Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa nami ni mara ya kwanza kuchangia hoja katika kipindi hiki cha bajeti, naomba pia nichukue fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema na kuweza kunifanya niwepo hapa.
Pia nawashukuru sana wananchi wa Jimbo la Ilemela kwa imani yao kubwa ambapo walipata mateso kwa miaka mitano bila huduma kwa jamii, lakini wakaamua kuachana na hiyo na kurudisha Chama cha Mapinduzi kuweza kuongoza Jimbo lile. Nasema sitawaangusha, tuko pamoja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuniamini na kunipa dhamana hii kuweza kuwa msaidizi wake katika Serikali hii ya Awamu ya Tano. Nachukua fursa hii pia kupongeza na kuishukuru familia yangu hasa muwe wangu Julius Mabula, watoto kwa namna ambavyo wamekuwa wavumilivu kwa muda wote niko hapa; nawashukuru ndugu, jamaa na marafiki ambao wamekuwa karibu sana kuhakikisha kazi yangu ya uwakilishi inakwenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoe pongezi sana kwa Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayofanya, Makamu wa Rais na hasa kwa kuwa ni mwana mama, Waziri Mkuu, Mawaziri na Manaibu Waziri, Wabunge wote lakini pongezi za dhati sana kwa Wizara husika ambayo leo tunajadili hoja yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichangie machache kuhusiana na Wizara yangu kama jinsi ambavyo yameguswa na wachangiaji wakati wakichangia hoja ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Nianze na migogoro. Naomba niseme wazi, migogoro ipo mingi, ndiyo maana Wizara imechukua hatua ya kupeleka waraka katika mikoa kuwataka waweze kuzungumzia migogoro iliyopo na chanzo chake ili tuweze kuona namna ya kuitatua.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukumbuke suala la migogoro ya ardhi ni suala mtambuka, haligusi Wizara moja, ndiyo maana limeingia sana katika mifugo na wakulima kule, lakini kwenye ardhi lipo, ukienda TAMISEMI lipo, ukiingia Maliasili na Utalii lipo, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) lipo. Kwa hiyo, suala hili kama Wizara tumeshaanza mchakato wa kukaa pamoja tuweze kulipitia kwa pamoja. Kwa hiyo, tukipata zile taarifa za mikoani, tutajua chanzo cha migogoro ni nini?
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ardhi imekuwa ni tatizo na ni chanzo kikubwa, basi tutajua. Inatokana na wananchi kuvamia maeneo? Inatokana na wakulima kukosa maeneo ya kutosha? Au inatokana na wafugaji pengine kutopata maeneo? Je, mazingira tunayalinda? Kwa hiyo, ili tuweze kupata ufumbuzi wa kweli ni lazima hizi Wizara zikae pamoja kama ambavyo tumekwishaanza tuweze kuona chanzo na namna bora ya kuweza kutatua. Kama ardhi imekuwa ni tatizo, pengine tuweze kuona namna ambavyo tunaweza kulitatua.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia mpango wa matumizi bora ya ardhi nao ni changamoto. Kwa hiyo, ni lazima pia tuangalie. Kuna wengine walitoa hoja kabla ya kilimo, suala la viongozi kupewa maeneo. Haikataliwi kama amefuata sheria, lakini suala la msingi ni je, sheria zimezingatiwa? Kwa hiyo, hapa tunasimamia ile Sheria ya Ardhi Namba (4) na Namba (5) ya mwaka 1999, kuona ni kweli limefuatwa. Kwa sababu kuna process ndefu ya kupata eneo. Lazima utapitia katika vikao husika. Vikao hivi kama vinakiukwa ndipo hapo ambapo unaona matatizo yanakuwepo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wakati mwingine tamaa za viongozi katika maeneo ya chini kuweza kutaka kumilikisha watu kwa kukiuka taratibu. Pia na siasa inaingia. Tukiondoa siasa katika suala la umilikaji wa ardhi, migogoro ya wakulima na wafugaji, migogoro ya ardhi itapungua sana, kwa sababu kila mmoja anaguswa katika eneo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara imezungumzia suala la kuwezesha vijana na sisi kama Wizara tunasema sawa. Wamezungumzia suala la kurejesha ardhi na kuwapa, lakini bado niseme Halmashauri zetu zitahusika sana kutambua yale maeneo na kuweza kujua ni jinsi gani vijana hawa tunawapa ili waweze kujikita katika uzalishaji ambao utakwenda vizuri katika kujipatia kipato.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala pia la wavuvi. Naomba ku-declare interest kwa sababu Jimbo ninalotoka ni la wavuvi. Kama Serikali ilivyozungumza, nami naomba, kwa sababu Sheria ya Uvuvi itakwenda kupitiwa upya, niwatake sana watu wa Jimbo langu na wale wote wanaotoka katika maeneo ya uvuvi waweze kuchangia mawazo yao ili sheria ile itakapokuwa imetoka, maoni yao yaweze kuwa yameingia. Walikuja kwa timu ya uongozi wakatoa kero zao nyingi, Waziri aliwapokea, tulikwenda nao na sisi tunasema kama Serikali tutayapitia haya kwa sababu kilio kinapotolewa ni lazima pia upitie, lakini nao wana sehemu kubwa ya kuchangia katika Muswada ule utakapokuwa umeanza mchakato wake, watoe mawazo yao ili tuweze kujua ni jinsi gani migogoro hii inakwisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, Upinzani wamezungumzia suala zima la Tume ile ya Bunge iliyoundwa katika kuchunguza migogoro na wakataka kujua ni maazimio mangapi yametekelezwa. Naomba niwahakikishe tu kwamba Wizara imeyashughulikia na kwa sababu yalikuwa yanagusa maeneo mengi, ndiyo maana ilikwenda kuwa chini ya Wizara ya Waziri Mkuu.
Kwa hiyo, yale ambayo yanatugusa, yapo, tumeainisha na tutayatoa wakati wa hotuba ya bajeti ya kwetu. Kwa hiyo, niseme tu kwamba kila ambacho kimezungumziwa tuko tunaendelea nacho kukifanyia kazi tukijua wazi kabisa kwamba bila kufanya utatuzi huu itatuletea shida katika namna bora ya kupanga maendeleo katika Wizara na katika Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo lingine ambalo limezungumziwa ni la kiusalama zaidi, kwenye usalama wa wavuvi ndani ya ziwa. Waziri mwenye dhamana tayari alishalichukua nalo linafanyiwa kazi kuhakikisha kwamba usalama wa wavuvi wetu unakuwa katika hali ambayo ni ya ulinzi zaidi. Bahati nzuri Waziri mwenye dhamana naye ana interest katika hilo. Naomba kusema tu kwamba tuko pamoja katika hilo.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAAZI: Niliambiwa dakika kumi, siyo tano Mheshimiwa.
NAIBU SPIKA: Ni kumi, ulishagongewa ya kwanza tayari.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.