Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mafia
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuunga mkono hoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hospitali ya Wilaya ya Mafia ipo katika hali mbaya sana. Kutokana na jiografia yake Wilaya ya Mafia hadhi yake inatakiwa iwe katika kiwango cha hospitali ya mkoa. Hii ni kwa sababu mazingira ya Kisiwa chenye changamoto kubwa ya usafiri, ukosefu wa huduma ya x-ray, vifaa vya maabara, Madaktari na Wauguzi kinapelekea uwepo wa adha kubwa kwa wananchi. Hivyo nikuombe Mheshimiwa Waziri kwa namna ya kipekee atupie jicho hospitali ya Wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Mafia haina kituo cha afya hata kimoja. Naishukuru Serikali imetenga shilingi milioni 500 kwaajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Kirongwe, kutokana na sisi kuwa na maeneo ya pembezoni nilitarajia Mafia ingekuwa katika awamu ya mwanzo ya kupatiwa fedha hizi za ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, tunaomba sana Serikali itekeleze ahadi hii kwani wananchi hususan wakazi wa Tarafa ya Kaskazini wanalazimika kusafiri masafa marefu kufuata huduma ya afya. Wananchi hawa wamefarijika sana na taarifa za ujenzi wa kituo cha hiki cha afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hayo hospitali ya Wilaya ambulance iliyopo ni kuukuu na inaharibika mara kwa mara. Kwa mazingira ya Mafia tunahitaji kuwa na ambulance mpya na ya uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni pamoja na Mafia kuwa Kisiwa ndani yake kuna visiwa vingine vidogo ambavyo wanaishi watu; Visiwa hivyo ni kama Juani, Jibondo, Chole na Bwejuu ambapo kuna zahanati za Serikali. Kwenye visiwa hivyo, kuna changamoto kubwa ya kuvifikia na kuna wagonjwa wanaopata rufaa ya kuja katika hospitali ya wilaya, hakuna ambulance boat ya kuwaleta na kuwapeleka akinamama wajawazito, kupanda mitumbwi na vyombo vingine ambavyo si salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeangalia katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI ametoa boats kwenye maeneo mengine ambayo yanaweza kufikika kwa barabara lakini kumepewa boat. Hivyo kwa namna ya kipekee, naomba kuwasilisha ombi la wananchi wa Mafia kutoka katika Visiwa vidogo vya Juani, Kibondo, Chole na Bwejuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la elimu pia ni changamoto katika Kisiwa cha Mafia. Tunaishukuru Serikali tumepata shule za kata, lakini uhaba wa Walimu hususani Walimu wa sayansi limekuwa ni tatizo, tunaomba Serikali ituongezee Walimu wa sayansi ili kiwango cha ufaulu kiongezeke. Sambamba na hili ujenzi wa mabweni hususani kwa wanafunzi wasichana, kwa mfano Kata ya Kirongwe yenye shule ya sekondari Kirongwe wanafunzi kutoka Kijiji cha Jiji na Banja wanalazimika kusafiri masafa marefu karibu kilometa 10-15 kila siku jambo ambalo si salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la utendaji wa TARURA Wilaya ya Mafia linatakiwa kutupiwa macho. Mpaka sasa barabara na madaraja katika Wilaya ya Mafia hakuna kilichofanyika, kwa mfano, barabara ya kunganisha Kijiji cha Banja na Jiji inapitika kwa tabu hasa kipindi hiki cha mvua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja.