Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Hamidu Hassan Bobali

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mchinga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwanza niendelee kumwombea Mbunge Mwenzangu Ndugu yangu Mheshimiwa Kasuku Samsoni Bilago safari yake anayokwenda Mwenyezi Mungu ampokee na amuweke mahali pema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri anisikilize. Mwaka jana nilimpongeza humu ndani ya Bunge kwa kazi aliyoifanya pale Mchinga ya kuamua kumnyang’anya yule mtu ambaye alituibia ardhi yetu zaidi ya hekta 4,000 na kuzirudisha Serikalini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri nataka nimwambie kwamba lile jambo kuna Watendaji wa Serikali waliopo ndani ya Mkoa wetu wa Lindi halikuwafurahisha. Huwezi kuamini kwamba mwaka jana mwezi Machi, Mheshimiwa Rais alifika Mchinga akaoneshwa vile Vituo vya Afya viwili ambavyo alijenga yule jamaa pale Mchinga na Ruvu, akatoa agizo kwamba ndani ya mwezi mmoja viwe vimefunguliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka nimwambie Mheshimiwa Waziri mpaka sasa hivi tumepata mfadhili amekubali atatuletea vifaa tiba vyote. Hivi sasa ninavyosema viko baharini vinaelea vitafika mwezi wa Tisa, lakini lile eneo tumezuiwa tusilitumie, tumezuiwa zile Zahanati tusizitumie, tumezuiwa kila kitu pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kuna vitu vinaletwa na mfadhili lakini Serikali ya Mkoa na Serikali ya Wilaya tena iliagizwa na Mheshimiwa Rais kwamba walishughulikie jambo lile ili tupate funguo, mpaka sasa hivi yule jamaa funguo amezi-withhold, hataki kuzitoa, Mkoa ule una Mkuu wa Mkoa, una Mkuu wa Wilaya na una watendaji wote wa Serikali lakini wanashindwa namna ya kufungua zile Zahanati

Mheshmiwa Mwenyekiti, sasa Mheshimiwa Waziri nataka nimwambie jambo lile halikuwafurahisha. Tulikwenda kwenye kikao cha RCC, Kiongozi ninayemheshimu sana wa mkoa anasema kwamba kuna utaratibu ambao haukufuatwa vizuri, kwa hiyo jamaa amegoma kutoa funguo. Yeye kama Mkuu wa Mkoa, kama kiongozi wa mkoa anachukua hatua gani kulazimisha ama kuhakikisha kwamba zile funguo tunazipata na yule jamaa lile eno letu anatuachia. Maana inakuwa ni kana kwamba lile eneo bado analo yeye. Kama tunashindwa kuvitumia vitu ambavyo yeye alivijenga na tukamnyang’anya, sasa inaonekana kwamba sisi wenyewe kwenye Mkoa ndio tuna matatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, kama alitoa amri ambayo haikuwa na document, hakufanya documentation, naomba aiandikie Serikali ya Mkoa yale maagizo yake, kwa sababu inaonekana kwamba wao wanaona just business as usual. Sasa namwomba sana Mheshimiwa Waziri alichukulie jambo hilo kwa umuhimu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni kuhusu tatizo la mipaka kati ya vijiji, kati ya halmashauri na halmashauri, kati ya kata na kata. Mheshimiwa Waziri huwezi kuamini kwamba Wilaya ya Lindi ambayo mimi ndiko ninakotokea; sisi tuna migogoro mizito kwanza ndani ya Wilaya kati ya Halmashauri ya Manispaa ya Lindi na Manispaa ya Lindi DC. Pia tuna mgogoro wa kati ya Lindi DC na Wilaya ya Ruangwa. Sasa naomba sana Mheshimiwa Waziri jambo hili la migogoro ya mipaka walichukue, walifanyie kazi, waje mpime.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachonishangaza mimi Ruangwa ilikuwa sehemu ya Wilaya ya Lindi, wao wametoka mbavuni kwetu wakachukua eneo lao wakaondoka. Sasa leo na wao wanakuja wanasogea wanachukua baadhi ya maeneo yetu tena ya Lindi DC wanasema ya kwao. Kuna mgogoro mzito, hata pale ambapo mimi napasema kila siku kuna mjusi alichukuliwa leo watu wa Ruangwa wamesogea kabisa na tusipokuwa makini mwakani tutakuja kuambiwa yule mjusi amechukuliwa Ruangwa. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri naomba sana hii migogoro aje atutatulie, aje aseme kwamba mpaka wa Wilaya umepita humu na GN inasoma hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna migogoro ya kwenye kata huko, hiyo ndiyo mingi, lakini kwanza angalau tuanze na hii ya Wilaya. Huwezi kuamini kwamba watu wa Manispaa maeneo ambayo tuliyowapa juzi tu ili wakidhi vigezo kuwa Manispaa leo wanakwenda wanatunyang’anya. Wao wameanzisha mkakati wao wa kuhakikisha watu wanalima korosho wanauza maeneo yao, wanawapa wenye fedha walime mashamba makubwa ya mikorosho. Sasa wamegawa maeneo yamekwisha wanakuja kuchukua na maeneo yetu ya Lindi Vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri atume watu wake, waje Lindi, waje watutatulie migogoro iliyopo kati ya Lindi Manispaa, Lindi DC, na watu wa Wilaya ya Ruangwa kwa sehemu ndogo. Naamini hata huu mgogoro wa Ruangwa hata Waziri Mkuu sijiu kama anaufahamu labda kwa sababu yupo bize na mambo mengine ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri aje atatulie hili, kwa sababu tatizo la migogoro ya ardhi Lindi sasa hivi, viongozi tunaowaamini kwamba wanaweza kuwa ma-referee wao ndio part and parcel ya hii migogoro; kwa sababu nao wamejichukilia hayo maeneo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hao watu wa Manispaa watu ambao wamegawa maeneo, hao ambao tunawategemea kwamba wangesimama katikati ndio waliochukua hayo maeneo. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri hili ni tatizo. Sasa ukienda ukawaambia hili eneo la Lindi DC na hili la Manispaa hawakuelewi kwa sababu wao ni wanufaika wa hayo mambo. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri aliangalie kwa umakini sana suala la migogoro ya ardhi kwa sababu linaleta shida.

Mheshimiwa Mweyekiti, jambo la tatu, ni suala la upatikanaji wa hati ya umiliki wa ardhi. Jana nilimsikiliza vizuri sana Mheshimiwa Waziri, akasema kwamba wameongeza upatikanaji wa hati ndani ya miezi sita, sijui miezi mingapi, lakini mchakato huu bado ni mkubwa sana, bado mchakato ni mrefu. Mimi naishi Dar es Salaam, tupo pale kwenye mtaa wetu kule Chamazi, tumefanya application tangu mwaka jana mpaka leo hatujapata hati, tunahangaika na suala la hati na tuko watu wengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri akija akisema kwamba tumeongeza na mimi naamini si suala la kwangu; na nilimwona wakati anazunguka Mikoa ya Kanda ya Ziwa, aliona namna ya watu wanavyomjalia, alikuwa anafanya kazi mpaka saa sita usiku, ni ushahidi kwamba kuna tatizo kubwa kwenye mfumo wa Wizara yake, kuna tatizo kubwa kwa walio chini ya Wizara yake, kwamba wao ndio wanategemewa waipunguze hii migogoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ukiona kwamba Mheshimiwa Waziri anakwenda anapokelewa na zaidi ya watu 1000 au 2000 which means walio chini yake hawawajibiki vizuri. Kwa hiyo hili liwe changamoto kwa Mheshimiwa Waziri, lisiwe suala la Kanda ya Ziwa na maeneo
mengine tuu, hata akija Lindi na Mtwara tatizo litakuwa ni hilo hilo, kwamba kunakuwa na ucheleweshaji mkubwa, mtu anaomba hati, basi namna ya kuja kuipata zaidi ya miaka miwili au miaka mitatu hili nalo ni tatizo sana. Kwa hiyo namwomba Mheshimiwa Waziri suala la upatikanaji wa hati za ardhi liwe ni suala ambalo ni haki ya Mtanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, ziko hati zinaitwa Hati za Kimila. Sisi Halmashauri yetu ya Wilaya ya Lindi, kwa kutumia MKURABITA na sisi wenyewe tumeomba baadhi ya maeneo tupatiwe Hati za Kimila. Hata hivyo, hapa tunapomweleza Mheshimiwa Waziri hakuna hata kijiji kimoja ambacho kimeanza kutoa Hati za Kimila.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mahitaji makubwa sana kwa Mkoa wa Lindi na Mtwara sasa hivi ardhi ikawa inamilikishwa na kwa sababu mbili; kwanza kwa potentiality ya maeneo yale, kugundulika kwa gesi kumeongeza au kume-attract watu wengi kuja kumiliki ardhi kule. Sasa hawa watu leo wasipokuwa na Hati zao, ni rahisi kuja kunyang’anywa, ni rahisi kuja kurubuniwa na watu wenye vijisenti wakachukua maeneo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina ushahidi mkubwa, katika eneo ambalo linakwenda kujengwa mradi wa LNG, pale Likong’o mpaka ukija pale Geza eneo ambalo lipo kwenye jimbo langu; maeneo yale tayari wale watu wamiliki wa asili wote walishaondolewa. Wale wamiliki wa asili wameondolewa na waliopo sasa hivi ukienda ukiangalia majina yao hakuna hata mtu mmoja ambaye ni mwenyeji wa Mchinga, hakuna mtu ambaye ni mwenyeji wa maeneo yale. Kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri suala la upatikanaji wa Hati za Kimila kwa Lindi na Mtwara liwe priority kwa sababu ya potentiality ya maeneo yale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.