Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Madini

Hon. Jumanne Kibera Kishimba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kahama Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Madini

MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuchangia kwenye Wizara hii ya Madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitakwenda moja kwa moja kwenye dhahabu. Katika Jimbo langu la Kahama ni miongoni mwa maeneo ambayo yana machimbo mengi sana madogo madogo, pamoja na mgodi mkubwa wa Buzwagi na jirani yangu Bulyanhulu. Kinachosumbua sasa hivi, kule ni Sheria ya Madini ambayo watu wa migodi mikubwa wanatumia sheria hiyo hiyo na wachimbaji wadogo wadogo wanatumia sheria hiyo hiyo. Sasa hivi wachimbaji wadogo wadogo, akitoa mifuko 10 ya mawe ya dhahabu, anatoa mfuko mmoja kwa ajili ya madini, mfuko mmoja kwa ajili ya TRA, mfuko mmoja kwa ajili ya Halmashauri na mfuko mmoja kwa ajili ya mwenye shamba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mtu huyu akimaliza tena kusaga mchanga ule kwenda kutoa dhahabu analipa tena, mchanga ule tena ukienda kuchenjuliwa unalipiwa tena lakini huyu mwenye mgodi mkubwa akilipa ushuru wake yeye atarekebisha kwenye hesabu zake za TRA atapunguza zile gharama alizolipia, lakini huyu mchimbaji mdogo hana mahali ambapo anaweza kwenda ku-claim fedha aliyolipa. Matokeo yake inasababisha kuwa na rushwa na migogoro mingi sana maeneo yale. Kwa hiyo, tunaomba Wizara ya Madini ni vizuri ikaoanisha kati ya sheria ya migodi mikubwa na sheria ya wachimbaji wadogo wadogo ambao ni kama wakulima wadogo wadogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye suala hili la dhahabu nafikiri Serikali ingetamka wazi kwamba inataka kufanya kweli kazi ya dhahabu au ni kama tunataka kuruhusu uchawi lakini wakati tukiona bundi au fisi tunaogopa. Tanzania haina elimu ya biashara ya madini ina elimu ya miamba na tunachoibiwa na matatizo yetu makubwa yako kwenye elimu ya biashara ya madini ambayo haiko shuleni. Kwa hiyo, ni vizuri kama tunaamua kuruhusu biashara ya madini ionekane kwamba madini yameruhusiwa lakini hata tukiunda Tume 100, kama hatujasema wazi kabisa tunataka nini kwenye madini, bado tuna wakati mgumu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi ya Uganda leo ina- charge service levy ya export 0.5%; Rwanda wana-charge 0.6%; Burundi 1%; Tanzania tuna-charge 14%. Mheshimiwa Waziri hata kama ni wewe unaweza ukapata dhahabu ya Sh.10,000,000 ukalipa Sh.1,400,000, inawezekana? Umechimba peke yako, ukapata dhahabu ya Sh.10,000,000 ukabeba kupelekea Serikalini Sh.1,400,000, inawezekana? Wafanyabiashara hawa wanafanya biashara ya madini zaidi ya miaka 10 hata mke wake hajawahi kuiona dhahabu, ni vipi Serikali inaweza ikachunga dhahabu kutoka Lindi mpaka Mara? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sekta hii ya wachimbaji wadogo wadogo imeajiri zaidi ya watu milioni 5. Kwa hiyo, ni kweli Serikali kwenye kitabu inaonesha wamechangia asilimia 2 lakini tunapoteza zaidi ya tani 2 au 3 za dhahabu kila wiki. Kwa nini Serikali isiruhusu dhahabu ikawa 1% na alipe anaye-export ili hawa wachimbaji wadogo wadogo waondokane na huu msururu wa usumbufu walionao halafu wale wenye migodi mikubwa waendelee na procedure ya kawaida ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii itasaidia hata jirani zetu ambao wana madini wanaweza kuyaleta hapa kwetu. Ni vizuri Serikali ikafikiria sana kuruhusu madini kutoka nje. Ni kweli tuna mikataba ambayo inasema lazima wapate certificate of original lakini ni kweli sisi tunapokea wakimbizi kutoka Congo, tunapokea kila aina ya matatizo kutoka nchi jirani, tunaweza kupata ebola, mbona tunakataa kupokea dhahabu na tuko tayari kupokea dola? Ni vizuri Serikali ikafikiria upya maana dhahabu haina alama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini watu hawa watanunua mali hapa na sisi tutapata pesa kutoka kwenye kodi. Sisi hatufanyi service Msumbiji, hatutengenezi barabara Congo ina maana tutapata pesa ya bure. Kwa kuwa Mwanasheria wa Serikali na Waziri wa Sheria wapo hapa waiangalie sana hii Sheria ya Madini ambapo dhahabu ni moja lakini inapatikana kutoka kwenye vyanzo viwili tofauti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo, nahitimisha mchango wangu, naunga mkono hoja, ahsante sana