Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Madini

Hon. Joseph Kasheku Musukuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Madini

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kumteua Waziri wa Madini, dada yangu Mheshimiwa Angellah na kuwateua mapacha, vijana wazuri na namwomba sana dada yangu Mheshimiwa Angellah awalee hawa vijana, najua yeye ni senior kwao na tunaona kazi wanayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niliwahi kusema humu Bungeni ni vizuri sana Waheshimiwa Wabunge, kila mtu ana neema tofauti, ni vizuri sana ukajikita kwenye neema ambayo iko kwenye Jimbo lako kulikoni kuja kuropoka vitu ambavyo huna takwimu na huvielewi na haviwasaidii Watanzania wanaoumia na sekta ya madini. Nimesikia mchangiaji mmoja hapa anaropoka vitu ambavyo ni tofauti kabisa. Ukiangalia Wizara hii kwa sasa na zamani tulivyokuwa tunalalamika, acha Wabunge wananchi tunaowawakilisha, ni tofauti kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna watu humu ndani wana vitu ambavyo wanaweza kuzungumza wakati Wizara ya Miundombinu ilikuwa hapa, Mbunge mmoja tu nataka nimwambie, angeweza kuchangia kwa nguvu kubwa kwa sababu yeye ana fly over ya ghorofa. Kuna Wizara ya Maliasili ni vizuri sana mtu anayemiliki mbuga za wanyama Serengeti akajikita kuchangia kwenye Serengeti kusaidia watu wake kulikoni kuja kupotosha watu. Mtu anamiliki flyover anakuja kuchangia mambo ya dhahabu, anapotosha wananchi na hatusaidii watu ambao tumeumia na sekta hii ya madini. Nadhani wamejielewa watu ninaowazungumza, hiyo ni preamble, sasa naenda kuchangia. (Makofi)

T A A R I F A . . .

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo siyo taarifa wala siipokei. Hawa ndiyo wasomi tunaowategemea, huyo ni Mwalimu, ndiyo maana huwa nalalamika kila siku tuchunguze vyeti. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia sasa kwenye agenda halisi za Wizara ya Madini. Watu wa Geita tumekuwa tukilalamika muda mrefu kuhusiana na Mgodi wa GGM na kumekuwa na kutokuelewana. Kwa vile Wizara na dada yangu Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake ni wasikivu, mje mkae na Madiwani wa Halmashauri za Geita kwa kina, siyo kwa harakaharaka siku moja, mtusikilize mtoe maamuzi ili hili suala la kudaiana kati ya wananchi wa Geita na Mgodi liweze kuisha. Mnavyokuja tu mna-rush, mnatuma barua, hawa watu hawatusikilizi, ndiyo maana tunafika mpaka mahali tunasema tijichukulie sheria mkononi, siyo vizuri, namshauri sana Mheshimiwa Waziri hebu atafute muda aje atusikilize na aweze kufikia mwisho wa kulimaliza suala hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, sijui huu mgodi au sisi watu wa Geita tuna tatizo gani? Tulilalamika kuhusu tanzanite, Mheshimiwa Spika akaunda Tume. Kumekuwa na Tume ya Makinikia, watu wa Geita tumeomba mara nyingi kwa nini isiundwe Tume kwa ajili ya kuuchunguza Mgodi wa Geita GGM? Kwa bahati nzuri Mheshimiwa Rais ameshawapa tu mwongozo kwamba muangalie, mgodi ule ulikuwa unatoa dhahabu bila kuchunguzwa, sasa hivi tunaingia mpaka Halmashauri kuna tofauti kubwa, muanzie hapa ili muweze kuunda Tume.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine wako watu ambao wamekutwa na leseni ya mgodi, Mheshimiwa Kanyasu jana alizungumza vizuri. Wameenda Mahakamani, wamehukumiwa tarehe 19 Desemba, 2016, tarehe 20 baada ya hukumu ya Majaji sita, mgodi ukaandika tena warning ya kuwatoa wachimbaji wale. Jana Mheshimiwa Kanyasu alivyochangia tu, leo ninayo barua hapa jana mgodi unaandika kuwafukuza watu ndani ya eneo lao ambalo Majaji sita wamewapa haki ya kukaa pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Wabunge tuna haki ya kutetea watu wetu, Mheshimiwa Kanyasu amechangia jana leo kuna barua ya kuwafukuza, siku saba. Najua GGM wako hapa, Mheshimiwa Waziri akija hapa nataka atuambie kama GGM ni zaidi ya Serikali na ni zaidi ya mhimili wa Majaji sita tuelewe, lakini kama si sahihi basi naomba Mheshimiwa Waziri achukue hatua ya kuweza kuwasaidia watu hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mhimili ambao tunautegemea baada ya Serikali na Bunge kushindana ni Mahakama. Kama Mahakama ya Majaji sita, tena Majaji wanaoaminika Tanzania wametoa hukumu ya kuwapa haki wananchi hawa, inatokeaje mtu mmoja tu GGM anatoa siku saba kuwafukuza watu baada ya Mbunge kuchangia, hii ni dharau. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri alifanyie kazi na ana vijana shapu wanaweza kwenda hata kwa basi kusikiliza kesi hizi. Namwomba sana aende akatoe maamuzi kwenye hili suala hapa.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni Mgodi wa Buhemba, niombe sana Mheshimiwa Waziri katika vitu ambavyo tutakosea ni kuangusha wawekezaji wawili ambao mimi kama mfanyabiasha wa hiyo dhahabu, Mgodi wa Baraka na Mgodi wa Mauza, watu hawa tukifika mahali tukawafanya wakafilisika hatutakaa tupate mwekezaji Mtanzania atakayeweza kufanya kazi ya dhahabu. Sisi kama Kamati tumeenda tumeona, sawa kulikuwa na mwingiliano wa Jeshi lakini nataka niwaambie tu kwamba mazungumzo kama yanaendelea vizuri, ni vizuri tukawasaidia hawa watu wamewekeza zaidi ya dola milioni 25. Mtanzania wa kawaida amekopa, anaumiza kichwa tena darasa la saba, kitu ambacho hata watu wenye ma-degree wanaoropokaropoka humu hawawezi kufanya hivyo vitu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikuombe sana Mheshimiwa Waziri tusije tukafanya hiyo dhambi ya kuwaangusha hawa wawekezaji wazawa. Hata kama kulikuwa na makosa kwenye Wizara ya Madini na Wizara ya Ulinzi kaeni mmalize migogoro yenu watu hawa wapewe leseni waweze kuendelea na shughuli zao. Hata kama leseni inachukua process ndefu kuna njia nyingine mnayoweza kuitumia ili aweze ku-cover hayo mambo aliyonayo. Hawa watu wanadaiwa na mabenki, tukiwa-ignore hawa hamtamkuza Mtanzania yeyote kwenye biashara hii ya dhahabu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka kutoa ushauri…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, naunga mkono hoja lakini dada yangu kwenye shilingi ujaribu kuja na majibu mazuri naweza nikaondoka nayo. (Kicheko)