Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali Wizara ya Maji na Umwagiliaji 2018/2019

Hon. Livingstone Joseph Lusinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtera

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali Wizara ya Maji na Umwagiliaji 2018/2019

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, namshukuru Mungu kupata nafasi asubuhi hii ili nami niweze kuchangia Wizara hii ya Maji ambayo nyeti na muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Mtera niweze kueleza machache kwa ajili ya Wizara hii ya Maji.

Mheshimiwa Spika, ni maneno mazuri sana yanazungumzwa na Waheshimiwa Wabunge tangu jana mpaka asubuhi hii na wengine wanashauri sasa Serikali hii itolewe ingiizwe Serikali ambayo hamna kitu wala ofisi haina, halafu ilete maji. Vitu vya ajabu sana! Hata aliyeanzisha benki alihakikisha jengo zuri, imara, wahudumu wazuri ili kuweka imani ya watu kuweka hela zao. Lakini hiyo benki nyingine mtu aende akaweke huko, benki ya makuti, ofisi hakuna, matete, haiwezekani. Nadhani alikuwa anajifurahisha, haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya hilo, kama alivyotoa utangulizi aliyezungumza, na mimi naingia kwenye Wizara ya Maji. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri na Naibu wake, wanafanya kazi nzuri. Hata katika umri alionao Engineer tunamwona namna anavyohangaika kwenye Majimbo na mpaka Mheshimiwa Aweso anazidi kutoka kipara kwa kujitwisha ndoo za maji, pamoja na Katibu Mkuu Profesa Kitila Mkumbo, tunawashukuru sana.

Mheshimiwa Spika, Wizara na Maji ni Wizara muhimu sana na kama ikifanikiwa, kwa kiasi kikubwa itapunguza bajeti za Wizara nyingine, maana Wizara hii ni mtambuka, inaweza kusaidia Wizara ya Afya, inaweza kusaidia hata ongezeko la watu mijini. Hivi kwa sisi Wabunge wa vijijini, kwenye vijiji kule hakuna maji, hakuna barabara, hakuna afya, watu wataachaje kuja mjini kuzifuata huduma hizo?

Kwa hiyo, Wizara hii ikiweza kufanya kazi zake sawa sawa, watu wakapata maji safi na salama, baadhi ya magonjwa kama ya matumbo yanafutika kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilikuwa nataka niishauri Serikali, wakati mwingine ijifunze kupitia vitu vidogo. Nataka nichukue nafasi hii kuwashukuru sana watu wa WFP chini ya uongozi wa dada Neema Sitta kwa kazi nzuri waliyoifanya kwenye Jimbo la Mtera.

Mheshimiwa Spika, hapa Mheshimiwa Waziri akinisikiliza vizuri, anaweza kuona namna ambavyo Serikali wakati mwingine inashindwa kusimamia matumizi mazuri tu. Ikisimamia matumizi mazuri, value for money ikazingatiwa, tutapata maji mengi na kwa uhakika.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano watu wa WFP wametupa shilingi milioni 799 kwenye Jimbo la Mtera. Katika milioni hizo hizo 799 tumepata matenki makubwa matatu ya lita 800,000, tumepata visima 18, tumepata mashamba heka 300 kwa ajili ya umwagiliaji, tumepata visima12 vilivyofungwa solar power kwa ajili ya wananchi kupata maji.

Mheshimiwa Spika, hebu angalia matumizi haya ya shilingi milioni 800 tu hizi kasoro moja yameweza kuleta vitu hivyo vikubwa ambavyo wananchi leo hii wananufaika. Ukija kwenye Serikali, hamna kitu. Inatolewa shilingi bilioni moja pale Mkwayungu kwa ajili ya kujenga bwawa la umwagiliaji, bwawa halijakamilika, hakuna miundombinu na shilingi bilioni moja imeliwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, unaweza ukaona matumizi mabaya kwenye miradi ya maji kwa upande wa Serikali yanatuletea matatizo makubwa. Hawa wameweza kutoa shilingi milioni 800 zimetengeneza mambo ambayo ni maajabu kabisa. Mheshimiwa Waziri na Katibu Mkuu na Naibu Waziri piteni mwone kwa macho namna ambavyo pesa ikisimamiwa hata ikiwa kidogo inaweza kufanya vitu vikubwa.

Mheshimiwa Spika, watu wamepata maji ya kunywa, wamepata irrigation wanamwagilia na maisha yao yako safi. Ukienda kwenye Kata ya Fufu katika Vijiji vya Suri, Chibori na Fufu yenyewe, WFP wametufanyia mambo makubwa kwa pesa kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukienda mahali pengi kwenye miradi ya Serikali, hela nyingi zimetumika, zaidi ya shilingi bilioni moja imeliwa pale Mkwayungu na maji hakuna. Kwa hiyo, nakuomba sana, hebu twende tuangalie wenzetu hawa wamewezaje? Wamefanikiwaje? Wamefunga solar system katika visima vyote. Hakuna mwananchi anayehangaika kutafuta bill ya umeme, kutafuta nini na pampu za kisasa, zinazomwagilia mashamba kwa uhakika.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naishauri Serikali, tumepata Makao Makuu ya Nchi, haitakuwa na maana kama Mkoa wa Dodoma hautakuwa scheme za umwagiliaji. Vijana wakiweza kumwagilia huko kwenye Majimbo ya vijijini waleta bidhaa zao hapa mjini, zitakuja kuwanufaisha na wao na watoto wao. (Makofi)

Msheshimiwa Spika, Wizara ya Maji ikijitahidi kusimamia resource kidogo iliyopo, nina uhakika inaweza kutosha kutusukuma mbele. Kwa mfano, nimekuja hapa kuomba maji kwa ajili ya vijiji vyangu; Kijiji cha Loji hakina maji, Kijiji cha Ng’aheleze hakina maji, kijiji cha Handali hakina maji. Hivi ni vijiji vikubwa mnoo! Kijiji cha Ng’ng’i leo hii kina wakazi karibu 8,000 lakini hakina maji ya uhakika. Halafu Halmashauri baadhi ya visima vya zamani vikiharibika vinashindwa kuvitengeneza. Kwa hiyo, utakuta kuna matatizo ya visima vya zamani na kuna matatizo ya visima vipya, havipatikani.

Mheshimiwa Spika, naomba sana, Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa kujibu, atupatie maji katika Jimbo la Mtera na atupatie maji katika Kijiji cha Muheme.

T A A R I F A . . .

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, taarifa yake wala siwezi kuikataa, naipokea. Naipokea kwa maana ya kwamba akasimamie na pesa alizosema CAG zimeliwa kwenye chama chake, kama anao uwezo huo akasimamie ili ziweze kuleta maendeleo. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilijua tu, ukisikia kelele ujue tayari tiba. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba Mkoa wa Dodoma ambao hamna mito inayotiririka maji kwa msimu mzima, uangaliwe kwa makini hususan katika uchimbaji wa mabwawa. Sisi maji yetu yanapita tu, mvua ikinyesha, yanapita yanaondoka moja kwa moja. Hatuna mito inayotiririsha maji msimu mzima. Kwa hiyo, tunaiomba Wizara ilitazame hilo kama eneo mahususi tukipata mabwawa ya kutosha, tuna uwezo mkubwa sana wa kuzalisha, tuna uwezo mkubwa sana kwa kulima kilimo cha kisasa, tuna uwezo mkubwa sana wa kujisimamia. Tunachotaka Serikali mtuangalie muwe mnafanya research basi, kuna Mkoa huu tofauti yake na Mkoa huu.

Mheshimiwa Spika, WFP wameleta hela kidogo lakini zimefanya mambo makubwa, zimejenga mpaka matanki ya maji ya shule za msingi, hela kidogo hii! Ndiyo maana namwomba Mheshimiwa Waziri na Katibu Mkuu na Naibu Waziri watembelee wakaone, siyo vibaya kuona kwa macho na kuja kusimamia pesa zenu mlizonazo ili ziweze kutusogeza mbele. Hata mabwawa ya zamani yaliyochimbwa enzi za Mwalimu Nyerere, leo hii yapo; mengine yameshajifukia. Liko bwawa la Mkulabi hapa Dodoma Mjini, lipo Bwawa Mlowa Bwawani pale. Mwalimu alichimba mabwawa makubwa lakini leo hii hayana maana yoyote.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa naomba sana atakaposimama Mheshimiwa Waziri atusaidie sana kupata maji katika vijiji nilivyovitaja vya Jimbo la Mtera na kuhakikisha kwamba tunapata kilimo cha umwagiliaji. Mbona nimewaomba sana kwenda Mkwayungu kuona ule mradi ambao Serikali imetumbukiza shilingi bilioni moja, lakini hamna kitu chochote? Mbona hamuendi? Twendeni mkaone kwa macho ili mfananishe yale yaliyofanyika pale Mkwayungu na ambayo wenzenu wanaweza kufanya.

Mheshimiwa Spika, tukifanya namna hiyo tutakuwa tunazuia ulaji, tutakuwa tunazuia wizi na umangimeza na nina uhakika Serikali ya Awamu ya Tano itazuia mambo hayo na ndiyo maana nawasihi mfike mwone ufisadi uliofanyika, mchukue hatua ili wananchi wa Kijiji cha Mkwayungu waweze kupata maendeleo kwa kilimo cha umwagiliaji ambacho kilikusudiwa kufanyika eneo lile.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema maneno hayo, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na naipongeza sana Serikali kwa kazi nzuri mnayoifanya. Wizara hii lazima iwe na kelele kwa sababu maji ni muhimu sana. Tunataka kuwatua ndoo kichwani akina mama. Tusiwatue wa mijini tu, hebu tazameni na Majimbo ya vijijini jamani. Vijijini nako kuna akina mama wengi wanaoteseka, wanatoa maji mbali, wanachelewa kufanya kazi zao za kujiletea maendeleo.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri anafanya ziara mwenyewe anakutana na hiyo hali, tusaidieni na sisi Wabunge wa vijijini. Hawa wa mjini ambao wana lami, wana hospitali nzuri na nini, nao kwa maji wangesubiri kidogo, geukieni upande mwingine.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, ahsante na ninaunga mokono hoja.