Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Madini

Hon. Ester Alexander Mahawe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Madini

MHE. ESTHER A. MAHAWE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii nami niweze kutoa mawazo yangu katika bajeti hii ya Wizara ya Madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba huwezi kuanza kuzungumza habari ya madini na rasilimali za nchi hii pasipo kutoa pongezi kwa Mheshimiwa Rais. Nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli kwa nia yake ya dhati ya kulinda maliasili ya Taifa hili yakiwemo madini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nia yake ya dhati imepelekea kujengwa kwa ukuta katika Mji wa Mererani Mkoani Manyara ambako ndiko nakotokea mimi. Nia hii ya dhati imepelekea Jeshi letu la Ulinzi kulinda ukuta ule, nimeona watu wanabeza ulinzi wa Jeshi letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukizungumza suala zima la uzalendo, uzalendo huo unapatikana jeshini kwa asilimia 100. Isingewezekana tuweke ukuta wa gharama kiasi kile halafu tuweke walinzi wa Jadi. Kwa hiyo, mimi nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa ujenzi wa ukuta ule na hatimaye kuweka Jeshi letu kulinda maliasili zilizoko pale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunajua kwamba bado tunahitaji CCTV Camera kwa ajili ya kudhibiti upotevu ama utoroshwaji wa madini kwa namna nyingine, maana eneo lenyewe ni kubwa ni kilometa zaidi ya 24. Kwa hiyo, niombe tu Serikali iendelee na nia yake ya dhati kabisa ya kudhibiti upotevu wa madini, siyo tu madini ya tanzanite yaliyoko Mererani lakini maeneo mengine yote ambako madini ya namna mbalimbali kama dhahabu na madini mengine yanakopatikana ili madini haya yaweze kusaidia uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nitoe pongezi za dhati kwa Mawaziri wa Wizara hii nikianza na Mheshimiwa Angellah Kairuki, Mheshimiwa Doto Biteko na Mheshimiwa Stanslaus Nyongo. Hawa watu wanafanya kazi, tunawaona muda mwingi wapo field na kazi yao inaonekana kusema ule ukweli. Kazi yao imepelekea sasa kuongezeka kwa mapato haya kupitia mauzo ya madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukirudi katika eneo la Mererani ongezeko la pesa ambayo ilikuwepo kabla ya 2017/ 2018 tumeiona, ongezeko limekuwa kubwa madini haya sasa yanawafaidisha wananchi wa Manyara pamoja na Tanzania kwa ujumla. Niseme hongera kwa Rais, hongera kwa Serikali kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue pia nafasi hii kupongeza Bunge lako Tukufu ambalo lilifanyia marekebisho Sheria ya Madini ya mwaka 2017 na Kanuni zake saba zilizoundwa kwa ajili ya kuhakikisha malengo ya kulinda na kudhibiti rasilimali hii ya madini yanatimia. Mwaka jana tulipitisha hapa Sheria mbili za The Natural Wealth and Resources (Permanent Sovereignty) na The Natural Wealth and Resources Contracts (Review and Re-Negotiation of Unconscionable Terms), kisa ni kwamba lazima tuhakikishe madini haya yanawanufaisha Watanzania ambao ni wazawa na ndiyo wenye uchungu na madini haya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la EPZA pale Mererani. Naomba Serikali itusaidie kuhakikisha kwamba EPZA wanawavutia wawekezaji ili lile eneo pale liweze kutumika. Tuna eneo kubwa tu ambalo lina almost hekari 1,311 ambalo ni kwa ajili ya uwekezaji. Tunaomba Serikali kwa kushirikiana na Wizara ya Madini pamoja na EPZA waweze kujenga eneo lile ili kuweza kuwavutia wawekezaji ili madini yale yachakatwe, yauzwe mahali pale na ajira na mapato yaweze kuongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie ajira katika sekta ya madini. Kwa mujibu wa tafiti zilizofanywa mwaka 2012 tulikuwa na ajira kati 500,000 mpaka 1,500,000. Nataka tu kufahamu ni takribani miaka sita sasa tangu tafiti hizo zimefanyika, maana kwenye kitabu hiki sijaona ajira hizo zimeongezeka ama zimepungua kwa kiwango gani kwa mwaka huu 2017/2018. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia ukiangalia dira na dhima ya Wizara hii ya Madini ni kuhakikisha pia wanabuni na kusimamia sera, mikakati na mipango ya kuendeleza sekta ya madini; kusimamia migodi na kuhamasisha shughuli za uchimbaji pamoja na utafutaji wa madini; kuratibu na kusimamia uongezaji wa thamani ya madini kwenye biashara ya madini; kukuza ushiriki wa wazawa yaani local content kwenye shughuli za utafutaji; kusimamia na kuratibu shughuli za maendeleo ya wachimbaji wadogo; na kusimamia taasisi na mamlaka zilizoko chini ya Wizara hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa dhima ya Wizara hii inajieleza, tuna wachimba wadogowadogo nchi hii. Eneo la Mererani tuna wachimbaji wadogowadogo wanaitwa Apolo, niombe Serikali iweze kusaidia kuwapa elimu ya kijiolojia kwamba madini haya yanapatikana wapi zaidi, ukiacha eneo tu la Mererani lakini pia wapatiwe elimu ya namna ya uchimbaji na ruzuku ili waweze kusaidia familia zao na kuongeza mapato kwa ajili ya nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, siku za nyuma kulikuwa kuna pesa wanapewa wachimbaji wadogowadogo kama ruzuku. Nishauri kwa kuwa zile fedha wakati mwingine utakuta walikuwa wanagawana nusu kwa nusu na hawa waliokuwa wanawapatia hizo fedha zikawa haziwanufaishi kihivyo, wapewe vifaa vya uchimbaji. Hivyo vifaa vya uchimbaji vinaweza vikawasaidia wachimbaji hawa wadogowadogo na kuwainua na hatimaye kuwa wachimbaji wa kati na wakubwa ambao wataongeza thamani ya kazi wanayoifanya na hatimaye kuongeza mapato. Kwa hiyo, niombe sana watu hawa wapatiwe mafunzo ya kutosha ya kiteknolojia ili na wao waweze kuchimba kisasa zaidi kuliko kuchimba kwa njia ambazo ni za kizamani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mambo ya smelter yamesemwa na Wabunge wenzangu na mimi nichangie hilo. Ni muhimu kupata smelter sasa kwa sababu katika uchimbaji kwa mfano wa dhahabu ama tanzanite kuna madini mengi madogomadogo ambayo yangeweza kuongeza thamani ya madini yetu yanapotea kwa sababu smelter hii ilikuwa inatumika nje ya nchi. Niweze kuiomba Serikali na kuiombea Serikali yangu iweze kufanikisha suala la uwekaji wa smelter hapa nchini ili tuweze kufaidika na madini yale mengine yanayopatikana baada ya kuchenjuliwa kwa yale madini makubwa kama dhahabu na tanzanite. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna wachimbaji wadogowadogo ambao ni wanawake, ni nini mkakati wa Serikali katika kuhamasisha na kusaidia kuwapatia wanawake wachimbaji elimu ya kutosha ili na wao waweze kuongezeka kimapato na hata uwezo. Maeneo mengi yanayozunguka madini haya, wanawake kazi yao imekuwa ni kupika ama kufanya biashara ya mama ntilie. Ifike sasa mwanamke pia ainuliwe katika suala zima la uchimbaji wa madini. Wapo wanawake kadhaa tunawafahamu ambao kwa kweli wameweza kufanya hizi kazi, wamesomesha watoto wao, wamejenga nyumba zao na kusaidia ongezeko la mapato katika Serikali yetu. Kwa hiyo, naomba Wizara iangalie kwa macho mawili suala zima la kumuongezea mwanamke uwezo wa uchimbaji wa madini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bado madini haya hayajatangazwa vilivyo duniani ya kwamba yanatokea Tanzania na katika kijiji kidogo hicho ama maeneo madogo haya ya Simanjiro. Niliwahi kusafiri kwenda Marekani mwaka 2011 nikatembelea Taasisi moja inaitwa Tanzanite Liquidation Channel iko Austin pale Texas pale Marekani. Taasisi ile nilipofika pale ilikuwa imeajiri Wamarekani 400 wanaofaidi kupitia tanzanite inayotoka Mererani lakini karibu kabisa na maeneo ambako tanzanite hiyo inatoka, ukifika ukizungukia zile shule zilizoko maeneo yale, mfano shule moja inaitwa Imishie hawana...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana.