Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali Wizara ya Maji na Umwagiliaji 2018/2019

Hon. Omary Ahmad Badwel

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bahi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali Wizara ya Maji na Umwagiliaji 2018/2019

MHE. OMARY A. BADWEL: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia kwenye bajeti hii ya Wizara ya Maji.

Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nichukue nafasi hii kuwashukuru sana mheshimia Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri ambao kwa kweli, wametoa ushirikiano mzuri sana kwangu katika kipindi chote ambacho wamekuwa Mawaziri. Wamefika kwangu Bahi kwa nyakati tofauti na Mheshimiwa Waziri hivi ameniahidi Jumamosi ijayo tena anakuja Bahi. Kwa hiyo, kwa kweli nina kila sababu ya kuwashukuru na matokeo ya ujio wao pia yameonekana kwa sababu pale Mji wa Bahi tumekuwa na shida ya maji kwa muda mrefu sana, lakini Mheshimiwa Waziri aliruhusu pesa shilingi milioni 400 katika bajeti hii ambayo tunakwendanayo na kwa kweli, watu wa Bahi wameanza kupata maji angalau kwa kiwango kidogo, lakini maji yameanza kutoka na kwa mara ya kwanza watu wa Bahi wameyaona maji ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia katika bajeti hii nimeona wametuongezea shilingi milioni 400 kwa ajili ya kuendeleza Mradi wa Maji wa Bahi, ingawaje fedha hizo hazitoshi, na Mheshimiwa Waziri kwa kuwa unakuja basi utaona namna ambavyo tutakuomba kule Bahi. Ninaamini utashirikiana na sisi kama ambavyo umeshirikiana kukamilisha kabisa ule Mradi wa Maji wa Bahi, mji ambao unakua kwa kasi ili watu waweze kuyatumia maji kwa shughuli mbalimbali za maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini Wizara ilitupa fedha ya kuchimba visima vitano katika mwaka huu wa fedha ambao tunakwendanao na tayari tumechimba visima vitatu katika vijiji vya Ilindi, Bahi Makulu na Mpamata. Sasa tunakwenda kuchimba katika Kijiji cha Ikungulu na Lamaiti. Katika bajeti ambayo tunakuja sasa kwa kuwa mlitupa fedha za kuchimba visima katika vijiji vitano bila pump, lakini naona mmetuwekea sasa katika hivi vijiji vitano, safari hii mmetuwekea fedha shilingi milioni 100 kwa kijiji kimoja cha Ilindi. Sasa nilikuwa nataka nijue Mheshimiwa Waziri umetupa mwaka jana fedha za kuchimba visima vitano, tumeshachimba vitatu na tunakwenda kuchimba viwili vingine na vitakuwa vitano ambavyo havina pump, lakini kwenye bajeti hii unatoa tu kisima kimoja kama tukafunge pump kwa maana ya kisima cha Kijiji cha Ilindi. Nilikuwa nakuomba Mheshimiwa Waziri kama umesahau vijiji viko vitano, basi niongezee hivyo vijiji vinne pia navyo tupate fedha kwa ajili ya kufunga pump ili wananchi wameona visima vimechimbwa wawee kupata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia, viko vijiji kadhaa ambavyo navyo vina shida kubwa katika Wilaya ya Bahi na hususan kwa sababu Wilaya ya Bahi ile ni Wilaya ya ukame, ningeomba pia katika vijiji baadaye utakaapopanga bajeti zako vijiji vya Chikola, Chonde, Ikumbulu, Chifutuka, Chaliigongo, Chikopelo, Chalisanga na Mkola navyo kwa kweli uweze kuvipata fedha kwa ajili ya uchimbaji wa visima.

Mheshimiwa Spika, lakini kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri cha hotuba yake katika ukurasa wa 273 ziko taarifa ambazo mimi nataka nimwambie taarifa zile si sahihi. Nimeona kwamba katika mradi ule wa visima vilivyochimbwa na Wakala wa Uchimbaji Visima na Ujenzi wa Mabwawa (DDCA) imeonesha pale kwenye ukurasa wa 273 kwamba kwenye Wilaya yangu ya Bahi viko vijiji vya Mzogole ambapo kuna kisima namba 278 kwa kupitia Mkandarasi Godwin Mwasombwa na kijiji cha Zejele namba 279 kupitia Mkandarasi Emmanuel Nyaumba kwamba vijiji hivyo vimkechimbiwa visima na kwa bahati mbaya visima vimekutwa havina maji.

Mheshimiwa Spika, jambo hili sio kweli Mheshimiwa Waziri. Kama nkuna watu walikupa taarifa hizi wamekudanganya kwa sababu mimi binafsi nimeshituka kuona hapa kwenye kitabu chako kwamba mmetuchimbia hivyo visima katika Vijiji vya Mzogole na Zejele lakini hakuna maji. Nikafanya utafiti, nimewasiliana na uongozi wa kijiji, nimewasiliana na Mheshimiwa Diwani, Mhandisi wa Maji wa Wilaya na Mkurugenzi, wote wamenijibu kuwa jambo hili halikufanyika. Kwa hiyo, nilikuwa naomba jambo hili wakati unajibu hoja mbalimbali za Wabunge na mimi unijibu kumetokea kitu gani zimeletwa taarifa hapa ambazo si sahihi. Kama ahawajachimba na fedha hizi zipo waende wakachimbe visima hivi na nina uhakika maeneo haya watapata maji.

Mheshimiwa Spika, lakini wakati tunaendelea na miradi hii ya maji ni vizuri pia tukaiangalia kwa jicho lingine miradi ya umwagiliaji. Kwa mfano sisi watu wa Dodoma kila mtu anajua namna ya ukame wa Dodoma, hata watu mwaka huu wameshangaa kuona mvua kubwa namna hii, ni baraka tu za Mwenyezi Mungu. Lakini kwa kweli tuna shida kubwa ya ukame na mkombozi pekee kwenye Wilaya hizi za Dodoma, hususan Wilaya yangu ya Bahi ni kuwa na kilimo cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Spika, tunazo skimu kumi pale katika Wilaya yetu ya Bahi, lakini skimu hizi miongoni mwao zimechakaa, ni za muda mrefu, hazikutengenezwa kwa kiwango kizuri na skimu hizi zinazhitaji matengenezo makubwa. Katika bajeti iliyopita nilipata nafasi hapa ya kuchangia, nikaomba Wizara ije itume wataalam wake kuja kufanya tathmini ya kina kujua hii miradi ya umwagiliaji Bahi hasa mahitaji yake ni nini maana imepitwa na wakati. Miradi hiyo ni Bahi Sokoni, Nguvumali, Matajira, Mtazamo, Mtitaa, Uhelela, Chikopelo, Kongogo, Lubala na Uhelela. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilikuwa naomba Mheshimiwa Waziri safari ile hukutuma hiyo timu, lakini safari hii naomba utume timu Bahi ije ione miradi hii inahitaji mahitaji gani ili iweze kuendelezwa na sisi wananchi ambao wilaya yetu ni ya ukame tuweze kuitumia kikamilifu kupata chakula na tuepukane na ombaomba ya chakula kila mwaka.

Mheshimiwa Spika, uko Mradi wa Kongogo ambao umeniahidi Jumamosi ijayo unakuja kuutembelea. Huu ni mradi wa muda mrefu wa bwawa na sehemu nyingine inataka kwenda kumwagilia. Ni mradi ambao umekuwa ukilalamikiwa na wananchi muda mrefu, umetumia fedha nyingi na umeniahidi kwamba utafika siku ya Jumamosi. Mimi mwenzio nilipokwenda mara ya mwisho nilipokelewa na mabango juu ya namna ambavyo watu hawakuridhika na utengenezaji wa Mradi huu wa Kongogo. Sasa siwatumi hapa waje na mabango siku ya Jumamosi utakapokuja, lakini watakupa ujumbe wa namna ambayo wamesikitishwa na kuchelewa kukamilika na kutokuridhika kwa kiwango cha mradi huu kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, lakini gharama za miradi ya maji zimeelezwa na Waheshimiwa Wabunge hapa na mimi mwaka jana niliwahi kusema jambo hili kwa kweli gharama za miradi ya maji ni gharama kubwa mno. Wako baadhi ya wataalam wetu si waaminifu, wamekuwa wakishirikiana na wakandarasi kuhakikisha kuongeza kiasi cha fedha cha miradi hii na imekuwa ni vigumu sana. Mimi naamini kama miradi hii ingetafutiwa njia bora ya utekelezaji kwa miaka yote hii leo tusingekuwa na kilio hiki tunacholia hapa. Kilio hiki tunacholia kimesababishwa na sehemu ya wataalam wetu na wakandarasi ambao sio waaminifu, lakini pia na usimamizi hafifu na Wizara kutokujituma kutaka kubadilika na wakati kwamba, hivi kwa nini kila siku tunalia kilio hicho hicho.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ni vizuri na mimi nakubaliana, na umezungumza vizuri asubuhi kwamba miradi ya shilingi milioni 600, shilingi milioni 700 ni miradi ambayo imeumiza wananchi kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, umekuwa ukiunda tume hizi na zimekuwa zikifanya kazi nzuri sana, hebu tubadilike na kwenda kwenye tume ambayo itachunguza utekelezaji wa miradi ya maji. Uunde Tume hapa ya Kibunge iende ikaangalie namna ya kutengeneza miradi inavyotengenezwa, ifanye tathmini ya muda, gharama, kwa nini miradi ya umeme tunaambiwa ukienda kilometa kadhaa ni shilingi kadhaa, lakini miradi ya maji huwezi kukuta hiyo habari, kila mtu anajipangia vile anavyoona yeye inafaa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, lazima jambo hili kwa kweli liangaliwe kwa kina, kiki fedha zitumike chache, lakini zenye tija, vifaa bora na wananchi waweze kupata huduma hii ya maji kama ambavyo inasisitizwa na Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nakuomba sana hebu uunda tume itakayochunguza miradi ya maji tuisaidie Serikali. Tume ile ya Wabunge itakuja na mapendekezo na hapa tunapofikiria kuunda huu Wakala wa Maji Vijijini uwe na kitu cha kuanzia kwamba inakwenda kusimamia kitu gani ambacho kimechunguzwa kikamilifu na kimetolewa maelekezo na kinaweza kutoa tija na ufanisi, ili wananchi wetu hawa wasiendelee kulia kilio cha kukosa maji.

Mheshimiwa Spika, tunayo Tume ya Umwagiliaji, kwa kweli imekuwa na watumishi wachache na yule bosi wao anakaimu leo mwaka wa tatu, sijui ni mwaka wa nne, inakuwaje mtu anaweza kukaimu miaka yote hiyo na mtu anafanya kazi vizuri, anachapa kazi vizuri, tunashirikiana naYe vizuri? Mpeni nafasi ya kuwa Mkurugenzi kamili, ili aweze kujiamini na kufanya kazi ile kwa ukamilifu.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono tozo ya shilingi 50 iongezwe kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge wenzangu wameshauri, ili iweze kuongeza kiwango cha fedha ambacho kitatusaidia sana katika utekelezaji wa miradi ya maji.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. asante.