Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Azza Hilal Hamad

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kupata fursa hii ya kuchangia bajeti iliyopo mbele yetu ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.Kwanza naunga mkono hoja iliyo mbele yetu na nitumie fursa hii kuipongeza Serikali kwa kazi kubwa inayofanya katika shughuli za maendeleo. Hongera sana Mheshimiwa Rais, Dokta John Pombe Magufuli, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na bila kumsahau Mheshimiwa Waziri Jafo na Manaibu wake wote wawili, hongereni sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Serikali kwa kuamua kwa dhati kuboresha huduma za Mama na mtoto katika vituo vyetu vya afya Mkoa wa Shinyanga. Tumepata vituo sita ambavyo kwa sasa kazi ya ujenzi inaendeleea ukingoni. Tunashukuru sana kwa niaba ya wanawake wa Shinyanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, pamoja na shukurani zangu hizo kwa sekta ya afya, nina ombi maalum ambalo kila ninapopata nafasi ya kuongea lazima niseme chondechonde, Mheshimiwa Waziri naomba sana mwaka huu wa fedha Serikali iweze kuiona Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga kwa jicho la huruma. Naomba tupatiwe fedha ya kutosha katika ujenzi wa hospitali ya Wilaya ambao umeanza kwa muda mrefu sana ili kuweza kuunga mkono jitihada na nguvu za wananchi hatimaye hospitali hii ianze kutoa huduma zilizokusudiwa. Mheshimiwa Naibu Waziri, TAMISEMI wakati anajibu swali humu Bungeni alisema, kwa mwaka huu wa fedha 2018/2019, hospitali 67 zitajengwa; naomba sana miongoni mwa hizo 67 na hospitali ya Wilaya ya Shinyanga iwekwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu ipatiwe fedha za ujenzi wa hospitali ya Wilaya kwa kuwa ni Halmashauri mpya hivyo, huduma hii ni muhimu kwa wananchi wa Ushetu na kuwa na hospitali za Wilaya itasaidia kupunguza msongamano katika hospitali ya mkoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu pia, naomba mnapotoa fedha za kutosha katika ujenzi wa hospitali ya Wilaya, nashauri utumike utaratibu wa force account ambao unaonekana kuwa na tija kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Shinyanga ipatiwe fedha za kutosha ili iweze kukamilika kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe pia kilio changu katika sekta ya elimu, Halmashauri ya Shinyanga ina shule moja ambayo kwa miaka mitatu mfululizo imekuwa ikifanya vizuri katika mitihani ya darasa la saba. Shule hii inaitwa Shule ya Msingi Masunula. Shule hii haina nyumba hata moja ya mtumishi, Walimu wanaishi katika nyumba za kupanga huko mtaani. Naomba sana shule hii itazamwe kwa jicho la huruma ili Walimu hawa tuwape nguvu ya kuendelea kufundisha watoto wetu vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kuwapongeza wananchi wa Kata ya Solwa wakiongozwa na Diwani wao, wamekubaliana kwa pamoja, wameanza kampeni na wameweza kujenga vyoo katika shule zote za msingi katika kata yao na wamejenga madarasa matano, Ofisi ya Walimu na wamejenga na kuchimba vyoo matundu sita na Halmashauri imechangia upauaji wa majengo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa uamuzi huu wa wananchi wa Kata ya Solwa, naiomba Serikali iwaunge mkono wananchi hawa ili waweze kukamilisha ujenzi huo wa shule mpya ya msingi inayoitwa Solwa B ambapo ndiyo wamejenga madarasa matano, Ofisi ya Walimu na vyoo matundu sita. Naomba wananchi hawa wapewe fedha ya kutosha ili panapo majaliwa 2019 shule hii iweze kupokea watoto wa darasa la kwanza kwani wameonesha kilio chao kwa kufanya kazi kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba nitoe ushauri upande wa fedha za wanawake na vijana; naomba vikundi hivi wapewe vitendea kazi na siyo fedha. Hii inaweza kuwa na matokeo mazuri zaidi katika utekelezaji wa mpango huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kuiomba Serikali iweze kuajiri watumishi zaidi hususani sekta ya afya kwa Mkoa wa Shinyanga, kwani kuna upungufu mkubwa sana kuanzia hospitali ya mkoa hadi zahanati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi hii na naunga mkono hoja.