Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ismani
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa fursa hii uliyonipa mara ya pili baada ya ile kusoma. Nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote kwa kutupa moyo mimi na Naibu wangu na Watendaji wetu. Nataka kuwahakikishieni kwamba hatutawaangusha. Leo mmetuchaji zaidi, tutaongeza speed. Nataka mhakikishe kwamba mwakani mkija kuzungumza wote ambao mmeandika na kusema, mje mtoe ushuhuda kwamba tumefika kwenu na tumezungumza haya mliyotutuma tukiwa kwenye Majimbo yenu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na hoja yako, ulipokuwa unachangia hoja ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwenye maswali yako wiki mbili zilizopita, Mheshimiwa Waziri Mkuu aliahidi kwamba ile issue ya Chama cha Wapangaji na National Housing wakutane, Mheshimiwa Waziri Mkuu ni Kiongozi wetu, nawe ni Mwenyekiti wetu. Nataka kukuhakikishia kwamba National Housing watakutana na viongozi wa Chama cha Wapangaji. Jana nimekutana na Mwenyekiti yuko hapo nje. Naagiza wakutane kabla ya tarehe 15 Mwezi wa Sita, halafu waniambie wamekubaliana nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, yale maagizo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu yatatekelezwa, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi yuko juu hapa ananisikia na Kaimu Mkurugenzi wa National Housing yuko hapa. Naagiza wakutane kabla ya tarehe 15 Mwezi Juni baada ya hapo, wanione mimi kama Waziri nijue nini naweza kuamua. Kama liko ndani ya uwezo wangu au la kupeleka kwenye Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa pendekezo hilo na namshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa maagizo na namhakikishia kwamba nitatekeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wamezungumza wengi, nianze na rafiki yangu hapa Mheshimiwa Bobali. Amri yangu niliyoitoa ni kwa mujibu wa Sheria ya Mchinga. Lile eneo nataka wasikie wote, ni eneo la Serikali. Zile ekari zote zilizochukuliwa na kampuni ile iliyochukua kuzunguka Bahari ya Hindi, lote ni eneo la Serikali. Walichukua kinyume cha sheria na nilikwenda na viongozi wote, walitoa hati kinyume cha sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kuna mazungumzo na migongano inafanyika huko, haiwezekani. Nimeshatoa amri na amri siyo yangu ni ya kisheria. Kwa hiyo wajue tu hili eneo ni la Serikali. Halmashauri ya Wilaya ya Lindi wajue hili ni eneo la Serikali na lazima walipange kwa mujibu wa sheria. Nilitangaza siku ile walipandishe hadhi kwa sababu walianza kutoa hati kabla, eneo lenyewe likiwa kwenye hadhi ya vijiji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hili hatubabaishani ndani ya Serikali. Mimi ndio nimepewa jukumu hili na Mheshimiwa Rais, namsaidia kufanya jambo hili. Zile Zahanati zitafunguliwa, vinginevyo anayetaka azibomoe akazijenge huko alikotaka. Zile Zahanati zimejengwa kwenye ardhi yenu.
Kwanza nashangaa, mnasubiri nyie kufunguliwa na nani? Nani awafungulie? Ziko kwenu, nani anawafungulia? Kufuli gani hizo zimewekwa? Mwambieni azichimbe azitoe. Nani alimpa kibali cha kujenga? Hakuna makubaliano? Kwa hiyo, nasema, hilo la Zahanati siyo langu, lakini ardhi ile haitoki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimewasikiliza vizuri Mheshimiwa Bobali na issue zenu za mipaka, Mheshimiwa Kuchauka na Mheshimiwa Maftaha, ninyi mnatoka Mkoa wa Lindi na Mtwara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nimepanga, sasa mmenipa nguvu. Nitatembelea Mkoa wa Mtwara na Lindi. Nitarudi tena pale Mjini Mtwara ili nione yule tapeli kama anaendelea kunyanyasa, maana sehemu nyingi nimemkaba. Huyo huyo ndiye amehusika na huko Lindi, huyo huyo ndio Mtwara. Anatafuta watu wa Dar es Salaam wanakwenda kuchukua ardhi Mtwara kana kwamba Mtwara hawapo. Nitakuja Mtwara, Lindi na Newala kwa rafiki yangu Rashid. Kule nako ule mpaka kati ya Masasi na Newala tutakuja kuzungumza huko kwenye site, tutaelewana. Ni kweli baadhi ya Watendaji wa Ardhi kwa siku za nyuma walikuwa sio waaminifu. Tunapowatuma kwenda kurekebisha mipaka, wanarekebisha mipaka kutokana na eneo; wale wajanja wanaowapa fungu, basi mpaka unahamia huko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumejifunza juzi kwenye mpaka wa Kilindi na Kiteto; zaidi ya kilomita 15,000 zilikuwa zimehama. GN inaeleza watu waende Kaskazini Mashariki wenyewe wanakwenda Magharibi bila sababu. Sasa kutokana na nidhamu iliyowekwa n a Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, hakuna mtumishi anaweza kula hela tena. Kwa hiyo, sasa hivi mjue kila palipoandikwa GN, tutarekebisha kwa mujibu wa maandishi ya GN unless wananchi wakubaliane upya. Maana inawezekana GN na yenyewe imepitwa na wakati, lakini mkikubaliana, sisi tunakuja kuiandika tena. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimhakikishie kwamba sasa hivi utumishi wa Umma umebadilika, watu wana nidhamu, tutakuja kurekebisha hiyo mipaka ya Masasi na Newala na maeneo yote ambayo yana migogoro mipaka tutapitia na mingine tumeshaiandika, kama ile ya Makambako, Njombe na Mufindi, rafiki yangu Mheshimiwa Kigola amesema na mingine tuliyoandika tutakuja kuishughulikia ili angalau watu wakae vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI naye ametoa maelekezo kwa Wakuu wa Mikoa wahakikishe kwamba mipaka ya vijiji na vijiji migogoro yao wanaimaliza kwa sababu iko ndani ya uwezo wao. Alishaandika siku nyingi na nadhani hili wanalitekeleza. Maana haiwezi kuwa wanasubiri Mawaziri waende huko kushughulikia mipaka ya vijiji na vijiji wakati GN wanazo na mipaka hii ilibuniwa na Wilaya zao. Kwa hiyo, nawaomba Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa wasimamie ukamilishaji wa utatuzi wa migogoro ya vijiji na vijiji kwa sababu iko ndani ya uwezo wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimeyasikia ya Mheshimiwa Bobali, Mheshimiwa Kuchauka na Mheshimiwa Maftaha. Lile la Mheshimiwa Maftaha la mjini kuhusu mgogoro wa fidia, kwa sababu wananchi waliingia mkataba na UTT; na UTT ni chombo cha biashara, kiko chini ya Wizara ya Fedha, hata mimi niliwashangaa. Kwa sababu waliosema watalipa mwaka 2017 ni wao, nami nilikuja Mtwara na nyie tulikutana na wewe ulikuwepo. Baadaye wamesema hailipi, wameenda kwa mwenye Wizara yake, Wizara ya Fedha wakamwambia, Mzee huu mradi haulipi, Bodi ya UTT wamekataa kuchukua ile ardhi kwa sababu ule mradi wakipima viwanja watauza ghali na wananchi wa Mtwara hawataweza, hailipiki. Kwa hiyo, wameacha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi Wizara ya Ardhi hapa nilikuwa upande wa wananchi, lakini yamenishinda kwa sababu wenye mradi ambao mlikubaliana nao wamesema hailipi. Ardhi haijachukuliwa, imerudi mikononi, kwa hiyo, tushirikiane tuipange wenyewe, tupime viwanja ili kila mtu apate faida ya ardhi yake. Hatuwezi kuwang’ang’ania wale kwa sababu ilikuwa ni biashara. Nilitaka niseme hivyo, lakini nitakusaidia kuwaeleza zaidi nitakapokuja Mtwara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mtuka amezungumzia habari ya master plan kule Manyoni, yeye ni mtalaam, anajua kabisa kwamba masuala ya master plan yanaanza kwao. Waazimie wao kutengeneza master plan halafu tutashirikiana. Waazimie kwenye Council kwamba wanataka kutengeneza master plan na kupanga mji wao, tunajua wana matatizo ya vifaa, vitakavyokuja tutawaelezeni, wataviazima hivi vifaa kila Halmashauri ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuanzia mwezi wa Saba tutakuwa na vifaa nchi nzima, mtaviazima kila Halmashauri bure. Kabla ya mwezi wa Saba wataalam wa Serikali wa Halmashauri tulionao tutawafundisha sisi Wizara namna ya kutumia hivyo vifaa vya kisasa kupanga. Kwa hiyo, yeye kwa sababu anajua kupanga, yeye ni surveyor, hivi vifaa atavitafuta, tutampa avitumie ili angalau vimsaidie katika kuharakisha. Tunajua jitihada zake, anafanya kazi vizuri pale, lakini tutashirikiana naye kuhakikisha anakwenda kwa kasi nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, alivyosema Mheshimiwa Mwakasaka ni kweli Tabora kuna migogoro mingi, wajanja walishaiharibu pale siku nyingi. Nimekuja mara mbili, amekuja Naibu wangu lakini tutakuja tena. Tunajua siyo tatizo la Tabora, viongozi wengi wameshiriki katika kuharibu mipango miji na kudhulumu watu. Siyo Tabora, sehemu nyingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya viongozi, hata sisi wa kisiasa na Madiwani wakati mwingine huwa tunagombea kwa ajili ya viwanja. Kwa hiyo, kila mji umekwisha, umeshapangwa lakini umeingia kwenye madaraka, lazima upate viwanja. Sasa Watendaji wale walikuwa wanawaajiri ninyi, kwa hiyo, wakiwatisha kidogo wanabadilisha, wanawauzia. Sasa hawatawatisha tena. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais ameondoa hicho kichaka, wamekuja kwangu, maana walikuwa wanawatisha kwamba watawafukuza wasipotekeleza matakwa yao. Mheshimiwa Rais amewahamisha huko, amewaleta kwangu. Kwa hiyo, nataka niwaonye watumishi wote wa Serikali, sasa hakuna kwa kujificha, kitendawili kimeteguliwa, lazima watekeleze majukumu yao kwa mujibu wa sheria na hakuna vitisho. Mtu yeyote sasa atakayekosea huko hatajificha kwamba nililazimishwa na Kamati ya Mipango Miji, ni lwake, atakakufa na lwake na hahamishwi mtu, atafia hapo hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mwakasaka kwamba kwa issue ya Tabora lazima tuje twende tena. Kuna mambo ambayo yamekaa vibaya pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, alichozungumzia Mheshimiwa Mabula ni kweli, katika zoezi la urasimishaji Tanzania watu wanaoongoza wamefanya vizuri, kwa nidhamu na kwa heshima na kujitolea ni Wilaya ya Nyamagana na Ilemela. Amesema kweli kabisa. Kwa hiyo, nami nawapongeza sana. Mheshimiwa Mabula anajua watu wake aliowaleta wiki iliyopita, tumekubaliana tukutane mwezi wa Sita katikati kule Jimboni. Kwa hiyo, namshukuru sana na yeye ametoa ushirikiano sana kule Nyamagana katika zoezi hili. Nyamagana na Ilemela peke yake wameshatoa Hati zaidi ya 25,000. Namshukuru sana na Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza ametoa ushirikiano mkubwa katika zoezi hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nawaomba wananchi na viongozi wote wa Wilaya, wajue zoezi la urasimishaji halina mwenyewe. Watu wamejenga kwenye maeneo yasiyopangwa nchi nzima mijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kila wilaya ijipange ihakikishe inawaokoa wananchi wao katika maeneo yale yasiyopangwa yanayoitwa makazi holela wayapange ili waweze kupata Hati, iwaongezee mzunguko wa fedha, kipato kwa sababu watu wakipangiwa, wakipewa hati, wataingia benki, watazitoa zile hela za mabenki zitakuja mtaani, zitaongeza mzunguko wa fedha katika Halmashauri. Kwa hiyo, zoezi la urasimishaji ni la wote na viongozi wa Wilaya tushirikiane kwa pamoja kuhakikisha kwamba jambo hili linafanyika vizuri kama walivyofanya wenzetu wa Nyamagana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Mheshimiwa Shekilindi, tukipata Wenyeviti wengine wa Mabaraza, tumeahidiwa tutarekebisha upungufu tunaopata kule Lushoto. Suala la upimaji, nafikiri halmashauri yake lazima ijipange. Kama watu hawana Hati, basi ni uzembe wa Halmashauri yake. Kwa sababu Wizara haiwezi kwenda kupanga na kupima kila mahali, lazima tujipange tufanye wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemsikia Mheshimiwa Mgumba, ni kweli leo amenipa siri kwamba Morogoro walinipiga changa la macho. Nitakwenda tena na kabla sijaenda nitashirikiana naye ili aniambie siri hiyo. Ni kweli yapo matatizo Morogoro, nakiri kabisa, lakini kwa sababu ya muda, nafikiri kwa sababu amenipa kidogo ufunguo, tutakwenda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Kigola, nimeshamwambia. Mheshimiwa Malecela Kilango amenialika kule, mimi nakwenda katika hizo Kata zote mbili. Mheshimiwa Lupembe amenialika Katavi, nitakwenda. Nikitoka Tabora nataka kwenda Katavi na nitakwenda na Mheshimiwa Waziri wa Ulinzi ili twende kuangalia hilo eneo mgogoro kati ya maeneo ya ulinzi na ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kusema nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge, hatuna nafasi ya kuwataja kwa majina lakini wamechangia kwa maandishi na wengine kwa kusema. Mengine yaliyotoka kwenye Kamati ni maelekezo yetu. Haya yote waliyoyasema yametusaidia sasa kupanga ratiba ya kazi na Mheshimiwa Naibu Waziri. Kutokana na hayo waliyoandika na waliyoyasema sasa tumejua twende wapi. Tutawafikia kwenye Wilaya zao ili mtufafanulie zaidi. Kabla hatukwenda tutahakikisha tutawatafuta kwa simu ili tushiriki wenyewe kwenye Mikutano katika Wilaya zao. Tungependa wafunguke zaidi tukiwa pale ili angalau tushirikiane katika kukomesha hii migogoro katika maeneo yenu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nisisitize mambo matatu ya mwisho. Nataka kusisitiza kwa wananchi wote na viongozi na wananchi kwamba ulipaji wa kodi ni suala la kisheria, tumeongeza muda, hatuongezi tena, naomba wananchi wote walipe kodi. Baada ya mwezi nilioutangaza, sasa wale ambao wana malimbikizo wataanza kupelekwa Mahakamani kuanzia mwezi wa Sita. Naomba tulipe kodi kwa maendeleo ya Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ziko taasisi za Serikali ambazo tunafikiri hazifanyi biashara kuzifutia madeni haya, lakini pia kuziangalia namna ya ulipaji wao wa kodi. Hatuwezi kutoza kodi kwenye Zahanati, Shule za Msingi na Shule za Sekondari ambazo hazitengenezi faida. Vile vile vipo Vyuo na Taasisi za Serikali ambazo zimeomba zifutiwe, lakini zinafanya biashara. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mnataka kufutiwa. Tutaangalia ardhi ambayo mnaitumia kwa mabweni na kwa madarasa, lakini yale maeneo mnayofanya Mlimani City tutawatoza kodi. Kwa hiyo, siyo kwamba kila Taasisi ya Serikali tutaisamehe. Yale maeneo ambayo mnatoza hela na sisi tutatoza kodi. Yale ambayo mnafanyia bure nasi tutawasamehe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nizungumzie habari ya urasimishaji. Nimesema nawaombeni viongozi wote tushirikiane tufanye suala hili la urasimishaji, lakini partners wa urasimishaji makampuni binafsi lazima tuwe na nidhamu katika kufanya jambo hili. Imeonekana kama jambo hili sasa halina mwenyewe, mnaingia ingia hovyo, wasio na sifa na wenye sifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeagiza bodi zangu zote zinazoshughulika na upimaji na upangaji zisimamie na kuhakikisha zinayafuatilia makampuni binafsi yanayokwenda kufanya kazi hii kwa kukiuka utaratibu. Jana nilisema, wananchi wanachanga wenyewe gharama za urasimishaji, Serikali haichangii, lakini fedha zile zisiende mikononi kwa kampuni, zikae kwenye kikundi cha urasimishaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kusema nawaomba sana Halmashauri zote zisimamie suala la matumizi bora ya ardhi. Kupanga matumizi bora ya ardhi katika vijiji na miji ni kazi yetu wote. Naahidi kama nilivyosema, vifaa vya upimaji tutavisambaza kwenye kanda ili Halmashauri ivitumie. Lengo ni kupunguza gharama kwa wananchi ili kasi ya upangaji na upimaji iende kwa kasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, narudia kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kama nilivyomshukuru mwanzo kwa kasi na ushauri mbalimbali ambao amekuwa anatupa. Sisi tunafanya kazi na pongezi hizi, lakini mjue kuna mtu anatusukuma tunafuata vision yake na mnajua aliwahi kuwa Wizara hii na kasi yake, vision yake tunaifuata. Tunamshukuru sana kwa msukumo na ushauri wa mara kwa mara ambao anatupatia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwaahidi kwamba baada ya bajeti hii, tutapanga ratiba ili tupate fursa ya kuwatembelea Waheshimiwa Wabunge kwa sababu ratiba yenu sasa tumeshaipanga kulingana na kero mbalimbali mlizotupatia hata ambao wameandika kwa maandishi tumeona kero zao. Tumejipanga, mpaka mwezi wa Saba ninyi wenyewe mtakuwa mashahidi kwamba kweli mlikuja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja.