Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Lupa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili nami niweze kuchangia hoja yetu ambayo iko mezani.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, Manaibu Waziri wote wawili na Watendaji wote Wizarani kwa kazi kubwa wanayofanya kwenye sekta hii ya madini iweze kuchangia maendeleo ya Watanzania. Mnachapa kazi kweli kweli, nimeona mnafika kila mahali, hata kwangu Chunya mmefika na huko mnatimiza Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwa ruhusa yako nisome sehemu moja kwenye Kitabu cha Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 22, anasema, “Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia GST na STAMICO chini ya mradi wa usimamizi endelevu wa rasilimali madini, ilikamilisha utafiti wa kina wa kijiosayansi uliohusisha uchorongaji na ukadiriaji wa mbale katika maeneo ya wachimbaji wadogo kwenye maeneo sita ya ujenzi wa vituo vya umahiri vya Katente huko Bukombe, Itumbi Chunya kwangu, Kona - Tanga, Kapanda – Mpanda, Buhemba – Musoma na Kyerwa. Vituo hivyo vitatumika kwa ajili ya mafunzo ya uongezaji thamani madini na uchimbaji salama pamoja na kuongeza uzalishaji, tija na hivyo kuongeza mapato kwa wachimbaji wadogo.” (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana Wizara kwa jambo hili. Naomba kwenye kituo changu na vituo vingine vyote ambavyo mmevisema, mkivijenga na kuvianzisha, muweke mitambo ya kukodisha wachimbaji wadogo wadogo. Kwa sababu sehemu kama Chunya kwangu Wilaya nzima ni mwamba, dhahabu iko chini ya mwamba. Kwa hiyo, wachimbaji wadogo wadogo wanashindwa kupata vifaa vya kuweza kuchoronga hiyo miamba na kuweza kuifikia dhahabu. Kwa hiyo, naomba kwenye vituo hivi muweke mitambo yote ya kuweza kukodisha ili wachimbaji wadogo waweze kupata huduma hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nilimwomba Mheshimiwa Waziri wa Nishati kwamba kwenye kituo changu cha Itumbi ambako anaweka hii Center of Excellence wapeleke umeme kwenye awamu hii ya tatu ya REA. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri wa Nishati apeleke umeme kwenye kituo hiki cha Itumbi ili wachimbaji wadogo wadogo waweze kunufaika na kituo hiki ambacho mnawachimbia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda kuishukuru Serikali na Wizara, wamenijengea mtambo wa kuchakata na kuvunja miamba na mawe kwenye Kituo cha Matundasi ili kuwasaidia wachimbaji wadogo wadogo. Naishukuru sana Serikali, naomba mwendeleze mpango huu kwa sehemu nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya nzima ya Chunya, hata kwenye nyumba ya Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya ni leseni za utafutaji. Wilaya nzima ya Chunya imejaa leseni za utafutaji ambapo wenye leseni hizo wako Dar es Salaam, siyo wachimbaji wadogo wadogo wa Chunya. Leseni yake ikiisha kwa mujibu wa sheria, huyu mtu anakwenda Wizarani kama anarudisha nusu, lakini hairudishi, anaomba kwa kutumia kampuni nyingine ya mtoto wake au ya mjomba wake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Wizara kwa huu moto mlioanza nao, kupitia Tume ya Madini, mpitie upya leseni zote katika Wilaya ya Chunya. Kuna watu ambao wana leseni ya utafutaji kutoka mwaka 2007/2008 mpaka leo anayo yeye mwenyewe, wakati sheria inasema ikifika miaka minne hujapata chochote, unarudisha nusu kwa Kamishna wa Madini, unabaki na nusu, hawajafanya hivyo. Naiomba sana Wizara ipitie upya kupitia Tume ya Madini ili leseni hizi zirudishwe wapate wachimbaji wadogo wadogo waweze kujiongezea kipato. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana hili lifanyike kwa sababu kuanzia Chunya Mjini kwenda Makongolosi, Malangamilo kwenda Ngwala mpaka Mbikatoto, maeneo yote hayo ni leseni za utafutaji na waliokamata leseni hizo ni wajanja ambao wako Dar es Salaam (speculators), wana- speculate kwamba atapata lini. Naomba sana Serikali ilishughulikie suala hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri Mkuu alikuja Chunya nawe ulikuwepo, nashukuru sana kwa ziara ile. Mlitembelea kampuni fulani ya uchimbaji ambayo mliona inatii sheria, hata hii Sheria mpya ya Madini ya 2017 kampuni hiyo inatii. Hiyo kampuni ikaomba iwemo kwenye mchakato wa kujenga smelter nchini. Naomba sana Wizara hii ya Madini iifikirie kampuni hiyo ambayo iko Chunya ili smelter ya kuweza kuchakata makinikia ijengwe Chunya ili yasiende nje ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee pia ruzuku kwa wachimbaji wadogo wadogo. Wizara imeanza na ni jambo jema sana. Kwangu Chunya mmetoa kwa wachimbaji wawili, watatu, naomba Wizara iendelee kutoa ruzuku kwa wachimbaji wadogo zaidi ili waweze kuinua kipato cha nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii, naunga mkono hoja.