Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Dr. Haji Hussein Mponda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Malinyi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Waziri, Naibu Waziri na Watendaji wa Wizara kwa kufanikisha majukumu yao katika kiwango cha kuridhisha. Naomba nijikite mchango wangu katika sehemu zifuatazo:-
(a) Kuongeza tija na uzalishaji wa mazao ya kilimo; usambazaji wa pembejeo nashauri uende sambamba na mahitaji halisi kwa eneo husika na muda muafaka, mfano wakulima wa Bonde la Kilombero hususan Wilaya ya Malinyi na Ulanga hawahitaji sana mbolea, ni vema Serikali ikatoa pembejeo za mbegu bora za mpunga badala ya mbolea ambayo haitumiki au kuhitajika sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakulima wa zao la mpunga bado wana changamoto kubwa ya soko la uhakika. Naiomba Serikali waendelee kununua mpunga kupitia Mfuko au Wakala wa Hifadhi ya Chakula (NFRA). Katika mwaka huu, Wakala waweke utaratibu wa kuja kununua mpunga katika Wilaya za Malinyi, Ulanga na Kilombero badala ya kujikita zaidi maeneo ya Mbeya na Sumbawanga peke yake.
(b) Utatuzi wa migogoro ya wakulima na wafugaji; naipongeza Serikali katika kuanzisha na kutekeleza zoezi la mpango wa matumizi bora ya ardhi na upimaji wa ardhi. Mkakati huu peke yake hautamaliza kutatua migogoro inayoendelea bila ya kujenga miundombinu rafiki kwa mifugo ikiwemo kujenga visima vya maji, malambo, majosho katika maeneo tengwa kwa ufugaji. Serikali inaweza kuwawezesha wafugaji kupitia SACCOS zao kujenga miundombinu hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, nashauri Serikali kuelimisha na kuwezesha utaratibu wa kudumu wa uvunaji wa mifugo kwa kuwezesha upatikanaji wa soko la mifugo.
(c) Uvuvi; uwezeshaji wavuvi; katika bajeti hii Serikali imejikita zaidi katika uvuvi wa bahari au ziwa na kuwawekea taratibu za uwezeshaji wake. Nashauri Serikali pia kuangalia uwezeshaji kwa wavuvi katika mito mikubwa kama vile Kilombero, Rufiji na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Shukurani.