Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Madini

Hon. Richard Mganga Ndassa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sumve

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Madini

MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Niunge mkono hotuba zote mbili kwa maana ya hotuba ya Waziri pamoja na hotuba ya Kamati ya Madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita sana katika kushauri na moja litakuwa ni ombi na baadaye Mheshimiwa Waziri atakaposimama kesho basi anisaidie kupata majibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa jana kuizinduzia rasmi Tume ya Madini chini ya Prof. Kikula pamoja na wenzake akiwepo pia Prof. Mruma. Sina wasiwasi na watendaji hawa kwa sababu nawafahamu ni wazuri. Mheshimiwa Rais amewaamini na kwa sababu ni watu wenye weledi mkubwa Tume hii ya Madini sasa wataibadilisha italeta taswira ambayo itaakisi matokeo mazuri kwa rasilimali zetu ambazo Mungu Mwenyezi ametujalia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine niishauri Serikali, nimejaribu kupitia kitabu naangalia zile takwimu, madini yanayosafirishwa nje au yale yanayouzwa ndani ukiangalia rasilimali zote tulizonazo, takwimu hizi kama vile zimepikwa, lakini hata kama zimetengenezwa kwa uhakika zitakuwa ni za uwongo kwa sababu madini tuliyonayo na takwimu tulizoonyeshwa hapa hazifanani hata kidogo. Mimi naomba sana Tume hii nategemea mwakani utakapokuja Mheshimiwa Waziri atatuletea takwimu za madini yote, siyo almasi peke yake, dhahabu peke yake, atuletee takwimu za madini yote kokote yanakochimbwa. Kwa mfano, hapa ametulea takwimu za madini yanayouzwa ndani, yanayouzwa nje, ametaja Chunya na Mwanza peke yake, sasa nikawa najiuliza hivi madini yako Chunya na Mwanza peke yake, kwa maana ya Kanda, hizo Kanda zingine kwa nini hawakuonesha? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa sababu ofisi hii ni mpya kwa maana ya Wizara iwe inatupa taarifa kamili za kila Kanda ni kiasi gani imekusanya na hili liwe jukumu lao. Nimwombe Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati, najua atatoa taarifa yake Machi mwakani, napenda tupate taarifa kamili kwa kila Kanda imefanya nini na imekusanya nini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba Tume hii iongeze ukusanyaji wa maduhuli. Kwa sasa wanasema mpaka Machi wamekusanya shilingi bilioni 310 ni ongezeko la asilimia 59 lakini inawezekana walikisia makisio ya chini, haiwezekani mka-surpass kwa asilimia 59 hata kidogo. Tunaomba makisio yafanane na hali halisi ya kile ambacho kinavunwa, makisio hayo ni madogo mno. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Tume hii wasiwe na urasimu wa kutoa leseni. Nimwombe Mheshimiwa Waziri anisaidie, kuna machimbo ya dhahabu ya kule Muheza, machimbo yapo sehemu moja inaitwa Magambazi kupitia kampuni ya CANACO, Mheshimiwa Doto mdogo wangu alienda pale akapaona, akazungumza na Mkuu wa Mkoa, mwekezaji yule amewekeza pesa zake nyingi, hebu lisuluhisheni hili ili huyu mwekezaji aweze kufanya kazi zake lakini pia Serikali kupita machimbo yale tuweze kupata mrabaha wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine tuna GST, najua Profesa Mruma alikuwa kiongozi pale, anajua matatizo ya GST, kazi zao zinajulikana lakini huyu mtoto GST hatumtendei haki kwa sababu hatumpi pesa za kutosha za kwenda kufanya utafiti wa maeneo ambayo kuna madini. Tunampa pesa kidogo lakini tunamwambia akafanye utafiti, hawezi kwenda kufanya utafiti kwa sababu hana pesa za kutosha. Kwa hiyo, niombe sana ili GST ifanye utafiti na moyo wa kujitolea ni lazima watu hawa wapewe pesa za kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kwa hayo makampuni ya wawekezaji wanapokuja nishauri sana Mheshimiwa Waziri ushirikishwaji wa wananchi kule kunakochimbwa madini ni wa muhimu. Ni lazima kuwe na sheria inayomtaka mwananchi kushiriki, kwamba wewe mwekezaji wetu, tunashukuru umekuja lakini ni lazima kuwe na clause inayosema ni lazima uchangie au ufanye moja, mbili, tatu. Ukimwachia huyu mwekezaji peke yake aamue yeye kwa jinsi anavyotaka na ataamua, anaweza akatoa au asitoe, lakini kama kutakuwa na clause inayosema kwamba lazima utatoa hiki na hiki na hiki hii itasaidia, huo ndiyo utakuwa ushirikishwaji mzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kitabu cha hotuba ya Mheshimiwa Waziri anazungumzia mambo ya sera na sheria. Wizara imetengeneza Kanuni saba za Madini ambazo sitaki nizitaje kwa sababu ya muda, siyo vibaya kwa sababu hizi Kanuni nafikiri Waheshimiwa Wabunge, najua kwenye mfuko mmetupa zile sheria, tunamwomba sasa Mheshimiwa Waziri hizo Kanuni saba hizo, siyo vibaya akazileta Bungeni hapa na siyo tu kwetu hapa ni vizuri akazishusha mpaka chini kwa DC na RC kule ambako madini yanachimbwa ili kusudi wajue hizo kanuni zinasemaje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuhusu Mthamini wa Madini hasa Almasi yupo mmoja tu kama siyo wawili. Sasa Mthamini wa Madini ya Almasi akiwa mmoja au wawili unategemea nini? Anaweza akashirikiana na wale watu wa upande mwingine kuidanganya Serikali. Tuwe na
utaratibu mzuri wa kuwasomesha na siyo madini ya almasi peke yake nafikiri na madini mengine, tuwe na utaratibu wa kuwasomesha hawa wataalam wetu waje wafanye kazi ambayo tunaitaka ili mapato ya Serikali yaongezeke.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ni kuhusu utoaji wa leseni kwenye maeneo mbalimbali yale ambayo hayaendelezwi. Ndugu yangu amesema hapa Mheshimiwa Mwenyekiti wa Wazazi Mstaafu, yale maeneo ambayo yamechukuliwa na watu ambao hawayaendelezi, zaidi ya miaka 10, 20, 30, hivi tunasubiri nini kuwanyang’anya? Nashauri kwenye zile leseni muangalie namna nzuri zaidi, mbali ya kuandika jina na anuani muweke na picha ya huyo mwekezaji tuione, hii itasaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tena kwamba naunga mkono shughuli za Serikali lakini niwapongeze sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Mawaziri, Katibu Mkuu na taasisi zote zilizo chini ya Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.