Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Hamoud Abuu Jumaa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibaha Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. HAMOUD A. JUMAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kutumia fursa hii kumshukuru Mungu, mwingi wa rehema kwa kuniwezesha kuwepo mahali hapa na kuchangia hotuba hii ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba hii inakwenda kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi katika nyanja mbalimbali za kimaendeleo, uchumi, elimu, barabara, afya na kadhalika. Nichukue pia nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri na timu yake yote kwa kuandaa hotuba ya bajeti nzuri yenye malengo chanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuipongeza Serikali kupitia Wizara hii kwa kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo na utawala bora Wakuu wa Mikoa yote, mafunzo hayo yametolewa Tanzania Bara. Aidha, Makatibu Tawala wa Mikoa, 26; Wakuu wa Wilaya, 139; Wakurugenzi wa Halmashauri, 185; Maafisa Utumishi,185; Maafisa Mipango, 185; wamepata mafunzo kuhusu majukumu na mipaka ya kazi zao, maadili ya uongozi, utawala bora usimamizi wa sheria, kanuni na miongozo mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango huu ni mzuri na uwe endelevu, kwani mafunzo hayo yamesaidia kuboresha utendaji na kuondoa mwingiliano wa majukumu baina ya viongozi na watendaji. Katika mafunzo hayo, viongozi na watendaji wetu wamekumbushwa wajibu wa kusimamia maendeleo na kutatua kero mbalimbali za wananchi katika maeneo yao ya utawala ili kusaidia kumaliza kama si kupunguza malalamiko ya wananchi ya muda mrefu ambayo yanapelekea kusababisha mabango ya kero zao pindi viongozi wetu wa juu wanapofanya ziara mbalimbali nchini. Napendekeza mpango huu uwe endelevu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inajitahidi sana katika kuwatetea wananchi wetu kwa kasi ya hali ya juu, lakini kumekuwa na changamoto mbalimbali katika safari hiyo ya maendeleo, changamoto hizo zimenigusa mimi pamoja na wananchi wenzangu wa Kibaha vijijini, kwa muda mrefu sana sasa tunaendelea kupambana na changamoto ya maji, wananchi wangu wanaendelea kukabiliana na changamoto hiyo kwa muda mrefu sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi ya maji ambayo ndiyo ingewakwamua wananchi hawa kwa kupata maji safi nayo haikamiliki kwa wakati na ikizingatiwa chanzo cha maji kiko katika eneo lao na wao wamekuwa walinzi wazuri wa chanzo hicho ili kuepuka uharibifu wa aina yoyote unaoweza kutokea na kuleta athari kwa watumiaji wa maji, lakini wamekuwa wakishuhudia maji yakipita na kwenda kutumika katika maeneo mengine na wao kuachwa na changamoto ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ambayo yamekuwa sugu kwa changamoto ya maji ni Magindu, Gwata, Kipangenge, Mwanabwito, Kisabi. Naomba katika bajeti hii kupewa kipaumbele katika sekta ya maji hasa katika miradi ya maji ambayo ina changamoto ya kusimama kufanya kazi kutokana na kuharibika vifaa basi nayo ipewe kipaumbele kwa kufanyiwa marekebisho ya haraka, hii itasaidia katika utekelezaji wa miradi ya maji ili wananchi waondokane na kadhia hiyo ya muda mrefu.

Mheshimiwa, Mwenyekiti, nichukue fursa hii kuipongeza Serikali kwa hatua mbalimbali inazoendelea kuzichukua katika suala zima la kutambua ukuaji wa maji na kuchukua tahadhari ili kuepuka yaliyotokea hapo awali katika miji yetu yasijirudie tena, Serikali inatambua ukuaji wa miji na fursa ya kimaendeleo kijamii, kiuchumi kimazingira. Kwa kutambua hilo ndio maana mipango ya matumizi bora ya ardhi ikaandaliwa katika vijiji 1,764 ikilinganishwa na vijiji 12,545 nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo langu la Kibaha Vijijini tumejiwekea utaratibu wa kuandaa maeneo ili kuepuka matatizo ambayo yamejitokeza katika maeneo mbalimbali nchini kwa kutokutenga maeneo kwa ajili ya shughuli mbalimbali, hivyo basi napenda kuleta ombi kwa Serikali yangu sikivu kupitia Wizara walete na kujenga soko kubwa la kushushia mazao Mlandizi ili kuepusha sasa msongamano ambao upo katika masoko yetu ya mijijini kwa mfano Kariakoo na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mlandizi tuna maeneo makubwa yenye nafasi za kutosha na kupangika hivyo kujenga soko hilo kutasaidia kupunguza msongamano kama nilivyosema hapo awali, lakini si msongamano tu bali pia kutoa fursa ya kuendeleza miji yetu kama Serikali inavyoainisha katika mipango yake, kwani machache ya kuweza kutanua mji huo na ukiangalia mifumo ya mipango miji kwa kiasi kikubwa katika Jiji hili haiko sawa, kwa kuwa ilishakosewa tangu hapo awali.

Mheshimiwa, Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa hatua mbalimbali inazochukua katika sekta ya afya, hatua hizo ni kama kuratibu na kusimamia hospitali zote za halmashauri, vituo vya afya na zahanati kuhakikisha zinatoa huduma bora kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, changamoto hazikosekani. Katika sekta ya afya, katika jimbo langu baadhi ya maeneo bado changamoto zipo, Vituo vya afya Ruvu, Soga, Magindu, Boko, Gwata, Dutumi, Kata ya Kikongo na Kalangalanga vina changamoto mbalimbali ambazo Wizara kama msimamizi na mratibu wa sekta hii hakuna budi kuzitatua changamoto hizo, kuboresha vituo hivyo vya afya ili viweze kutoa huduma bora kwa wananchi na kupungunza idadi ya vifo vinavyotokana na uduni wa vituo hivyo.

Kuongeza ujenzi wa vituo vya afya kutasaidia sana wananchi wangu kupata huduma kwa wakati pale inapohitajika na kuepuka kutembea kwa muda mrefu kufuata huduma ya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine ambayo ipo katika Sekta ya Afya jimboni kwangu ni upungufu wa nyumba za watumishi wa vituo vya afya, zilizojengwa na Serikali bado kasi yake hairidhishi. Nashauri Serikali kuongeza kasi ili zikamilike kwa wakati mnamo 30 Juni, 2018 kama ilivyosema. Mpango huu ukikamilika utasaidia kupunguza adha hiyo. Vilevile usambazaji wa dawa na vifaatiba uongezwe kwa kiwango kikubwa ili kurahisisha upatikanaji wa dawa kwa wananchi na vifaa tiba.

Mheshimiwa, Mwenyekiti, Serikali inaendelea kupambana na changamoto katika sekta nzima ya elimu; kutoa elimu bure kuanzia darasa la awali hadi sekondari kuwezeshwe kwani shule nyingi kuwa na madarasa ya awali ni hatua nzuri na inahitaji kupongezwa kwani watoto wetu wanapata elimu wakiwa katika vyumba vya madarasa salama kabisa tofauti na hapo awali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, bado changamoto zipo katika sekta ya elimu, baadhi ya maeneo jimboni kwangu tuna changamoto ya matundu ya vyoo, nyumba za Walimu, upungufu wa madarasa, Walimu kulipwa stahiki zao na upungufu wa walimu. Naiomba Serikali kuziangalia changamoto hizi kwa jicho la pekee kwa kuniongezea Walimu, matundu ya vyoo, ujenzi wa nyumba za Walimu na Walimu hawa kulipwa stahiki zao kwa wakati. Mkoa wetu wa Pwani tulikuwa nyuma kielimu ukilinganisha na sasa hivi, changamoto hizi zikiendelea basi zitarudisha juhudi zetu za kuendelea kupandisha kiwango cha elimu jimboni kwangu, matumaini yangu kilio hiki kitapewa kipaumbele kwa maendeleo ya wananchi wangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa uendelezaji wa miji ya kimkakati Tanzania ni mpango mzuri kama ulivyoainishwa na Serikali kwa baadhi ya miji, lakini nina ombi;

katika mpango huu pia Halmashauri yetu ya Kibaha Vijijini ingeingizwa katika mpango huu wenye tija kubwa ya kimaendeleo kwa nchi na eneo husika kwani hukuza nyanja nzima ya ukuaji wa fursa mbalimbali za kiuchumi. Hata hivyo, napenda kukumbusha ahadi ya Mheshimiwa Rais aliyoitoa ya kujenga barabara yenye urefu wa kilometa tano itekelezwe kwani ni muda sasa umepita bila ahadi hiyo kutekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.