Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Magdalena Hamis Sakaya

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Kaliua

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kunipa nafasi nami niweze kuchangia hotuba za Mawaziri hawa wawili. Pia niungane na Waheshimiwa Wabunge kuwapongeza Mawaziri kwa kazi nzuri wanayoifanya na hasa Waziri wa TAMISEMI, Mheshimiwa Jafo na timu yake nzima kwa kusaidiana na Katibu Mkuu kwa kweli kazi inaonekana. Japokuwa Wizara ni pana sana lakini kwa kwenda field kwenda kuona kazi zinazofanyika kule wanaweza kutatua kiasi kikubwa sana cha changamoto ambazo zinaikabili Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana Serikali imetenga shule moja ya msingi katika kila Wilaya kuweza kupokea watoto ambao wana mahitaji maalum kwa maana ya watoto walemavu. Kwa bahati mbaya sana shule hizi miundombinu yake siyo rafiki kwa watoto hawa. Pia shule hizi hazina Walimu wenye uwezo wa kufundisha hawa watoto ambao wana mahitaji maalum na kwa sababu watoto wale kuna wengine ni vipofu, kuna wengine ni walemavu wa viungo, wengine ni usikivu wote wamekusanywa pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaiomba Serikali na fedha ya capitation kwa ajili ya shule hizi hazitoshi kufanya chochote kuboresha miundombinu, Serikali ihakikishe inaboresha miundombinu katika hizo shule ili watoto waliopelekwa pale waweze kupata elimu sawasawa na watoto wenzao wanaopata elimu maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni upungufu wa Watumishi. Kiukweli tuna shida kubwa ya watumishi katika sekta zote. Ukienda elimu, ukienda afya, ukienda ugani, ukienda Watendaji wa Kata kila kona, kwa hiyo TAMISEMI bila kuwa na watumishi wa kutosha wananchi hawawezi kupata huduma. Tunaomba Serikali ihakikishe inaongeza watumishi, Mheshimiwa Mkuchika ahakikishe tunaajiri watu, bahati nzuri wasomi tunao, wako wamesoma wako vijijini, wako mijini wanahangaika hawana kazi, kwa nini hatuajiri?(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya Wilaya ya Kaliua Sekta moja tu ya afya tuna upungufu wa asilimia 76, hujaenda elimu hujaenda kokote. Tunaomba sana Serikali iongeze watumishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lingine ni suala la watumishi kutokupanda madaraja kwa wakati. Leo Walimu wanakaa miaka minne hadi sita hawajapanda madaraja. Swali la kujiuliza watakuja kupandaje madaraja kwenda na wakati? Wakati anatakiwa miaka mitatu apande daraja, leo anapokaa miaka saba hajapanda daraja, anapandaje madaraja? Tunaomba watendaji wapande madaraja kuendana na wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la watumishi wa Kaliua walihama kutoka Urambo tangu mwaka 2013, mpaka leo mwaka wa sita hawajapata stahiki zao. Mwaka wa sita kuhamishwa na haki zao zote, leo wapo Wilaya ya Kaliua lakini tangu wakiwa Wilaya Urambo mpaka wamehamia Wilaya Kaliua leo miaka sita hawajapata stahiki zao. Waziri Mkuu alikuja Kaliua, akaagiza wapewe haki zao, leo ni mwaka wa sita hawajapewa. Naomba watumishi hawa wa Kaliua ambao walitoka Urambo wapatiwe stahiki zao kutokana na majukumu yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la Hospitali ya Wilaya. Wilaya yetu ya Kaliua ambayo ina takribani wananchi laki nne hatuna hospitali ya Wilaya. Tuna vituo vinne tu vya afya, tumeweka kipaumbele chetu ni hospitali ya Wilaya kwa mwaka huu, tukaiomba Serikali itusaidie bahati mbaya sana nimeangalia hiki kitabu hatupo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana tumeanza kama Halmashauri tumejenga jengo la OPD lenye ghorofa moja, mara nyingi nimeongea hapa Bungeni tumekamilisha tuko kwenye finishing, tukawaomba Serikali itusaidie majengo mengine, tunamwomba sana Mheshimiwa Waziri aiangalie Wilaya ya Kaliua kwa jicho la pekee. Tunazo Kata 26 tuna vituo vya afya vinne (4), tuna vijiji 101 vituo vya afya ni vinne.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wanafuata huduma za upasuaji wa akinamama Urambo, tunafuata Kigoma. Naomba sana kwa mwaka huu Kaliua iangaliwe kwa jicho la pekee, kama imesahaulika naomba iingizwe tupate hospitali wananchi wa Kaliua, tuokoe vifo vya akinamama na watoto vinavyotokea kwa kukosa huduma za afya.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la uwezeshaji wa vijana na kina mama. Tumeongea sana hapa Mheshimiwa Jenista alituambia tuna mifuko 17. Nashangaa kama kuna mifuko 17 mbona katika Wilaya yangu ya Kaliua kwa miaka mitatu tumepata vikundi vya SACCOS vimeletwa vinne tu, vijana viwili, akinamama viwili. Fedha nyingine yote ambayo tunawapa vikundi ni ya ndani ya Halmashauri, hii mifuko 17 inasaidia watu wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pengine mgawanyo wake siyo sahihi, pengine mgawanyiko hauna uwiano kwenye Wilaya mbalimbali, inawezekana kuna maeneo ambayo zinakwenda zaidi wengine wanakosa. Naomba sana hata fedha inayotengwa na Halmashauri ni kidogo haitoshi, akinamama vikundi viko zaidi ya mia, hatuwezi kuwapatia mtu anaomba milioni 10 unampa milioni mbili!

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilichangia kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu, lakini bado hapa kwa umuhimu wa Wizara hii na kwa kuwa Mheshimiwa Jafo anajua tukiwawezesha akinamama, tumewezesha familia, tumewezesha jamii, haiwezekani kuendelea kusema tunawawezesha wakati ambapo tunawapa kidogo na hatuwezi kuwasaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni TARURA. TARURA anafanya kazi nzuri shida hawana fedha nimeongea jana hapa barabara zimeharibika nyingi TARURA wako ofisini hawana fedha ya kufanya kazi. Nakubaliana na Waheshimiwa wengine kwamba tuwape TANROAD asilimia 50 na TARURA asilimia 50 kwa sababu barabara za vijijini ndiyo barabara za uchumi, mazao yanatoka kule, wananchi wako kule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkuu wa Wilaya, nyumba imeanza kujengwa tangu mwaka 2013, mpaka leo imekuwa ni pagale haiendelei, imeota majani tunaomba sana nyumba ya Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya wa Kaliua imaliziwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ni suala la kuendelea kuwepo mishahara hewa. Nimeangalia kitabu cha CAG kuendelea kuwepo na mishahara hewa, hivi jamani ndani ya miaka yote na juhudi zote, bado Halmashauri zaidi ya 29 zinaendelea kulipa mishahara hewa. Tunalia habari ya watumishi, tunalia hatuna watumishi wa kutosha lakini fedha zaidi ya milioni 329 wanalipwa mishahara hewa. Huu ni udhaifu kwa kweli wa hali ya juu!

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana tatizo la mishahara hewa watu waliokufa wanalipwa mishahara, liwe ni mwisho. Ni aibu kuendelea kuonekana kwenye vitabu vya CAG na anashauri anasema mapendekezo anayotoa hayafanyiwi kazi, Serikali amkeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.