Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Madini

Hon. Hamidu Hassan Bobali

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mchinga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Madini

MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza niendelee na kumuombea Kaka na ndugu yangu na Mbunge mwenzetu ambaye leo ameingia kaburini, Mheshimiwa Bilago, Mwenyezi Mungu ampokee na amlaze mahali pema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri na Naibu Mawaziri wote watatu bado ni wapya na huu ni mwaka wao wa kwanza, kwa hiyo, leo sitakuwa na malalamiko mengi ya kuwashutumu na kuwalaumu, nataka niwashauri. Personality zao nawafahamu namna walivyo na namna wanavyoweza kukimbia kwa sababu bado ni vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na suala la leseni za uchimbaji wa madini na utaratibu wa namna zinavyotolewa. Mwaka jana na mwaka juzi nililalamika kwamba kuna watu wamechukua leseni wakisema kwamba wanakwenda kuchimba au kuchukua gypsum kwenye eneo la Jimbo la Mchinga hasa katika Kijiji cha Mchinga. Watu hawa leseni wanazo kutoka Wizarani lakini Serikali ya Kijiji, Kata na Halmashauri hazijui. Zipo leseni 15 ambazo zimechukuliwa kwa ajili ya uchimbaji wa madini ya gypsum katika eneo la Mchinga lakini Serikali ya Kijiji na Halmashauri hazijui. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujua utaratibu ukoje, wakati ule Kamishna wa Kanda wa Madini alikuwa Ndugu yangu Benjamin Mchwampaka na baadaye akaletwa hapa akaja kuwa Kamishna Mkuu na sasa sijui yuko wapi, nilimwambia na suala hili akawa analijua na bahati alinipa ushirikiano wa kunipatia na addresses za wale wahusika na ni kweli kabisa alikiri kwamba hao watu wana leseni na wamechukulia leseni pale eneo la Mchinga. Nataka kujua sasa, utaratibu gani unatumika wa mtu akaenda kwenye eneo ‘A’ akaomba leseni akapewa, wakati wahusika wa pale hawajui? Kwa hiyo, hii ni changamoto kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni suala la mineral cutter. Hapa katika viwanja vya Bunge kuna watu ambao wanatuonesha namna tasnia ya madini inavyofanya kazi, tumekwenda kutembelea pale, jana mimi nimetembelea. Wale wanaohusika na suala la ukataji wa madini, nimekwenda kuangalia ile mineral cutter yenyewe kwa saa moja sijui ni gramu ngapi, ni kitu kidogo kabisa ambacho kinakatwa kwa kutumia saa moja na wakatuambia nchi yetu hazifiki hata mashine 200.

Mheshimiwa Mwenyekiti, asubuhi nimemsikia mchangiaji mmoja na mimi naunga mkono, hivi kwa nini Wizara isifikirie kununua mashine nyingi za kukata madini ili utaratibu wa ukataji wa madini ukawa unaharakishwa? Nimesikia kwamba kuna watu wanasimama foleni muda mrefu wakisubiri madini yao yawe yanakatwa kabla ya kusafirishwa nje ya nchi, lakini mjue kwamba madini ni fedha, tena fedha kwelikweli siyo ya masihara, madini ni fedha. Kama mtu anakaa na mzigo wa madini wa nusu kilo au kilo moja akisubiri kukata, hivi mtu huyo anashindwa kwenda kufanya mipango huko mipakani akavuka akaondoka nayo? Badala ya kuwa tunafikiria kwamba Serikali itakuwa inapata fedha kumbe tutakuwa tunapoteza mapato ya Serikali. Kwa hiyo, kama kuna jambo la makusudi mnapaswa kulifanya ni kuhakikisha kwamba hizi mashine za kukatia madini zinakuwa nyingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, tuwa- train watu wetu. Sekta ya madini ni muhimu kweli, ingeweza hata kuendesha nchi hii peke yake. Kama tutaweza kuweka udhibiti mzuri kwenye madini tunaweza kwenda Tanzania kwa kutegemea sekta ya madini. Chuo cha Madini mkitengee fedha za kutosha tu-train watu, tufanye kama ilivyo kwenye kilimo, kuna ma-Extension Officer mpaka kwenye Kata, ninyi mngeanzia hata kwenye Halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Halmashauri kama za kwetu kule Lindi, Ruangwa, ukitaka huduma ya madini unakwenda Kanda. Hivi kwa nini kwenye level ya Halmashauri hakuna watu wenu? Changamoto iliyopo ni kwamba huko kwenye Halmashauri, sifikirii kwamba hakuna Halmashauri ambayo siyo wadau wa madini, mchanga upo huko, kuna gypsum na kuna madini mengine ambayo yanapatikana katika maeneo hayo, kwa nini sasa Wizara isi-train watu wa kutosha, tutumie chuo chetu wenyewe, mkawa mmeajiri Maafisa Madini kwenye ngazi za Halmashauri, wangekuwa wanatusaidia sana kufanya hizi kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukienda nyumba zinazojengwa nchi hii Halmashauri zinakusanya mapato kwenye mchanga lakini Wizara sijui kama mmepata shilingi ngapi kwenye madini ya mchanga. Hapa nimesoma kitabu cha Kamati wanasema mpaka Machi mmepata asilimia 3 za maendeleo, lakini fedha zipo kama mngeweza kuwa na watu kuanzia kwenye ngazi zile za Halmashauri naamini mapato yangekuwa yanakusanywa na mngekuwa mnaweza kujiendesha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ni suala la STAMICO, limezungumzwa hapa kwamba STAMICO inaitia hasara nchi hii na ni kweli kabisa. Nikifikiria taarifa ambayo ilitolewa na Mwenyekiti wa Kamati Maalum iliyokuwa imeundwa na Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Doto ambaye sasa hivi ni Naibu Waziri wa Wizara hiyohiyo, ilionekana STAMICO haina tija kwa Taifa. Nashangaa Waziri, nilitegemea leo angekuja na hatua madhubuti ama kutuambia kwamba anaifanyia restructuring ya Management au mfumo wenyewe anautengeneza upya au anaamua kuiweka pembeni kuja na taasisi nyingine ambayo itakuja kusimamia masuala haya kwa sababu imekuwa ikilaumiwa maeneo mengi. Sasa na lenyewe hili ni jambo la kuliangalia sana kwa sababu kila mtu anayesimama analalamikia STAMICO, nadhani kama haina tija ni bora kuachana nayo kuona namna nyingine ya kufanya. Huu ni ushauri wangu mwingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, mimi binafsi nimetoka maeneo ya Lindi na Mchinga kule, tuna madini ya chumvi. Sasa hivi kumekuwa na utaratibu wa chumvi kuongezewa madini joto na wale wakulima wa chumvi wanalalamika sana kwamba upatikanaji wenyewe wa hayo madini joto ni changamoto, lakini siyo upatikanaji tu, wanachokilalamikia kingine pia ni gharama. Sasa nataka kujua, hawa wakulima wa chumvi ni wadogo kama walivyo wachimbaji wadogo wadogo, mna utaratibu gani wa kuwasaidia? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, imeelezwa kwamba mkulima wa chumvi aliyeko Mchinga anayelima katika lile eneo la Namdima analazimika naye pia aende Mtwara akapate hayo madini joto kwa Kamishna wa Madini wa Kanda. Kuna utaratibu gani wa kuweza kusaidia? Kama nilivyosema kwamba watu wa Madini kwa nini wasikae kwenye Halmashauri, kwa nini msi-decentralise haya mambo ya madini yakawa yanashughulikiwa kwenye ngazi za Halmashauri au walau ngazi ya Mkoa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kumalizia, Wilaya ya Lindi pamoja na Wilaya ya Kilwa tuna deposit nyingi sana ya gypsum. Naomba sana muandae utaratibu kwa sababu wale watu wanaosomba madini ya gypsum wanatumia barabara hizi ambazo zinatengenezwa na TARURA, baada ya miezi mitatu au sita TARURA wanatumia pesa kuzitengeneza baadaye wao wanatumia magari makubwa wanapita mule wanaharibu zile barabara. Kuna utaratibu gani wa kufanya compensation? Kwa sababu kwenye Halmashauri tunaamini kwamba hawa wanaochimba madini ya gypsum wanapaswa walipe fidia ya barabara kwa sababu wanaziharibu na magari wanayotumia ni makubwa, kinyume na utaratibu na uwezo wa zile barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana mtoe maelezo magari yote makubwa ambayo yanabeba gypsum, kwa mfano eneo la kutoka Kilanjelanje pale Kilwa kuingia kule ndani kuna magari mengi makubwa ya tani 18, 30 yanabeba gypsum katika barabara hizi za TARURA wanatusababishia barabara kuharibika ndani ya muda mfupi sana. Kwa hiyo, tunaomba Waheshimiwa Mawaziri kama kuna chochote ambacho wanapaswa wakitoe kama fidia mtueleze ili nasi tuendelee kuwadai. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, nawatakia kila la kheri Mawaziri watatu wa Wizara hii.