Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali Wizara ya Maji na Umwagiliaji 2018/2019

Hon. Susan Limbweni Kiwanga

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Mlimba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali Wizara ya Maji na Umwagiliaji 2018/2019

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante naomba nilindiwe dakika zangu.

Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa hiii nafasi na naanza moja kwa moja kwa sababu dakika zenyewe tano, kwamba miaka mitatu mfululizo kwa mujibu wa vitabu vyao na takwimu zinaonesha kwamba Serikali ya CCM ilikuwa tunapitisha bajeti Bungeni mabilioni ya pesa, lakini ni asilimia 26 tu ya pesa tunazopitisha na Bunge ndiyo zinaenda kufanya kazi ya maji. Ndiyo maana tunapotaka kusema kwamba hii bajeti ukilinganisha na bajeti ya ndege yaani ni mara mbili ya bajeti ya maji. Sasa tukisema Serikali ya CCM kipaumbele chake ni ndege siyo maji mnakataa nini? Tukisema Serikali ya CCM inashughulikia maendeleo ya vitu badala ya watu mnakataa nini?(Makofi)

Mheshimiwa Spika, hiyo ni hatari kwa Taifa letu, ndiyo hivyo hivyo Mheshimiwa Jenista siku ile alinipunja dakika zangu unamwona yule ameshaanza. Nilindie dakika zangu Mheshimiwa Spika.

T A A R I F A . . .

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Spika, Bunge lingekuwa live ingekuwa tamu sana. Hii taarifa siipokei kwa asilimia 220 kwa vile umekuwa Waziri sasa ndiyo maana unasema hayo unayoyasema, ulivyokuwa unakaa hapa mbona ulikuwa husemi hivyo, acha hizo wewe. (Kicheko/ Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi namuuliza huyo aliyesema hiyo taarifa kama nyumbani kwake ana shilingi 100 na chakula cha watoto kinagharimu shilingi 80 na anataka aende akajenge nyumba ya shilingi 100, je atatoa 100 kwenda kujenga nyumba au atalisha kwanza watoto? Acha hizo wewe! (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, ninasema hapa nikiwa na uchungu mkubwa, leo ndani ya Jimbo la Mlimba Naibu Waziri nakushukuru ulienda na mimi mama yako, uliona wananchi wa Mlimba walivyokulilia na wewe ukashuka ukalia nao. Machozi yananitoka, wanaimba Mlimba maji, Mlimba maji, mito mingi lakini kuna kisima kimoja, haki ya Mungu nasema akina mama, watoto, wazee wanapata maji kwa wiki moja mpaka wiki mbili kwa mzunguko. Naibu Waziri umewaona wananchi wa Mlimba, leo unaniambia kipaumbele ndege wewe Mungu atakulaani Kigwangalla, haki ya Mungu nasema hapa nikimaanisha. Ukiniambia leo kianze nini nasema maji, wananchi wa Mlimba wanataka maji. Kuna mito mingi lakini inatuharibu wakati wa mvua, inatupasulia nyumba, barabara lakini ikiisha mvua hakuna maji, nataka maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tulipita na Naibu Waziri kuna mradi mkubwa wa umwagiliaji pale Njage, Kata ya Mchombe Serikali imeingiza hela nyingi lakini cha kushangaza ule mradi wanamwagilia wakati wa mvua, wakati wa kiangazi hakuna maji. Ndiyo maana tunaomba tuwekeze kwenye kilimo cha umwagiliaji kwa kuchimba mabwawa ili kuleta tija kwa pesa mnazopeleka, kwa mfano pale Njage Serikali itenge pesa kwa kujenga bwawa ili tukinge maji ya mvua, tumwagilie na tupate mpunga masika na kiangazi.

Mheshimiwa Spika, maji ni uhai, hapa wote mmeoga maji, mnakunywa maji, hebu mkae hapa Mawaziri wote na wote tusioge angalau siku mbili tuone kama tutafungua air condition humu ndani! Maji ni kipaumbele.(Kicheko)

Mheshimiwa Spika, sasa nataka niseme kwa Watanzania Serikali ya CCM ya Awamu ya Tano inashughulikia vitu siyo maendeleo ya watu hiyo haiwezekani. Muda haunitoshi mpaka nimelia.

T A A R I F A . . .

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Spika, taarifa yake naipokea kwa tahadhari kwa kuwaambia kwamba wananchi wa kule Jimboni kwake wanakunywa tope, tena pamoja na punda. Naikataa kwamba, kipaumbele, eti vitu kwanza, wewe vipi? Yaani wewe uanze kwanza kujenga nyumba watoto ndani wasile? (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, nyumba yenyewe unajenga na maji, viwanda vyenyewe maji, umeme Stiglers’ Gorge maji, kila kitu maji, leo unasema maji siyo kipaumbele. Tunataka kipaumbele kiende kwanza, halafu hivi vingine vitakuja, hamuwezi mkatunanihii, Serikali ya CCM ya Awamu ya Tano inafanya maendeleo ya vitu siyo maendeleo ya watu, ndiyo maana mnapeleka asilimia ndogo sana kwenye masuala muhimu kama ya maji. Naomba wapeni pesa hawa Mawaziri ili wafanye kazi.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Hata kwenye Jimbo lako la Kongwa tunapita barabarani tunaona watu wanavyokwangua maji. Kwanza ni aibu barabara kubwa inayokuja Makao Makuu watu wanachota maji kwenye madimbwi, shame Tanzania, shame CCM. Hebu boresheni wapeni pesa za kutosha kama tunavyopitisha, ili watuletee tuwasulubu Mawaziri, kwa sasa hivi hatuwezi kuwasulubu wanajitahidi lakini hawana pesa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama alivyoomba Mheshimiwa Mnyika badala ya bajeti hii tufanye kweli, mbona tulifanya kweli kwenye Wizara ya Ujenzi, tuliweka mguu chini wakaenda wakajadili wakaongeza pesa na safari hii tuwaoneshe Bunge kwamba hawa lazima wapewe pesa ili miradi iongezeke huku chini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na Mungu atusimamie.