Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Lupembe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nishukuru sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia katika Wizara hizi mbili TAMISEMI na Menejimenti ya Utumishi wa Umma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa shughuli anazozifanya za kuhakikisha kwamba anatetea maisha ya Watanzania na kuleta maendeleo katika nchi yetu. Pia kwa namna ya pekee nichukue fursa hii nimshukuru sana kwani katika jimbo langu aliweza kutoa vitanda 25 , vitanda 20 vikiwa ni kwa ajili ya wagonjwa wa kawaida na vitanda vitano kwa ajili ya labour, nashukuru sana .
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Mheshimiwa Waziri Suleiman Jafo kwa jinsi anavyojituma katika kuhakikisha kwamba anaisimamia vizuri Wizara yake ya TAMISEMI. Vile vile nimpongeze Mheshimiwa Mkuchika pia naye anajitahidi kusimamia kuhakikisha kwamba mambo yanakwenda vizuri. Niwapongeze pia Naibu Mawaziri wote Mheshimiwa Kakunda na Mheshimiwa Kandege; niwapongeze Katibu Mkuu injinia Musa Iyombe, niwapongeze Naibu Makatibu Wakuu kwa namna wanavyofanya kazi usiku na mchana kuhakikisha kwamba wanawaletea maendeleo Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi wanazofanya Wizara hizi zote mbili ni kazi zinagusa maisha ya Watanzania, zinagusa maendeleo ya wananchi. Maana sote tunajua kwamba Wizara hizi hasa Wizara ya TAMISEMI inahusika sana na huduma za jamii kama vile ujenzi wa shule, vituo vya afya, ujenzi wa barabara na hakuna eneo ambalo shughuli hizi hazifanyiki, kila kijiji na kila eneo kama ni mjini na vijijini kote shughuli hizi zinaendelea. Kwa hiyo wanafanya kazi kubwa sana ya kuhakikisha kwamba Watanzania wanyonge wanapata maendeleo, kwa hiyo nawapongeza wote kwa maana ya mawaziri lakini pia na watumishi wote wa Wizara zote mbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kazi wanazofanya zinagusa maisha ya watu, niombe sana Mwenyezi Mungu awasaidie ili kuhakikisha kwamba wanasimamia vizuri hasa recourses. Pesa wanayoiomba ni trilioni 6.58, ni fedha nyingi lakini ndogo kutokana na jinsi matatizo yaliyopo huko kwenye maeneo yetu yalivyo mengi, kwa hiyo niwaombe sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe sana hasa kwenye zile fedha za maendeleo hasa zile zinazotokana na wafadhili, tujitahdi kusimamia vizuri kwa sababu tusipozisimamia vizuri zinaweza zikasababisha manung’uniko katika baadhi ya maeneo. Halmashauri yetu sisi ya Wilaya ya Njombe ipo Mkoa wa Njombe na ni Halmashauri mama ya Mkoa. Mkoa wa Njombe una halmashauri sita na Halmashauri ya Wilaya ya Njombe ndiyo iliyozaa halmashauri hizi zote; na sasa hivi resources zake zote zimekuwa zikigawanywa kwenye halmashauri nyingine na imebaki halmashauri mzee ambaye hana kitu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, halmashauri hii pamoja ni kwamba ni halamashauri mama ni halmashauri pekee ambayo haina hospitali ya wilaya, halmashauri zote tano za Mkoa wa Njombe zina hospitali za wilaya lakini Halmashauri hii ya Wilaya ya Njombe haina hospitali hata moja ya Serikali lakini pia hata ya binafsi hatuna.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna vituo vya afya vinne tu; tuna Vituo vya Lupembe, Matembwe, Kichiwa na Sovi. Vituo hivi vyote vilikuwa havina huduma ya upasuaji. Mpaka mwaka 2015 tulikuwa na kituo hicho kimoja cha Lupembe tukaongeza vikawa baadaye vinne na sasa hivi tunajenga kituo kingine cha pale Ikuna ambacho tupo kwenye umaliziaji (finishing), kwa hiyo si muda mrefu tutakuwa pengine na vituo vitano vya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu mwaka 2016 nilivyoingia Bungeni hapa, nimekuwa nikiomba Kituo cha Afya cha Lupembe kipewe fedha kwa ajili ya kujenga theater, kutoa huduma ya theater na kujenga wodi. Kituo hiki ni cha muda mrefu sana, mwaka 1985 ndipo kilipoanza kazi yake, kwa hiyo ni kituo ambacho kimeshachakaa. Hata hivyo, bahati mbaya hatujapata hizo fedha pamoja na kwamba tulikuwa tumeahidiwa muda mrefu, lakini hatujapata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, basi kwa kuwa na sisi tulianza kujipanga kuhakikisha kwamba wananchi wetu wale wanapata huduma ya upasuaji, baada ya kuona akinamama wanafariki wanafia njiani kwa kukosa huduma ya uzazi. Kwa hiyo kwa uchungu huo tukaamua kujipanga na mimi Mbunge kwa kushirikiana na halmashauri tukajenga jengo la mama na mtoto. Mimi nilichangia bati katika lile jengo kwenye fedha binafsi nje ya Mfuko wa Jimbo na halmashauri imesaidia wananchi wamefyatua tofali na tukajenga lile jengo ambalo Mheshimiwa Kigwangalla alikuja na akalaifungua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla alipokuja tulimwomba fedha kwamba tupate angalau fedha kidogo kwa ajili ya huduma hii ya upasuaji lakini mpaka leo hatujapata. Hata Kituo kingine kila cha Kichiwa tuliomba tupate fedha na wananchi wameshafyatua tofali tayari, lakini mpaka leo hii hatujapata fedha yoyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi mwezi wa Pili tumeambiwa kwamba tukae kikao kuna fedha milioni mia sita zitakuja, tukakaa vikao vyote Kamati zikakaa kwenye halmashauri yangu na Baraza la Madiwani likakaa, tumetuma Mkurugenzi na Mwenyekiti wamekuja hapa lakini wamerudi bila fedha. Nitaomba Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI atakaposimama basi tuweze kupata ufafanuzi angalau wa hizi fedha milioni mia sita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru kwa namna ya pekee Mheshimiwa Jafo, katika bajeti tumeona kuna hospitali ya wilaya itaaanza kujengwa na wametutengea shilingi bilioni 1.5 nashukuru sana. Hata hivyo pamoja na kutenga hizi fedha tunaomba hizi fedha kwenye hivi vituo ili tuweze kujenga chumba cha theater room na vyumba vingine vinavyohitajika ili hatimaye wananchi wetu hawa wasiendelee kufa kwa sababu ya kutekeleza jukumu lao la msingi la kuongeza wanadamu hapa duniani, kwa hiyo namwomba sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme juu ya barabara kwa maana ya TARURA. TARURA kwangu wanafanya kazi nzuri sana lakini wanakwamishwa na fedha, bado fedha haziendi za kutosha. Sisi kwenye halmashauri yetu tuna mtandao wa barabara ambao una kilometa 586 na zaidi, lakini fedha kwenye bajeti mwaka jana tulipangiwa biloni 1.1, tukapata miloni mia saba na milioni mia nne zimeenda kulipa madeni ya mwaka wa fedha ulioisha, kwa hiyo tumebakiwa na milioni mia tatu. Sasa ukiangalia mtandao wa barabara ulivyo na kiasi cha fedha…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuunga mkono hoja. Ahsante sana.