Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Spika, ahsante na mimi naomba nichangie katika Wizara hii ya Maji na Umwagiliaji katika maeneo mawili.
Mheshimiwa Spika, maji ni uhai wa kila kiumbe chenye uhai katika uso wa dunia, lakini nchi yetu imekuwa ni kinyume na matarajio, maji yamegeuka kuwa mtego wa umaskini kwa uchumi wa Mtanzania wa kawaida. Maskini analipia maji bill kubwa kuliko mtu mwenye uwezo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, moja kwa moja kutokana na muda naomba niende kwenye mpango wa maji vijijini. Tuna vijiji vingi katika nchi hii ambavyo havina maji tofauti na sisi tunaokaa katika maeneo ya mjini. Naomba nitolee mifano miwili tu katika Mkoa wangu wa Manyara.
Mheshimiwa Spika, ukiangalia pato la kawaida la Mtanzania kwa mwaka ni shilingi 2,131,299; hii ni kutokana na takwimu ya Juni, 2017 ili uone ni jinsi gani tuna hali mbaya katika sekta hii ya maji, tuna vijiji katika Wilaya ya Hanang, tuna vijiji vinaitwa Gehandu na Laganga, vijiji hivi umbali wa kupata maji ni kuanzia kilometa mbili mpaka kilometa nne watu wanatafuta maji. Hata hivyo pale unapopata hayo maji pipa la lita 200 ni shilingi 7,000. Sasa ndio ujiulize ukiwa na familia ya watu sita utakuwa unagharimia katika uchumi wako shilingi ngapi? Halikadhalika vijiji vya Endakiso na Nkaiti maji yanauzwa kwa gharama hizo hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pato la huyu mkulima na mwananchi wa kawaida badala ya kufanya masuala ya kiuchumi pato lake linaishia katika manunuzi ya maji. Hapa tunasifiana, lakini hata Biblia inasema kusifu kunawapasa wanyoofu wa moyo, hivi mnasifu nini katika hili? Wanaokufa ni akina nani? Tuna watoto tuna ndugu zetu, hata kama sisi tunaishi mjini, tumewaacha babu zetu na mama zetu huko nyuma. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, familia moja inahitaji angalao pipa moja kwa kubana matumizi, lakini mwananchi huyu anahitaji takribani shilingi milioni 2.5 kwa mwaka ili watoto wake wale, waoge, wapige mswaki na matumizi mengine, lakini pia familia ya watu sita wastani wa hicho kipato ni asilimia 16 ya kipato cha kila mwanafamilia. Kwa muktadha huu hata mtoto aliyezaliwa leo wa siku moja anahusika katika manunuzi ya maji. Hebu tujiulize kwa Tanzania nzima na vijiji vyote hali hii ya adha ya maji uchumi wa Watanzania tumeukaba kiasi gani na tumewarudisha kiasi gani? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunaomba Waziri utakapokuja utuambie umeongea vipi na watu hao wa Wizara ya Fedha? Tunajua tatizo haliko kwenu, tatizo liko Hazina. Kwenye Kamati za kisekta watu wa Hazina wanakuwepo, mara waje kwanza na ukomo wa bajeti, mmeweka ukomo wa bajeti kile kidogo mlichokiweka hamkitoi. Kwa nini mnatuchosha kukaa kwenye Kamati tunachambua nini? Unawezaje kuwa na akili nzuri hujaoga, hujala, wewe utapata wapi hiyo afya? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ahsante.