Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Madini

Hon. Goodluck Asaph Mlinga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ulanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Madini

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza naomba ni-declare interest kuwa na mimi ni mchimbaji ambaye mpaka leo bado sijafanikiwa. (Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitampongeza Mheshimiwa Rais kwa mpango wake wa kuzuia makinikia kupekwa nje ya nchi. Kwa nini nasema hivyo? Tanzania ni nchi ya nne kwa uzalishaji wa dhahabu nyingi katika Bara la Afrika na nchi ya 16 duniani tukitanguliwa na China, Australia na Russia. Katika orodha ya nchi matajiri wa uzalishaji wa mali tupo lakini mafanikio ya Serikali na wananchi yako chini. Kwa hiyo, hapa nimeona dhamira ya dhati ya Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze pia Mheshimiwa Rais kwa kuona umuhimu wa kujenga ukuta katika mgodi wa Mererani kwa sababu haya ni madini adimu katika dunia hii yanatoka Tanzania tu. Licha ya hivyo, Tanzania pia ni nchi ya nne kwa uzalishaji wa gesi katika Bara la Afrika na ni ya 22 katika dunia katika uzalishaji wa gesi. Hapo ndipo unapoona dhamira ya Mheshimiwa Rais katika kulinda rasilimali zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Mheshimiwa Spika naye kwa kuona kuwa suala la gesi ni muhimu kwa sababu nchi matajiri duniani ndiyo zinaongoza katika utoaji wa gesi na madini ya aina mbalimbali. Katika orodha za nchi maskini duniani Tanzania ni ya 25 toka mwisho tukitanguliwa na Central Africa, Congo na Malawi. Kwa suala la madini nchi yetu ipo juu, vinara katika kutoa madini lakini katika nchi maskini na kwenyewe tuko juu, ndiyo tunaona kuwa Mheshimiwa Rais ana dhamira nzuri na nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, namshauri pia Mheshimiwa Rais afanye pia reshuffle katika Wizara ya Madini kwa sababu watendaji wa Wizara ndiyo waliopelekea nchi hii kufika hapa leo hii. Mheshimiwa Waziri na Naibu Mawaziri tunajua mnafanya kazi vizuri lakini nawapa angalizo watendaji wa Wizara zenu ni wapigaji, nimeshaongea hapa tangu mwanzo kuweni nao makini hasa wanasheria. (Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili naomba nije kwenye Mkoa wa Morogoro. Mkoa wa Morogoro na Wilaya zake za Ulanga, Malinyi, Kilosa, Mvomero, Morogoro Vijijini, Matombo ni wilaya tajiri, tunatoa dhahabu tena dhahabu zake siyo kama za Wasukuma kule, dhahabu zetu sisi ni asilimia 98. Tunatoa rubi, graphite, copper, uranium kwa hiyo mkoa wetu ni tajiri kweli.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunatoa angalizo kwa Serikali hasa Wizara, kuna watumishi wa Wizara ya Madini wamehodhi maeneo makubwa kwa kutumia majina mengine. Anapotokea mtu anapotaka kuchimba unasikia eneo hili lina mtu, kumbe mtu mwenyewe ni mfanyakazi wa Wizara ya Madini. Kwa hiyo, tunaomba leseni zote ambazo ziko Mkoa wa Morogoro zifuatiliwe kwa undani zinachimbwa au lah, wamiliki halisi ni watu gani.

Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee sasa Ulanga. Jimbo langu la Ulanga miaka ya 90 kuna kijiji kimoja kinaitwa Lukande kilikuwa kinajulikana Thailand. Thailand walikuwa wanaijua Lukande kuliko Dar es Salaam, lakini kijiji hicho mpaka leo hii kimechimbwa madini yameachwa mashimo tu hawajanufaika lolote. Sasa hivi chini ya uongozi wa Mbunge wao kijana machachari nahakikisha hamna wizi wowote wa madini utakaofanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo langu lina makampuni makubwa mawili ya uchimbaji wa graphite ambayo ni TanzGraphite na Mahenge Resource. Mahenge Resource ndiyo tumeitambulisha juzi, inaanza mchakato wa kutaka kuongea na wananchi ili kuwaahamisha na kufanya malipo, TanzGraphite ina miaka sita lakini bado ina ubabaishaji, wamefanya uthamini wa mali za wananchi mwaka mmoja na mwezi mmoja, leo hii wanataka kuja kuanza kulipa. Sheria inamtaka ukishafanya uthamini miezi sita ina-expire lakini wao imepita mwaka mmoja na mwezi mmoja wanataka kulipa, wanataka kulipa kwa mkataba upi wakati tayari ile tathmini imesha-expire.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri aje na majibu, nimewaambia wao wenyewe kuwa uthamini unatakiwa ufanywe upya, maana tukiongea sisi Wabunge wanasema wameongea wanasiasa, tafadhali naomba tusidharauliane kwenye kazi, wafanyekazi yao na mimi kama Mbunge niwatetee wananchi wangu. Nahikikisha hakuna mwekezaji atakayewekeza kwa kukiuka sheria. Nawahakikishia wananchi wangu wa Ulanga na wananchi wa Ipanko walale usingizi mzuri, hakuna uwezekazaji mpaka wananchi wote wamelipwa haki yao inayostahili kisheria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi lingine kwa wananchi wa Ulanga, tunaomba ofisi ya Madini ifunguliwe katika Wilaya ya Ulanga. Ulanga tuna madini mengi, lakini hakuna Afisa Madini ambaye anayeishi huko huko.

Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee pia kuhusu wachimbaji wadogowadogo, Mheshimiwa Waziri tumeshaongea sana kuhusu wachimbaji wadogowadogo, hasa wa gemstone nikiwemo na mimi ambaye mpaka leo hii sijanufaika. Uchimbaji wa madini ni kama kamari lakini Serikali unapochimba haiangalii umewekeza shilingi ngapi na umepata kiasi gani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, nimechimba miaka miwili, nimetumia shilingi milioni mia moja, siku napata jiwe la shilingi milioni ishirini, Serikali inataka kodi hapo hapo, haijui mimi nimewekezaje. Ndiyo maana tunawaambia, mtoe semina na muwekeze kwa wachimbaji wadogowadogo, muwe nao karibu mtajua matatizo gani wanayapata. Sasa wewe hujui mtu amewekeza kiasi gani, haujui amepata kiasi gani, unaenda kumdai kodi, kwa mfumo huo hamtopata kodi kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana leo hii Mererani mmjenga ukuta sawa, lakini wale wachimbaji wadogo wadogo wanawapiga chenga. Cha msingi ni kuwafanya wawe marafiki inakuwa rahisi hata wao kujitolea kutoa kodi kwenu, kwa sababu inakuwa tayari mmeshawajengea mazingira ya ukaribu.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo nataka kuliongelea ni kuhusu kujenga ule mtambo wa kuchenjua dhahabu. Serikali ituambie sasa ni lini mtambo huo utakuwa tayari, kwa sababu tunajua dhahabu bado kabisa haijachimbwa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kidogo mpaka Waziri aje na majibu ya hoja zangu.