Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Aysharose Ndogholi Mattembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuipongeza hotuba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitapenda kuchangia katika maeneo matatu; eneo la kwanza ni uhaba wa watumishi. Suala hili limekuwa likiathiri kwa kiasi kikubwa utoaji wa huduma kwa wananchi na kupunguza ufanisi katika utendaji wa kazi katika halmashauri zetu na limekuwa ni la muda mrefu hata kabla ya uhakiki wa watumishi hewa na wasiokuwa na sifa, malalamiko yalikuwa ni makubwa na baada ya zoezi hilo likaongeza zaidi makali ya changamoto hii ya uhaba wa watumishi. Mfano, katika Mkoa wangu wa Singida, Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama pekee ina upungufu wa watumishi 462 katika Sekta ya Afya; Manyoni uhaba wa watumishi 446; Itigi watumishi 269 na Ikungi 822.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa takwimu hizi unaweza kuona jinsi gani changamoto hii ilivyo kubwa. Naishukuru Serikali kwa kukubali ushauri na kuwarejesha watumishi kazini kulingana na sifa zao, lakini naishauri ni vyema sasa ikaja na mikakati ya makusudi ya kuajiri watumishi wengi ili kuziba upungufu uliopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo napenda kulichangia ni ucheleweshwaji wa fedha za shughuli za maendeleo katika halmashauri zetu. Suala hili limesababisha kukwama kwa miradi mingi au kutokukamilika kwa miradi kwa wakati na kuisababishia Serikali hasara na kwa upande wa wananchi imekuwa ni kero kubwa kusubiri mradi kwa muda mrefu na hivyo kuwakosesha huduma muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua kwamba bajeti yetu hutegemea makusanyo ya mapato kwa mwezi, lakini uhalisia wa kiasi cha fedha tunachokiidhinisha katika shughuli za maendeleo kinatofautiana kwa kiasi kikubwa cha fedha zinazopelekwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali ni vyema sasa ikajitathmini na kurekebisha hali hii, miongoni mwa mikakati ya kujirekebisha na kujitathmini ni kupeleka fedha zlizobaki za miradi ya maendeleo katika Mkoa wangu wa Singida. Ni vyema Serikali ikaimarisha ukusanyaji wa mapato kwa njia ya kisasa (kielektroniki) ikiwemo elimu ya mlipakodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la mwisho ambalo napenda kulichangia ni asilimia 10 ya mikopo kwa vikundi vya wanawake na vijana zitokanazo na mapato ya ndani katika halmashauri zetu. Imekuwa ni kawaida kwa Maafisa Masuuli kutokupeleka kwa makusudi au kutokupeleka kwa wakati asilimia 10 ya mikopo kwa vikundi vya wanawake na vijana. Muda uliopita nilikuwa ni Mjumbe wa Kamati ya LAAC na tatizo hili tumekuwa tukikutana nalo kila mara tulipokwenda kufanya ukaguzi katika halmashauri zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikumbukwe kwamba wanawake na vijana hawa ndio makundi muhimu na nguvu kazi ya Taifa katika kukuza uchumi lakini wengi wao hawana dhamana ya kukopa katika mabenki na taasisi za fedha kwa kutopeleka asilimia 10 ya mikopo kwa vikundi vya vijana na wanawake ni kuwakosesha fursa ya kukua kiuchumi. Naishauri Serikali ije na mikakati mahususi ambayo itawabana Maafisa Masuuli waweze kupeleka asilimia 10 za mikopo kwa vikundi vya vijana na wanawake kwa kiasi kikubwa kinachotakiwa na kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niishauri Serikali iimarishe Idara ya Maendeleo ya Jamii ili iweze kufanya kazi yake ipasavyo kwa kukaa na makundi haya na kuwaelimisha juu ya mikopo hiyo hatimaye iweze kuleta tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, nawapongeza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Mheshimiwa Jafo na Naibu Mawaziri, Mheshimiwa Kandege na Mheshimiwa Kakunda kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya ya kuwaletea wananchi maendeleo; nawatia moyo waendelee na kasi hiyohiyo ya utendaji wa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na naunga mkono hoja.