Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Madini

Hon. Rashid Abdallah Shangazi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlalo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Madini

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuchangia katika Wizara hii mpya kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nami niwapongeze Mawaziri wote wanaohudumu katika Wizara hii. Pia nimpongeze sana Katibu Mkuu Profesa Msanjila kwa kazi kubwa ambayo anaifanya na nipongeze dhamira njema kabisa ya Mheshimiwa Rais kutenganisha Wizara hii kutoka Nishati na kuifanya sasa kuwa Wizara kamili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze na suala hili la Corporate Social Responsibilities. Tumeona miradi mingi sana ya madini bado haijaweza kuleta manufaa kwa wananchi wanaozunguka maeneo ambayo madini yanatoka. Hapa tunaona tatizo liko kwenye sheria. Sera ya Madini iko wazi kabisa inaeleza umuhimu wa makampuni ambayo yanachimba madini katika maeneo husika kuweza kusaidia katika jamii zile zinazozunguka, lakini Sheria yetu ya Madini iko kimya katika jambo hili. Nataka Waziri mwenye dhamana na Wizara kwa ujumla waje na majibu yanayoonesha namna sera na sheria zinavyoweza kuungana na kuweza kuleta harmonization kiasi kwamba wananchi wanaotoka katika maeneo ambayo madini yanachimbwa waweze kufaidika na huduma hizi za kijamii na tusiachwe na mahandaki kama walivyofanya Mgodi wa Resolute kule Nzega. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo napenda nilizungumzie ni suala la madini ya ya madini ya bauxite ambayo yanapatikana katika Milima ya Usambara, Wilaya ya Lushoto. Tunayo madini mengi sana kule yanapatikana katika Kata za Malindi, Magamba, Soni eneo la Shashui pia na eneo la Makanya kule Lushoto. Madini haya inawezekana kwa kutofahamu tunayatumia kama sehemu ya kifusi barabarani lakini kwa kuwa sasa Wizara hii ina Mawaziri wa kutosha ambao wanaweza wakatembelea maeneo tofauti tofauti niwasihi sana wafike Lushoto waweze kuja kutoa elimu kwa wananchi wa Lushoto ili pamoja na rasilimali nyingine ambazo tunazo basi tuanze kufaidika na rasilimali hii ya madini ya bauxite ambayo ni madini muhimu sana na ambayo yana thamani sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, wapo wachimbaji wachache ambao wanachimba madini haya lakini bado katika Halmashauri hatujafaidika kwa kiasi kikubwa na upatikanaji wa rasilimali hii ya madini. Kwa sababu wanayachukua katika malori makubwa na wengi wanapeleka katika nchi jirani ya Kenya, naamini kwamba hata Serikali pia inakosa mapato. Kwa hiyo, pamoja na elimu hiyo watakayokuja nayo lakini watutafutie wawakezaji ambao wanaweza wakaja wakayachenjulia kule Lushoto ili angalau kile ambacho ni stahiki wachukue na yale mabaki yetu basi tubaki nayo tuendelee kutengenezea barabara zetu kwa sababu pia Lushoto tuna uhaba mkubwa wa ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la Tume ile ya Makinikia ambayo iliundwa, lakini nimejaribu kupitia katika kitabu sijaona mahali popote zile dola milioni 300 zimeandikwa. Sasa namuomba sana Waziri mwenye dhamana atakapokuja kujibu hapa aniangalizie kwamba zile dola milioni 300 ziko katika eneo lipi. Natambua kwamba Mheshimiwa Prosefa Palamagamba Kabudi ndiyo alikuwa mkubwa wa ile Timu ya Maridhiano, hivyo hili jambo nalo tungeweza kupata majibu lingetusaidia sana kuondoa sintofahamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nizungumzie suala la madini ya urani ambayo yanapatikana katika Hifadhi ya Taifa ya Selous haswa katika eneo la Wilaya ya Namtumbo. Zipo tetesi mitaani zimeenea kwamba yale madini yanachimbwa kwa siri. Ningependa kujua kutoka Serikalini kwamba jambo hili lina ukweli kiasi gani kwa sababu ile ni rasilimali yetu wote na hata kama iko ndani ya hifadhi, bado hifadhi hizi zipo kwa mujibu wa sheria na sheria hizi tunazitunga sisi. Yapo mambo yanaweza yakafanyika na tunaweza tukapata muafaka wa eneo hili lakini siyo vizuri kama Wabunge tukaendelea kupata maneno haya kwa siri kwamba urani inachimbwa katika Hifadhi ya Selous haswa katika eneo la Wilaya ya Namtumbo, ingependeza sana kama tungepata majibu kwa uhakika zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo pia ni pongezi kwa Jeshi letu la Ulinzi ni suala la ujenzi wa ukuta katika machimbo ya Mererani, kila Mbunge amesimama hapa amelipongeza ni jambo nzuri. Nataka niseme pamoja na dhamira nzuri ya Rais na jitihada hizo ambazo Jeshi wamefanya, bado kuna jitihada za makusudi zinatakiwa ziangaliwe katika eneo linalogusa kodi, ni kwa nini madini haya yanatoroshwa kupitia nchi jirani ya Kenya, hapa lazima Wizara iende mbali zaidi kulitafutia ufumbuzi. Kujenga ukuta ni jambo moja lakini kutengeneza sera na miongozo mbalimbali inayotoa incentive nzuri kwa wasafirishaji hawa wa madini inaweza ikapendeza zaidi ili kuwavutia wasiwe na hamasa ya kupitia nchi jirani katika mipaka ambayo siyo rasmi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo liendane pia na madini katika Kanda ya Ziwa kwamba madini mengi yanatoroshwa kupitia Kenya. Wafanyabiashara wa Kenya wanawaambiwa kabisa hawa wafanyabiashara wadogo wadogo bwana wewe ukishafikisha hapa tayari ni suala
dogo yanakwenda huko duniani. Kwa hiyo, tuziangalie pia sheria zetu haswa katika maeneo ya kodi kwamba kodi zetu ni rafiki kiasi gani kwa wachimbaji hawa wadogo wadogo lakini pia wachimbaji wakubwa ili ziweze kutoa nafasi kwa kuruhusu mambo haya kufanyika ndani ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine kwa ujumla ambalo limezungumzwa ni STAMICO. STAMICO kweli ni janga kama ambavyo Wabunge wengi wamesema. Katika vitu ambavyo unawea ukawashangaa STAMICO kwamba pia wameshindwa ni katika hata migodi hii ya chumvi. Kutengeneza chumvi ni kazi rahisi sana, ni kuchukua maji ya bahari na kuyaweka katika mabwawa na baada muda tayari chumvi imetengenezwa. Hivi ninavyozungumza Mgodi ule wa Salt Mining kule Saadani umekufa, kule Uvinza umekufa, lakini STAMICO hawa ndiyo ambao wametufikisha hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe Mheshimiwa dada yangu Angellah haya maoni ya Wabunge hebu yachukulie kwa kina, sidhani kwamba ni vema sana kufufua hili Shirika la STAMICO. Tungekwenda mbali zaidi tukatafuta solution nzuri ili angalau tusije tukaingia tena kwenye mtego huu ambao umetufikisha hapa tulipo. Hii migodi midogo midogo ya kokoto na chumvi kama imewashinda sidhani bado tunaweza tukawapa jukumu kubwa hili la haya madini ya uranium, nickel na madini mbalimbali ambayo yanaendelea kugunduliwa katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nitoe rai kwako Waziri kwamba alichukue jambo hili kama ni angalizo kwa Waheshimiwa Wabunge na kama anadhani kuna namna pekee ya kutushawishi basi siyo vibaya akatungenezea semina na hao watu wa STAMICO tukajadili na tukachakata na tukajiridhisha kwamba kweli wanaweza wakabadilika. Kama walivyo sasa naamini kabisa kwamba hili ni janga na tusingependa hela za Serikali ziendelee tena kupotea katika shirika hili.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante sana.