa sana. Shule ina wanafunzi zaidi ya 660, madarasa yaliyopo ni matatu. Shule ya msingi Mbae, watoto 650, madarasa matatu. Kwa hiyo, naomba sana, Wizara ya TAMISEMI ihakikishe inajenga madarasa, inapeleka fedha za maendeleo katika Halmashauri zetu ili madarasa yaweze kujengwa ili tuweze kuendana na kasi hii ya enrolment ya wanafunzi iende sambasamba na idadi ya madarasa tuliyokuwa nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wakati tunasoma wakati ule miaka ya 1990 kule mwanzoni, ilikuwa ukifika shuleni asubuhi ni lazima ukimbie mchakamchaka. Leo hii mchakamchaka haupo, watoto hawafanyi mazoezi. Hata michezo mashuleni imedorora sana. Nalizungumza hili kwa sababu, wakati fulani nilikuwa Mkuu wa Shule Mchinga sekondari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna michango mingi sana, inapofika suala la UMISETA na suala la UMITASHUMTA, yaani badala ya Serikali kutenga fedha kwa ajili ya michezo, wanawabebesha Wakuu wa Shule pesa zile ndogo ambazo ni za maendeleo, wanaambiwa wachangie kwa ajili ya michezo ya UMISETA na UMITASHUMTA. Mkuu wa Shule anakuwa kama kaibeba shule kichwani kama shule yake mwenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana, TAMISEMI itenge pesa za kutosha, zipelekwe mashuleni kwa ajili ya kugharamia michezo. Tunaamnini watoto wakifanya michezo, wakikimbia mchakamchaka asubuhi, wakicheza mpira, brain zao zinakuwa na uwezo wa kufikiri sawa kuliko hali ilivyo hivi sasa. Suala la michezo ni suala muhimu sana. Michezo ni afya, michezo ni burudani, michezo ni furaha, michezo ni ajira. Vipaji vingi vinapotea kwa sababu hatuwekezi vya kutosha katika ngazi za Shule za Msingi na Sekondari. Uhakikishe Mheshimiwa Jafo unatenga pesa za kutosha kupeleka mashuleni kwa ajili ya kugharamia UMISETA na UMITASHUMTA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie pia suala ambalo Waheshimiwa Wabunge wenzangu wamezungumza sana kuhusu posho za Madiwani kwamba hazitoshi. Nami naungana nao. Vilevile posho za Wenyeviti wa Mitaa, unaweza ukashangaa Halmashauri nyingine hizo posho hazipo kabisa. Wenyeviti wa Mitaa wanafanya kazi kubwa sana. Wenyeviti wa Mitaa wanahudumia wananchi sana. Tunaomba sana kwamba posho za Wenyeviti wa Mitaa zipelekwe, ziongezwe, iwekwe sheria maalum, waweze kupewa posho ambayo angalau inafanana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii hali iliyopo Wenyeviti hawa wanapata posho kulingana na maeneo na makusanyo ya Halmashauri. Ukija kwa mfano pale Mtwara, Mwenyekiti wa Mtaa mwezi mzima analipwa shilingi 20,000 tu, ni jambo la ajabu sana. Huyu Mwenyekiti wa Mtaa anahudumia wananchi usiku na mchana, halafu mwisho wa siku, mwezi mzima analipwa shilingi 20,000 kwa hisani ya Halmashauri. Naomba sana tuweke utaratibu wa kutosha kabisa, Wizara ipeleke fedha iweze kuwahudumia Wenyeviti hawa wa Halmashauri kwa sababu wanafanya kazi kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la miradi ni jambo ambalo linashangaza sana. Pesa za kuendeleza miradi haziendi katika Halmashauri zetu. Unaweza ukaangalia ukipitia randama hapa kwa mwaka mzima zimeenda 15% au 16%, ni jambo la ajabu sana. Miradi yetu haiendi kwa sababu pesa hazipelekwi kule kwenye Halmashauri. Nilikuwa naomba sana Mheshimiwa Waziri Jafo kwa sababu tunakufahamu sana, ni katapila, utenge pesa za kutosha zifike Halmashauri ili miradi yetu hii iweze kutekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine, kwa mfano pale kwangu Mtwara, siku moja DC alimuuliza Mkurugenzi kwamba tunataka tukakague miradi ya Halmashauri. Mkurugenzi hana miradi, pesa hazijaenda, anamwambia miradi iliyopo hapa ni Miradi ya Mfuko wa Jimbo tu, ya Mbunge. Twende tu ukakague ujenzi wa kupumzikia wagonjwa pale zahanati na maeneo mengine, lakini Halmashauri miradi imesimama kwa sababu pesa hazifiki. Ni jambo la ajabu sana, tulikuwa tunaomba pesa zinazotengwa kwa ajili ya miradi ya Halmashauri pesa ziweze kufika na kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni afya. Hili ni jambo muhimu sana, kwamba tunaekelezwa sasa hivi kwamba dawa zile tunaita tresa medicines zinafika asilimia 94 kwa taarifa za Waziri anavyosema. Bado ukiingia kwenye hospitali na zahanati zetu, tunaambiwa dawa hazitoshi ama dawa hazipo. Leo mgonjwa anatoka huko anaenda
hospitali anaambiwa dawa zimeisha. Bado tatizo lipo sana, tunaomba Mheshimiwa Waziri kama ni tatizo la watendaji basi tunaomba lichukuliwe hatua ipasayo, lakini kama ni tatizo kwamba tunaambiwa pesa zipo, dawa zipo kumbe kule pesa hazijafika, hili nalo ni tatizo lingine. Tunaomba sana kwamba dawa ziweze kupatikana kama taarifa zinavyoelezwa kwamba iwe kweli aslimia 94.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala hili la dawa zile maalum ambazo ni za kifua kikuu, ziko dawa za HIV na kisukari. Hizi dawa zinatolewa kwenye Hospitali za Mikoa tu, hospitali ambazo zina specialists. Ukipita kwenye vituo vyetu vya afya au kwenye zahanati zetu hakuna hawa specialists na zile dawa hazitolewi na mtu mwingine, hata yule Medical Assistant haruhusiwi kutoa zile dawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba sana, kwa sababu wagonjwa hawa wako wengi sana, wako huko vijijini mbali, wanatembea umbali mrefu sana tunaomba hizi dawa zipatikane kwenye zahanati zetu, zipatikane kwenye vituo vya afya. Kama issue ni mafunzo, basi hata wale medical assistant kwa sababu wanaokoa maisha ya Watanzania sana, wapewe mafunzo ya kutoa hizi dawa, isiwe tu pale kwenye specialist kwenye Hospitali za Mikoa ambazo ziko mbali sana na wananchi. Tulikuwa tunaomba sana hili liweze kupewa upekee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili la barabara kwenye miji yetu imekuwa changamoto sana. Watu wa TARURA wamekuwa ni Mungu watu. Leo ukienda kumwuliza mtaalam wa TARURA, ukimwomba mtaalam wa TARURA aje kutoa ufafanuzi kwa wananchi ambao anawatumikia, anakuwa hawataki, yaani wako pale kama Miungu watu.

Kwa hiyo, naomba kuwe na usimamizi, sheria hizi ziweze kurekebishwa sawasawa. Hawa watu wa TARURA kwa sababu wanawahudumia wananchi wa kawaida, wanahudumia Watanzania, basi waweze kusimamiwa na Madiwani, waweze kusimamiwa na Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi wakati nafanya mikutano ya hadhara pale Mtwara, utamaduni wangu ni kuhakikisha kwamba Wakuu wa Idara wanakuja kutoa ufafanuzi kwa sababu wanawatumikia wananchi, wapo kwa ajili ya wananchi wa Jimbo la Mtwara Mjini. Wote wanakuja, lakini Wakuu wa Idara wa TARURA hawataki kuja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana, kama wapo kwa ajili ya wananchi, basi wahakikishe ya kwamba wanawatumikia wale wananchi. Madiwani na Wabunge ndio wawakilishi wa wananchi. Sasa leo tunashangaa sana kusikia kwamba eti Diwani haruhusiwi kumuuliza mtu wa TARURA nini kinaendelea. Mtu wa TARURA akiulizwa, anasema mimi sisimamiwi na Diwani wala na Mbunge. Sasa wanafanya kazi kwa ajili ya nani? Tulikuwa tunaomba sana, hawa watu wa TARURA wawajibike kwa ajili ya wananchi.