Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Risala Said Kabongo

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. RISALA S. KABONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema kuniwezesha kuchangia hotuba iliyoko mezani. Nianze kwa kuzungumzia Mfuko wa Wanawake, Vijana na Walemavu ambao unatengwa kwenye halmashauri zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nipende kuwapongeza sana Mawaziri wote kwa kazi nzuri wanazozifanya, nimpongeze Mheshimiwa Jafo na wasaidizi wake kwa kazi nzuri na zinazoonekana. Ninachotaka kushauri ni kwamba Mfuko huu utengewe akaunti yake maalum katika halmashauri zetu ili kufanya usimamizi mzuri wa fedha hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwongozo wa Serikali ni kila halmashauri kutenga fedha asilimia 10 kutokana na mapato ya ndani. Jambo hili ni jema sana iwapo litaratibiwa vizuri kwa kuwa litasaidia ajira kwa makundi haya hasa kwenye ujasiriamali. Naomba kuishauri Serikali ilete Muswada wa Sheria ya Kusimamia Mfuko wa Wanawake, Vijana na Walemavu. Mfuko wa Walemavu 2% utungiwe sheria inayozielekeza halmashauri kutenga kiasi hiki kwa ajili ya walemavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wakala wa Ujenzi wa Barabara Vijijini (TARURA). Lengo ni kuhudumia barabara zote zilizokuwa zinahudumiwa na halmashauri za wilaya, miji, manispaa na majiji. Kumekuwa na changamoto mbalimbali katika TARURA kukubaliana na majanga kama mafuriko ambayo hupelekea uharibifu wa madaraja, makalavati na mashimo makubwa kwenye barabara vijijini, mijini na mitaa mingi nchini. TARURA inatekeleza majukumu yake kupitia fedha za Mfuko wa Barabara za mwaka wa fedha 2017/2018. Wakala waliidhinishiwa shilingi bilioni 230.8 kwa ajili ya matengenezo ya barabara yenye urefu wa kilomita 34,024.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia Februari, 2018 TARURA imepokea bilioni 98.5 ambazo zimetumika kutengeneza barabara yenye urefu wa kilomita 4,183.3 tu. Naomba Waziri atakapohitimisha atuambie ni kwa nini fedha hizi hazitolewi kwa wakati ili kukamilisha barabara hizi kwa mwaka wa fedha unaoishia 2018. Kwa mujibu wa Hotuba ya Waziri Mkuu ni kwamba barabara zilizopo chini ya TARURA ni kilomita 108,946.2. Mwaka huu wa fedha TARURA imesimamia matengenezo ya barabara ya kilomita 4,183.3 tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha za miradi ya maendeleo kutofika kwa wakati katika halmashauri zetu. Katika kujiletea maendeleo rasilimali fedha toka Serikali Kuu ni muhimu sana, lakini kuna tatizo la Serikali kushindwa kupeleka fedha kwa ukamilifu na kwa wakati kiasi kwamba utekelezaji wa miradi unashindikana na utaratibu wa manunuzi kutofanyika kwa wakati na kutofuata Sheria ya Manunuzi ambayo inahitaji kutimizwa kwa masharti hivyo kupelekea fedha kurudi Serikalini.