Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali Wizara ya Maji na Umwagiliaji 2018/2019

Hon. Khadija Hassan Aboud

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali Wizara ya Maji na Umwagiliaji 2018/2019

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Kwanza kabisa nachukua fursa hii kuipongeza Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa jitihada zake zote inazofanya kuwasaidia wananchi wa Tanzania katika kuwaletea maendeleo na pia kuwasaidia kupata huduma muhimu ikiwemo ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naanza na Mfuko wa Maji ambao ni chanzo muhimu sana cha upatikanaji wa fedha za kusaidia maendeleo ya maji na tumeona ufanisi wake kwa kipindi hiki kwa kufanyiwa mpango na Serikali kutoza tozo ya shilingi 50 kwa kila lita. Ombi langu kwa Serikali, tuongeze tena shilingi 50 kwa kila lita ya mafuta ya petroli na dizeli ili kuufanya mfuko huu ukusanye jumla ya shilingi bilioni 316, fedha hizi zikipatikana zitasaidia sana miradi ya maji vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, taasisi za maji au Mamlaka za Maji zinakabiliwa na madeni makubwa ya maji kwa takribani shilingi bilioni 38. Naishauri Serikali ili Mamlaka za Maji ziweze kujiendesha na kuongeza huduma za maji kwa wananchi, madeni haya yalipwe kwa haraka ili mamlaka zetu ziweze kujiendesha na kutanua huduma za maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naipongeza Wizara ya Maji kwa kuanzisha prepaid meter ambazo zitasaidia sasa, wale wadaiwa sugu wa maji watakuwa hawana tena njia ya kukwepa kulipa madeni hayo. Namshauri Mheshimiwa Waziri, hizi prepaid meter watakapozifunga, wazianzishe kwa wale wadaiwa sugu wa madeni makubwa ya maji, muanzie huko. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maji yanahitaji dawa za kusafishia na kutibu. Katiba dawa za kusafishia na kutibu maji, naishauri Serikali iondoe au ipunguze kodi ili dawa hizi zipatikane kwa nafuu ili kumpunguzia mzigo mwananchi kwa sababu dawa hizi zinagharimu fedha nyingi na ni lazima tuzipate ili tusafishe maji yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashauri au nakubaliana na wazo la Wizara kwa kuhamasisha wananchi sasa katika Halmashauri, Wilaya na Mikoa na maeneo yote yanayojengwa, uvunaji wa maji ya mvua. Maji ya mvua uvunaji wake baada ya kutengeneza miundombinu inakuwa ni rahisi na salama na hayahitaji tena madeni makubwa ya kulipia umeme katika kuyavuta maji. (Makofi)

Kwa hiyo, tukihamasishana sisi wananchi katika uvunaji wa maji ya mvua, hii itasaidia sana kutatua baadhi ya matatizo hasa kwenye kilimo na mifugo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naipongeza Wizara kwa kuanzisha Wakala wa Maji Vijijini. Wakala wa Maji Vijijini itaisaidia sasa Wizara kusimamia moja kwa moja miradi ya maji lakini pia itasimamia moja kwa moja matumizi ya fedha za miradi ya maji na kufuatilia maendeleo yake kwa haraka zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikiendelea, niongelee kuhusu Tume ya Umwagiliaji. Tume hii ndiyo chemchem na chimbuko la kilimo cha umwagiliaji. Hivyo ni vyema basi fedha zinazotengwa kwa ajili ya Tume ya Umwagiliaji zipelekwe kwa wakati na pia kutafuta vyanzo mbalimbali vya fedha vya kusaidia Tume hii ya Umwagiliaji ili kuweza kutekeleza majukumu yake, kwani kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa na mabadiliko ya tabianchi kilimo chetu kimekuwa kinayumba. Kwa hiyo, kilimo cha kumwagilia ndiyo kilimo kitakachomkomboa mwananchi wa kijijini katika kukamilisha azma ya kujiletea uchumi wa maendeleo, uchumi wa viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna upungufu mkubwa wa wataalam wa maji na umwagiliaji, naishauri Wizara inayohusika na kuajiri itoe kibali sasa, Wizara iajiri wataalam hao wa maji na pia wataalam wa umwagiliaji ili kuweza kutekeleza majukumu ya kumsaidia mwananchi katika kilimo bora na pia kumsaidia mwananchi kule aliko kijijini kwenye Mamlaka za Maji na Halmashauri kuweza kupata wataalam wa maji na miundombinu ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda kuipongeza Serikali kwa hatua iliyochukua ya kukaribia kukamilisha zile fedha za miradi ya maji ya Mfuko wa India ambazo fedha hizi zikipatikana zitasaidia miji 17 ya Tanzania kupata maji. Hapo tutakuwa tumetatua tatizo kwa kiasi fulani la upungufu wa maji ndani ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika kudhibiti maji yasipotee, hatua ya Wizara ya kutengeneza miundombinu ya maji iliyo chakavu na kutengeneza mingine mipya ili kudhibiti maji yasipotee kiholea, nashauri suala hili litiliwe mkazo. Katika kutengeneza miundombinu hiyo ya maji na kuanzisha mingine mipya, tuangalie ubora wa vifaa, mitambo na miundombinu hiyo kwa sababu inaelekea kuna baadhi ya vifaa na miundombinu ni mpya lakini tayari imeshakuwa chakavu na inavujisha maji ovyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika uhifadhi wa vyanzo vya maji, naipongeza Serikali kwa kuhifadhi vyanzo vya maji vyote nchini na pia kuongeza vyanzo vipya vya maji na kuvifanya kuwa maeneo tengefu. Hili la uhifadhi wa vyanzo vya maji linahitaji sote wananchi tulipe kipaumbele kwa sababu baadhi ya vyanzo vya maji wananchi wanavichafua kwa makusudi. Kwa hiyo, jitihada za wazi zinahitajika katika kuhifadhi vyanzo vyetu vya maji ambavyo ndiyo chanzo kikuu cha maji. Tuvihifadhi na tuviwekee uangalifu wa kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niende kwenye Chuo cha Maji, hiki ndiyo chuo ambacho kwa Tanzania hii kinatoa wataalam wa maji na wataalam wa uchimbaji wa visima na mambo mengine.

Mheshimiwa Spika, nashauri chuo hiki kiendelee kuongeza wanafunzi na kuongezewa fedha ili tupate wataalam wengi wa maji, tuwasambaze vijijini kote ili wakasaidie miradi ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu Wakala wa Uchimbaji Visima (DDCA), nashauri Serikali, kwa sababu hiki kitengo ndiyo kinachosaidia kuchimba visima na mabwawa ndani ya nchi yetu, kiongezewe mitambo ya kisasa na wataalam wa kisasa wanaoweza kuchunguza maji ndani ya Tanzania yetu, wapi yapo, yapo kwa kima gani, kwa ukubwa gani, kwa mita ngapi ili tuweze kufanya kazi ya uchimbaji wa visima kwa usahihi zaidi na kuepusha kuchimba visima ambavyo baadaye havitoi maji.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hii DDCA inatakiwa ijengewe uwezo wa kutosha na vijana wetu watakaotoka DDCA wasambazwe wilayani na mikoani ili kusaidia uchimbaji wa visima, mabwawa na utengenezaji wa mabwawa ya kuvunia maji ili wananchi tuvune maji na tupate maji kwa uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho namalizia kwa kusema naipongeza Wizara kwa jitihada zake. Suala la maji ni la msingi, wananchi tunahitaji maji, mimea inahitaji maji, wanyama wanahitaji maji. Suala la maji sasa hivi Serikali tumejitwisha kwenye mabega, inafaa kwa wakati huu tuliweke kichwani liwe ndiyo agenda kubwa ya maji katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana nakushukuru.