Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ngara
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hoja hizi mbili zilizoko mbele yetu za Ofisi ya Rais, TAMISEMI na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenijalia afya na uzima na ambaye amenipa nafasi hii. Pia, niungane na wananchi wa Jimbo la Ngara, Watanzania, wanajumuiya ya UDOM kuonesha masikitiko yangu makubwa kumpoteza kijana Paschal Deogratius Mboyi, ambaye amefariki dunia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kijana huyu mwaka jana akiwa Chuo Kikuu cha UDOM aliandika kitabu chake cha Diwani ya Pakacha Limetoboka, kitabu ambacho nilimkabidhi nakala yake Waziri wa Elimu na ilikuwa katika mchakato wa kuona namna gani kinavyoweza kuingizwa kwenye syllabus kwa sababu ni vijana wachache sasa ambao wana vipaji. Kwa hiyo, niungane na Watanzania wote kusikitika kwa ajili ya kumpoteza kijana mahiri huyu katika wakati wa ujana na alikuwa na maono makubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na Wabunge wanaopongeza, aisifuye mvua maana yake imemnyea, imemnyeshea au imemnyea yote sawa. Nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anayoifanya. Mvua hii ya kazi kubwa anayoifanya Mheshimiwa Rais, mimi na wananchi wa Jimbo langu la Ngara imetunyeshea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepata takribani bilioni 1.4 kwa ajili ya upanuzi wa vituo viwili vya afya, Kituo cha Afya Murusagamba, Kituo cha Afya Mabawe, kwa maana ya milioni 400 kwa ajili ya miundombinu, milioni 300 kwa ajili ya vifaatiba, milioni 700 kwa kila kituo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepata milioni 226 kwa ajili ya miradi ya maji ya vijiji 10, lakini Mheshimiwa Rais mwenyewe mwaka jana alitupatia milioni 13 cash wakati amekuja Ngara kwa ajili ya kununua pump ya maji na milioni 24 tumepata kwa ajili ya maboresho ya huduma za maji. Mwaka jana huo nilimwomba mradi mkubwa wa maji kutoka kwenye vyanzo vya mito, Mto Ruvuvu, Mto Kagera na Mlima Shunga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kwenye bajeti inayokuja ya maji, kwa taarifa niliyonayo, tunategemea kupata karibu milioni 200 kwa ajili ya kuanza upembuzi yakinifu wa mradi huo. Nina kila sababu ya kumpongeza, kuwapongeza Watendaji wa Serikali kwa maana ya Waziri, Mawaziri, Makatibu Wakuu na Watendaji wote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye elimu. Wengi wamechangia na wamesema kwenye elimu, lakini mimi nitaomba nijikite pia kwenye upande wa elimu maalum na watoto wenye vipaji maalum. Nichukue nafasi hii kwanza kuwashukuru Watanzania ambao wamemuunga mkono kijana wetu Anthony ambaye amesambaa kwenye mitandao ya kijamii nchi nzima na nje ya nchi, anatoka Jimboni kwangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwashukuru wote ambao wameshiriki katika kuchangia kumwezesha ili kijana huyu ambaye ameonekana kuwa na kipaji maalum aweze kuendelezwa. Kwa namna ya kipekee pia, nimshukuru Ndugu Isaack Msuya, ambaye amekubali kumchukua kwenye shule yake anayoimiliki ya Mwanga kumsomesha kijana huyu, pia, wadau wote ambao kwa namna moja ama nyingine wameshiriki katika kumchangia mtoto huyu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni changamoto. Najua kwamba, tumekuwa na shule zenye vipaji maalum, shule hizi ni za sekondari japo nazo pia hazitoshi kama vile Mzumbe Sekondari, Kilakala, Weruweru, Ilboru, Kibaha, shule zisizozidi saba, lakini hatuna shule za msingi, sidhani kwenye record, nimejaribu kupitia kwenye mitandao ku-google, lakini sijaona kuna mahali ambapo tuna shule za msingi zenye vipaji maalum.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shule hizi za msingi ndizo ambazo zinaweza kulea watoto hawa ambao wana vipaji maalum na tukawekeza kwenye watoto hawa ili kusudi tuweze kuwa na wataalam waliobobea wanaoweza kuleta mabadiliko pia ya kweli na kwenda sawa na kasi ya Mheshimiwa Rais kuwa na uchumi wa viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe kwamba hii ni changamoto sasa, hivyo tuangalie uwezekano wa kuanzisha shule zenye vipaji maalum, sambamba pia na shule kwa watoto wenye ulemavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto kwa watoto wenye ulemavu hasa katika kupata elimu ni kubwa. Nilikuwa nikizunguka kwenye Jimbo langu, wapo watoto takribani mia mbili na kitu ambao wako vijijini na kila nilipokuwa nikipita wanauliza wazazi kwamba, kuna mkakati gani kwa ajili ya kuboresha au kuwapatia elimu hawa watoto wenye ulemavu. Tunayo Shule ya Msingi Murugwanza ambayo imeanza programu hii japo katika mazingira magumu, lakini niombe Wizara ya TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto kuona ni namna gani ambavyo tunaweza tukaunga mkono jitihada hizi ambazo zimeanza katika Jimbo la Ngara, hususan katika shule ya msingi Murugwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende upande wa TARURA. TARURA naiunga mkono kwa asilimia 100. TARURA iliundwa kwa maksudi thabiti ya kutaka kuboresha huduma za miundombinu ya barabara kwenye vijiji na miji. Kumekuwepo na ulinganifu kuona jinsi ambavyo Halmashauri zetu zilikuwa zinasimamia programu hii ya matengenezo na ukarabati wa barabara na jinsi ambavyo TANROADS wamekuwa wakifanya. Ukijaribu kuangalia asilimia 30 ambayo Halmashauri ilikuwa ikipata ndiyo hiyo ambayo TARURA nao wanapata, sasa sitegemei kwamba, kuna kiti kinaweza kikafanyika tofauti kama hatutaweza kuongeza bajeti.