Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali Wizara ya Maji na Umwagiliaji 2018/2019

Hon. Ezekiel Magolyo Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Msalala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali Wizara ya Maji na Umwagiliaji 2018/2019

MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Spika, naomba nikushukura sana na mimi kunipa nafasi ili nichangie hotuba ya Waziri wa Maji na Umwagilaji.

Kwanza naomba nipongeze sana juhudi zinazofanywa na Serikali hii Awamu Tano na kwa kiasi kikubwa kama ambavyo umesema kwamba kazi inayofanyika wa awamu hii inaonekana dhahiri. Yawezekana katika maeneo mengine yanaweza ikawa haijadhihirika sana lakini wanasema unapotapa ni vizuri ukasema ukweli. Miradi ambayo imeanzishwa na inatekelezwa kwenye Jimbo langu la Msalala kwa sasa hivi ni mingi na mikubwa sana.

Mheshimiwa Spika, utakumbuka mwaka 2014, tulikataa bajeti ya Wizara ya Maji hapa tukitaka fedha zitengwe kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji na hasa vijiji vilivyokuwa kandokando ya bomba kuu la Ziwa Victoria hadi Kahama na Shinyanga. Tuilipitishiwa fedha kwa ajlili ya kuanza kutekelezwa mradi wa Kagongwa Isaka, shilingi bilioni nane, wakati ule Naibu Waziri akiwa Mheshimiwa Amos Makala Waziri wa Maji akiwa Mheshimiwa Profesa Maghembe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mpaka mwaka 2015 mradi ule ulikuwa haujatekelezwa, mwaka 2015 Mheshimiwa Riasi John Pombe Magufuli amechukua nchi, akafika Isaka akasema ndani ya miezi sita mradi huo utakuwa umeanza kutekelezwa. Tumesikia hapa kwamba sasa hivi wakandarasi wako karibu 40 wakitekeleza mradi huu. Naomba pia nimpongeze sana Mheshimiwa Rais, lakini nimpongezea pia Mheshimiwa Wazri na Naibu wake. Kwa kiasi kikubwa wanajitahidi sana kusimamia miradi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nisemee mawili tu ya ujumla ambayo Waheshimiwa Wabunge wengi wameyazungumzia; kwanza usimamizi wa miradi hii. Ni kweli ukisikia fedha zilizotengwa karibu katika kila mradi ni hela nyingi sana. Mradi wa Isaka zaidi ya shilingi bilioni ishirini, mradi wa Bulyanhulu bilioni karibia kumi na saba. Miradi yoote hii ukiangalia fedha zinaengwa na utekelezaji wake mara nyingi unakuwa hauwiani. Mimi nishauri sana, Mheshimiwa Waziri umesikia jitahidi sana kuwa na mfumo mzuri wa usimamizi wa utekelezaj wa hii miradi, fedha ni nyingi lakini utekelezaji unakuwa haukidhi viwango.

Mheshimiwa Spika, suala la pili nilitaka kumshauri Mheshimiwa Waziri na hasa Serikali kwa ujumla wake kwamba tukubali hili wazo la kuanzisha mfuko maalum wa maji utakaokuwa na wakala wake unaojitegemea. Tumeona mifumo ya namna hii ambavyo inafanya kazi vizuri kwenye maeneo mengine. Tumeona kwa mfano REA wanafanyakazi vizuri kwa sababu kwa kiasi kikubwa fedha zinatengwa na zinakwenda kwenye eneo maalum ambalo limelengwa kwa ajili hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia tunaona kwenye barabara TANROADS wanavyofanya kazi vizuri kwa sababu wana Mfuko wa Barabara. Pamoja na changamoto zinazokuwepo za kibajeti kiujumla, lakini angalau miradi inakwenda vizuri. Kwa hiyo, mimi nilikuwa naomba sana, Waheshimiwa wengi wamesema na mimi nirudie ombi hilo kwamba ni vizuri sasa Serikali likakubali hili wazo la kuanzisha wakala maalum na mfuko maalum wa maji na hasa utakaokuwa unalenga vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vyanzo vimepekezwa, kwenye mafuta na maeneo mengine lakini kubwa ni kuwa na wakala maalum unajitegmea ili kutoka kwenye haya makucha ya kumtegemea Dkt. Mpango kila wakati ambaye mwisho wa siku anawapa asilimia 22.

Mheshimiwa Spika, wakiwa na mfuko unaojitegemea hawatapeleka kwa Dkt. Mpango au wakipeleka wanajua kabisa mfuko wa maji zimekusanywa kiasi fulani lazima zitapelekwa bila kusumbuliwa kama inavyotokea sasa hivi.

Mheshimiwa Spika, jambo la tatu la ujumla nilitaka kushauri pia juhudi ziongezwe katika schemes za umwagilaiji, ziwe nyingi zaidi. Tumeona mvua zilivyo nyingi lakini mwisho wa mwaka utajikuta tena kuna maeneo mengine tunalalamika kuna tatizo njaa kwa sababu maji yanatiririka mikoa ya Dodoma, Mikoa ya Shinyanga, hii yenye ukame, yanatiririka lakini hakuna namna ya kuyatunza kwa kilimo cha umwagilaji.

Mheshimiwa Spika, niombe sana Mikoa hii ya Shinyanga na Dodoma iwe na schemes maalum kwa ajili ya kufanya kilimo cha umwagilaji ili tuweze kuondokana na tatizo hili. Kwetu pale Msalala tulikuwa tumeshaanzisha tangu mwaka 2014 ulikuwepo mradi wa scheme za umwagiliaji, Mradi wa Kahanga ulikuwepo sasa hivi kwa Halmashauri ya mji pamoja na mradi wa Chela. Miradi hii ilitengewa fedha hazikutoka zote na haukutekelezwa. Nikuombe Mheshimiwa Waziri utakapopata nafasi ukija Kahama tukumbushane ili uweze kutembelea mradi wa umwagilaji scheme ya Chela. Utasikitika kwa sababu umeachwa asilimia 40 ya utekelezaji wake, fedha zimepotea, umwagiliaji haufanyiki na hakuna chochote kilichofanyika na ilikuwa ahadi ya Waziri Mkuu Mheshimiwa Mizengo Pinda alikuja Chela wakati huo na akasema mradi huo ungefanyika. Kwa hiyo, haya matatu nilitaka niombe sana Wizara izingatie.

Mheshimiwa Spika, nirudi kwemye miradi ya Msalala, kama ambavyo nimesema miradi ipo mingi, wasiwasi wangu ni utekelezaji wake kwa ukamilifu. Tuna mradi huu isaka kama ambavyo nimegusia, una awamu mbili, awamu ya kwanza inakwenda vizuri, lakini kuna hofu awamu ambayo inahusu usambazaji kwenye vijiji vilivyo kandokando ya bomba kuu, ukachelewa kutekelezwa kwa sababu ya huu mwenendo ambao tunao katika upatikanaji wa fedha na utekelezaji wa mradi wenyewe.

Mheshimiwa Spika, nilitaka kuomba sana Mheshimiwa Waziri na Wizara yako na Katibu Mkuu yupo hapa na rafiki yangu Mhandisi Karobero - Naibu Katibu Mkuu, wote kwa ujumla sasa muanze utekelezaji wa awamu ya pili kama tulivyokuwa tumekubaliana. Awamu ya kwanza ikifika asilimia 40; awamu ya pili iweze kuanza ili wananchi wa Kata za Mwalugulu, Isakajana waweze kupata maji kwa sababu kwa sasa hivi maji yanapita kwenye kata hizo lakini watapata wananchi wa Isaka Mjini na wananchi wa Kagonga Mjini, lakini Kata ya Isagehe, Mwalugulu, Isakajana hazitapata maji na ziko ndani ya kilometa nane/sita; chini ya kilometa 12. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mradi mwingine ni huu niliyougusia wa Bulyanhulu kutoka Manghu kwenda Bulyanhulu. Mradi huu nao tulikubaliana utekelezwe kwa ushirikiano baina ya Serikali na mwekezaji wa ACACIA. Nikuombe Mheshimiwa Waziri, ACACIA mimi nawafahamu, nimefanya nao kazi miaka yote, commitment yao ilikuwa kutoa dola milioni mbili, nadhani mnafahamu; mpaka hivi tunavyozungumza tumesaini mkataba na mkandarasi toka mwezi Desemba, mpaka sasa hivi hata advance haijatoka lakini ACACIA alishatenga dola milioni mbili, zaidi ya bilioni tano ambazo ziko lakini hazijatoka.

Kwa hiyo, nilitaka kuomba tu kwamba muwe macho na huyu mwekezaji, hakikisheni hizi fedha kweli zimetoka, ziko kwenye mfuko ambao Serikali inaweza ikazi-access na ikatumia kulipa wakandarasi, vinginevyo tutapigwa changa la macho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tulishaahidiwa mambo mengi kule, mimi nawajua na nimekuwa nikiwalalamikia hapa kila wakati. Kwa hiyo, tutauita mradi wa amoja kati ya ACACIA na Serikali lakini mwisho wa siku utakuwa ni mradi wa Serikali peke yake. Kwa hiyo, nataka kuhimiza hilo, Serikali mlione na mzingatie. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia awamu ya pili ya mradi huu, kama nilivyosema ule wa Isaka nao una sura hii hii, kwamba unapita kwenye vijiji, lakini tulikubaliana phase ya kwanza angalau bomba kuu liweze kufika Ilogi, vijiji vya pembezoni havipati maji. Itakuwa ni tatizo kubwa pale mradi utakapokuwa umefika, bomba kuu lipo, vijiji viko pembezoni havipati. Utekelezaji wa awamu ya pili unaosambaza maji pembezoni mwa hilo bomb kuu na kusogeza mradi huo hadi Lunguya kama tulivyokuwa tumekubaliana nao uweze kuanza kutekelezwa.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema, nimuombe sana Mheshimiwa Waziri, hatua za utekelezaji awamu ya pili ya miradi wa Isaka na Bulyanhulu ianze sasa hivi kwa sababu commitment tuliyoiweka kwa wananchi ni kwamba ifikapo mwaka 2020 wananchi wa Kata za Bulyanhulu, Bugarama, Lunguya, Busangi, Kashishi, Isaka, Mwalugulu na Isakajana wawe wamepata maji. Leo ni mwaka 2018 bado mwaka mmoja na nusu au miwili muda huu umefika wa kuja kuulizwa tumefikia wapi. Sipendi ifike wakati huo tuanze kuulizwa maswali ambayo tungeweza kuyaepuka kwa sasa hivi. (Makofi)

Nashukuru sana, kama nilivyosema naunga mkono bajeti, niombe tu Waziri asimamie awamu hizi zitekelezwe kwa ukamilifu. Nashukuru sana.