Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilindi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Mawaziri wote wawili kwa hotuba nzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wa sekta ya madini katika pato la Taifa. Niipongeze Wizara kwa jitihada kubwa za usimamizi wa sekta hii ambayo imeongeza mapato ya Serikali hii, ni jambo la kupongeza sana. Hata hivyo, katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ukurasa wa 25 katika marekebisho ya Sheria ya Madini ya mwaka 2017, Majukumu ya Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) na baadhi ya majukumu ya Kamishna yamehamishiwa Tume ya Madini, hili ni jambo jema pia. Ofisi zilizokuwa za Kanda na Maafisa Madini wakazi zipo chini ya Madini. Aidha, kila Mkoa utakuwa na Afisa Madini Mkazi na kila mgodi mkubwa na wa kati utakuwa na Afisa Mgodi Mkazi. Swali hapa ni kuwa, kwa wachimbaji wadogo wadogo, mfano Jimbo langu la Kilindi je, Serikali haijaona umuhimu wa kuwa na Afisa wa kusimamia? Mheshimiwa Waziri naomba kupata majibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, wachimbaji wadogo wadogo wana mchango mkubwa sana katika kuongeza pato la Taifa. Nashauri Kamisheni hii ya Madini ihakikishe kuwa katika maeneo yote ya wachimbaji wadogo wadogo pawepo na utaratibu wa Afisa Madini kwani watasaidia kutoa elimu na kutatua migogoro.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuimarisha usimamizi wa mapato ya Serikali, kwa mfano katika hotuba hii ukurasa wa 72 inaonesha makusanyo katika Wilaya ya Handeni hadi Machi 2018 ambao wanasimamia na Kilindi waliweza kukusanya Sh.191,177,340 tu. Hiki ni kiasi kidogo sana na hii imesababishwa na usimamizi mdogo na pengine baadhi ya watumishi kukosa uaminifu kwa kushirikiana na wachimbaji wadogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Wizara kuwa, kwa kushirikiana na Kamisheni ya Madini waone umuhimu wa kuleta Maafisa Madini katika maeneo ambayo yana wachimbaji wadogo wadogo. Hivi leo Afisa Madini yupo Tanga ambako kiukweli hakuna shughuli za uchimbaji, Serikali itakuwa na dhamira ya kusimamia mapato kweli?
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.