Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Lucy Fidelis Owenya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. LUCY F. OWENYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kwanza kuongelea kuhusu utawala bora. Utawala bora ni nini? Je, nchi yetu inazingatia utawala bora? Tumeona matukio mengi hapa nchini yasiyokidhi utawala bora wenye kufuata sheria na kujali haki za wananchi wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, uhuru wa kutoa maoni na kupata habari. Hii ni moja ya msingi wa utawala bora kwa wananchi kupata habari lakini tumeona kwa sasa Serikali imezuia hata wananchi kufuatilia majadiliano yanayoendelea ndani ya Bunge (live on TV). Baadhi ya waandishi ya habari wamekuwa wakipotea, wengine kupigwa na baadhi ya magazeti kufungiwa kisa ni kwa kutoa maoni yao dhidi ya Serikali. Hata vyama vya siasa vilivyoanzishwa kisheria kwa Sheria Na.5 ya mwaka 1992 bado haviruhusiwi kufanya mikutano ya hadhara ili kuwaeleza wananchi sera zao badala yake viongozi wengi wa upinzani wamekuwa wakifunguliwa mashtaka kwa kisingizio cha uchochezi. Je, huu ndiyo utawala bora?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, ukiukwaji wa haki za raia. Sasa hivi katika nchi yetu panakuwepo na kundi la watu wasiojulikana wanaoteka watu. Mara nyingi watu wamekuwa wakiokotwa pembezoni mwa bahari ya hindi wakiwa wamefariki. Mfano, Mwandishi wa Gazeti la Mwananchi, Ndugu Azovi Gwanda na Msaidizi wa Mwenyekiti wa CHADEMA, Ndugu Ben Sanane, mnadhimu wetu wa Kambi ya Upinzani, Mheshimiwa Tundu Lissu alipigwa risasi mchana kweupe lakini mpaka leo Serikali haijatoa taarifa yoyote kuhusu matukio hayo yanayoendelea hapa nchini. Je, usalama wa raia uko wapi hapa nchini? Ni lini Serikali itatoa maelezo ya kina juu ya hatua iliyofikia katika kukomesha matukio haya?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nne, ajira. Utawala bora ni pamoja na kuwaongezea watumishi mishahara lakini kwa miaka miwili sasa watumishi hawajaongezewa mishahara kama sheria inavyoelekeza. Huu siyo utawala bora kabisa. Hii ni pamoja na kuwapandisha madaraja watumishi wa umma kwani haijafanyika kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba niongelee Ofisi ya Rais, TAMISEMI kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha za maendeleo kutoka kwa wakati katika Halmashauri; fedha za maendeleo kutoka Serikali Kuu haziendi au hazitumwi kwa wakati kwenda kwenye Halmashauri na kupelekea Halmashauri kushindwa kutekeleza miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikumbukwe siku za nyuma Halmashauri zilikuwa na vyanzo vya mapato vya kukusanya kodi za ardhi na ada mbalimbali ambazo zote hizi zinakwenda Serikali Kuu. Ni vizuri sasa katika makusanyo hayo Halmashauri zikate asilimia 30 ya makusanyo ili zibaki kwa ajili ya maendeleo. Halmashauri nyingi zimeshindwa kutenga hata zile asilimia10 kwa ajili ya vijana, akinamama na watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu; ili mwanafunzi aweze kufaulu vizuri na Mwalimu akubali kufundisha bila kuchoka ni lazima mazingira ya kufundishia na miundombinu ya kufundishia iwe mizuri. Tumeshuhudia shule nyingi tukianza na shule za awali, nyingi hazina Walimu wa kutosha, hakuna nyumba za Walimu, zaidi vijijini, hakuna Walimu wanataka kwenda huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uhaba wa Walimu wa hisabati na sayansi ni mkubwa takribani 22,460 ni pungufu na shule za msingi ni takribani 186,003 ni pungufu sawa na asilimia 83.1. Serikali ina mikakati gani ya kuhakikisha upungufu huu unajazwa kwa kuajiri Walimu? Baada ya hayo ni lazima Serikali ihakikishe:-

(a) Walimu wanalipwa posho zao;

(b) Pawepo na mashimo ya vyoo ya kutosha; na (c)Maabara zikijengwa ihakikishwe zina vifaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, afya; Serikali imekuwa ikitoa kauli ya kujenga zahanati na vituo vya afya katika kila kijiji na kata lakini ikumbukwe kuna zahanati zilizopo lakini bado zina upungufu mkubwa, hazina Wauguzi wa kutosha, dawa hazipelekwi kwa wakati, hazina ambulance ya kupeleka mgonjwa aliyezidiwa pengine anahitaji rufaa kwenda ngazi ya juu. Mfano, kutoka zahanati kumkimbiza hata hospitali ya Wilaya wanashindwa na mara nyingine kupelekea wagonjwa kufariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni jambo la kusikitisha mahali kama Moshi Manispaa hakuna Mfamasia, aliyepo ni technician tu, hivi huyu anaendaje kukagua Mafamasia walio juu yake kitaaluma?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo; katika Hamashauri yetu bado kilimo hakijathaminiwa ila Serikali imekuwa ikija na mbwembwe za maneno tofauti kama vile kilimo ni uti wa mgongo, kilimo kwanza na kadhalika, lakini kilimo bila watalaam hakiwezi kuwa na tija. Kuna uhaba mkubwa wa Maafisa Ugani na uhaba wa pembejeo. Mfano, sasa hivi mbolea ni ghali sana mfuko Sh.53,000, mkulima wa kawaida anaweza kununua? Hata wakilima na kufanikiwa kuna uhaba mkubwa wa kuuza mazao yao. Sasa hivi mbaazi ziko tu nyumbani kwa wakulima na mahindi mengi yanaharibika na hata wakulima wakitaka kuuza nje Serikali inazuia na hata wakitaka vibali ni ngumu kuvipata.