Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali Wizara ya Maji na Umwagiliaji 2018/2019

Hon. John John Mnyika

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Kibamba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali Wizara ya Maji na Umwagiliaji 2018/2019

MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Toka jana nimekuwa nikisikiliza michango ya Waheshimiwa Wabunge wenzangu pamoja na leo na nimepitia taarifa ya Kamati na nimetafakari katika miaka niliyokaa Bungeni, nimekuja kugundua kwamba kwa miaka nane kwa kweli Bunge hili linajadili mambo yale yale, yaani ukiwa umeingia Bungeni leo tu au jana ukawa hujasikiliza Bunge huko nyuma, unaweza kufikiri sasa kuna Chama na Serikali mpya katika Bunge hili inajaribu kurekebisha mambo ya zamani. Kumbe ni chama kile kile na Serikali ile ile. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, sentensi moja ambayo iko bayana katika haya ni kwamba ninyi mmeshindwa kutekeleza na kutimiza matakwa ya wananchi kwenye masuala ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kabla sijaendelea mbele nisisitize ninachoendelea kusisitiza kwamba tiba ya kudumu ya haya matatizo tuliyonayo ni wananchi wa Tanzania kuwaondoa Serikali ya CCM madarakani na kuweka Serikali nyingine katika utawala wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wewe utakuwa unakumbuka vizuri kwa sababu ulikuwa kwenye kiti hicho hicho wakati ukiwa Naibu Spika. Tarehe 4 Februari, 2013 nilipoleta hoja Bungeni hapa juu ya maji Dar es Saalam na maji vijijini na namna ambavyo Wabunge wa CCM wakati huo Mheshimiwa Rais akiwa ndani ya Bunge, akiwa Waziri wa Ujenzi naye akisikiliza mlivyoshabikia kwa pamoja kwamba mambo yapo kwenye mkondo sahihi, kila kitu kipo sawasawa, hoja hii iondolewe isijadiliwe, hatimaye maji yakasababisha vurugu kubwa sana hapa Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa miaka mitatu au miwili na ushee, toka mwaka 2016 hadi 2017 na mpaka sasa mlinyamaza kimya kusema kuhusu maji, nikifikiri kwamba Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli kwa sababu alikuwa Mbunge anayajua vizuri matatizo haya ya maji na kwa sababu alikuja hapa Bungeni akaahidi kwamba ifikapo mwaka 2020 asilimia 95 ya wananchi mijini ikiwemo Dar es Salaam watakuwa na maji na asilimia 85 wa vijijini watakuwa na maji, nikafikiri kwamba kutakuwa na tofauti. Nimekuja kugundua kwamba Mheshimiwa Magufuli ni yule yule na CCM ni ile ile, mambo ni yale yale. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa huwa tunajengewa matumaini sana. Mwaka 2006, mwaka 2007 katika Bunge la Bajeti Waheshimwia Wabunge walisema mambo haya haya ambayo wanasema sasa tukajengewa matumaini wakati wa majumuisho ya Serikali kwamba kutakuwa na mabadiliko. Safari hii mmekuja na mkakati huo huo; na sasa kuna debate ya tozo ya mafuta ya shilingi 50 ili ikishafika hatua ya majumuisho Serikali iki-coincide kutoa tozo ya shilingi 50 watu walainike wote, bajeti ipite, halafu mambo yaendelee kuwa yale yale. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Kamati inasema mpaka mwezi Machi Serikali imetoa asilimia 22 tu ya pesa za maendeleo. Hizi asilimia 22 za pesa maendeleo ni katika bajeti ya maji ambayo imepunguzwa badala ya kuingezwa kutoka bajeti iliyotangulia. Halafu kwenye umwagiliaji haIi ni mbaya zaidi asiliamia 12 na kati ya hiyo 12 pesa za ndani ni 0.8. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika suala la sukari ulisimama ukataka kuonesha ukali. Maji katika maisha ya wananchi ni zaidi ya sukari kwa sababu ukikosa sukari unaweza ukanywa chai bila sukari. Katika suala la mafuta umeonesha ukali, maji ni zaidi ya mafuta, kwa sababu ukikosa mafuta unaweza ukapika bila ya mafuta. Ila ukikosa maji huwezi kunywa bia, ukikosa maji huwezi..., ni uhai. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, onesha ukali wako katika hili. Na mimi nakuomba ukubali, kwa sababu tumeishauri Serikali vya kutosha sana, lakini haisikii. Sasa nani wakati Bunge kutumia mamlaka yake ya Kikatiba kuisimamia Serikali. Mamlaka hayo yanaanza kwa kukubaliana kwamba hii bajeti ya Wizara ya Maji tusiipitishe sasa. Tukubaliane kwamba hii bajeti ya Wizara ya Maji tusiipitishe sasa. Sasa najua kwamba Waheshimiwa Wabunge wenzangu wana shauku sana ya kuchangia.

Mheshimiwa Spika, ingekuwa siyo shauku ya Waheshimiwa Wabunge wenzangu, ningesema nasimama sasa hivi kwa mujibu wa Kanuni ya 69(1) ambayo inaruhusu Mbunge kusimama wakati wowote kutoa hoja ya kwamba mjadala uahirishwe. Ningeweza kabisa kusema kwamba mjadala uahirishwe, sasa ni mwezi Mei na kuna bajeti zinajadiliwa mpaka mwanzoni mwa mwezi Juni, tungesema mjadala uahirishwe mpaka mwishoni mwa Mei ili Serikali katika makusanyo yake ya mwezi huu wa Serikali iingize pesa katika Wizara ya Maji, tuvuke kutoka hii asilimia 22, tufike juu ya asilimia 22.

Mheshimiwa Spika, tuna uwezo kabisa wa kufanya hivyo kwa kanuni za Bunge na tuna haki hiyo. Kwa sababu Waheshimwia Wabunge wenzangu wana shauku ya kuendelea kuchangia, bado tunayo nafasi hiyo.

Mheshimiwa Spika, ruhusu Wabunge wengine waendelee kuchangia lakini wakishamaliza kuchangia kesho, Serikali isiruhusiwe kuhitimisha, mjadala uahirishwe na nipewe nafasi ya kutoa hoja hiyo kesho, mjadala uahirishwe mpaka tarehe ngapi kwa mujibu wa kanuni.

T A A R I F A . . .

MHE. JOHN J. MNYIKA. Mheshimiwa Spika, nilisema awali kwamba ni mbinu tu ya kukwepesha hii bajeti ipite.

Mheshimiwa Spika, tulishapitisha bajeti hii ambayo Serikali imetoa asilimia 22. Serikali ikishapitisha Bajeti ni wajibu wa Serikali kutoa pesa. Nasema tuahirishe mjadala ili Serikali ilazimishwe kutoa hizo pesa. Sasa masuala ya tozo ni masuala ya kwamba tunakwendaje mbele? Tukifika huko napo hata katika tozo, kuna tozo zinatozwa na bado pesa nyingine haziendi vilevile. Kama ilivyo kwenye maji, kama ilivyo kwenye umeme, kwenye REA, hiyo ni jambo lingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niendelee, Waheshimiwa Wabunge mbalimbali wameeleza na kwa miaka kadhaa tumeeleza kuhusu ufisadi katika sekta ya maji na miradi ya ambayo kimsingi ni miradi ambayo imejengwa lakini maji hayatoki na matumizi mabaya ya fedha katika masuala ya miradi ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hali hii imeendelea, ipo katika sura nyingi hata mtu akisoma kitabu hiki cha Mheshimiwa Waziri, ukiangalia tu uchimbaji wa visima vya DCCA kuanzia ukurasa wa 267 utaona jinsi ambavyo Mheshimiwa Waziri anavyojipendelea katika Mkoa wa Katavi na katika Jimbo lake. Mimi nazungumzia kipengele cha matumizi mabaya ya fedha za miradi ya maji katika maeneo mbalimbali ya nchini na miradi ya maji kutokufanya kazi.

Mheshimiwa Spika, katika mazingira ya kero nyingi za ufisadi wa namna hii unaozungumzwa, nitaomba nafasi na ninaomba nitoe notice kabisa kwa mujibu wa Kanuni ya 120 ya Kanuni za Bunge 2A kwamba baada ya mjadala huu kukamilika, nipewe nafasi ya kutoa hoja ya kuundwa kwa Kamati teule ya kwenda kuchunguza masuala ya ufisadi na miradi mibovu katika masula ya maji maeneo yote nchini na katika maeneo mbalimbali nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wewe umeonesha kutaka kuunda Kamati za kiuchunguzi, umeunda Kamati ya Gesi, umeunda Kamati ya Tanzanite, umeunda Kamati ya Almasi na umeunda Kamati mbalimbali, lakini hizi Kamati zako ambazo taarifa zake hazijadiliwi humu Bungeni na Wabunge wote, sasa katika hili kwa sababu ya uzito wake iiundwe Kamati Teule ili ikachunguze na taarifa iletwe Bungeni ijadiliwe na hatua zichukuliwe. Ahsante sana.