Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Madini

Hon. Richard Phillip Mbogo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nsimbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Madini

MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza natoa pongezi nyingi kwa Waziri na Naibu Mawaziri kwa utendaji na ushirikiano wao kufanikisha malengo ya Serikali. Pili, nampongeza Mheshimiwa Rais Joseph Pombe Magufuli kwa uthubutu wake wa kulinda maliasili za Taifa ili nchi na vizazi vijavyo viweze kufaidi. Mheshimiwa Rais amefanya mabadiliko katika Sheria za Madini pia sheria mpya za Permanent Sovereignty na Unconscionable Terms ambazo zitasaidia kupitia mikataba isiyokuwa na tija kwa Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna tatizo la maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo ambao wanahangaika sana kutafuta kipato. Hivyo, Serikali ifanye mpango wa kuwa na maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo na watambuliwe kwa kusajiliwa na wapewe leseni za bei nafuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilisimamisha utoaji wa ruzuku kwa wachimbaji wadogo miaka miwili imepita. Fedha hizo zilikuwa zinasaidia wananchi na kuwainua kiuchumi. Hivyo, tunaomba Serikali irudishe ruzuku hiyo na kuweka mpango mzuri ambao utanufaisha wachimbaji wadogo nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, ufadhili wa uchimbaji bora kwa vituo saba. Tangu 2016 Serikali ilitoa taarifa kuwa kutakuwa na vituo saba vya mfano ili kutoa mafunzo kwa wachimbaji wadogo na moja ya kituo hicho ni Ibindi, Jimbo la Nsimbo, Wilaya ya Mpanda, Katavi. Tunaomba kauli ya Serikali mpango huu wa World Bank utafanikiwa lini? Je, Serikali ina mkakati gani wa kuuendeleza?

Mheshimiwa Naibu Spika, service levy za councils na soko huru. Kwa mujibu wa Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa, kila aina ya biashara katika Halmashauri wanatakiwa kulipa service levy, lakini changamoto iliyopo ni usiri wa mauzo kwa wafanyabiashara wa madini ambapo huwa hakuna uwazi katika kununua na kuuza inapelekea Serikali kupoteza mapato. Hivyo basi, nashauri Serikali ianzishe soko huru kwa maeneo yote ili Serikali ipate mapato pia Serikali za Mitaa zipate service levy. Halmashauri ya Nsimbo ina wachimbaji wadogo wengi 98% ambao hawana uwazi na Halmashauri inapoteza mapato.

Mheshimiwa Naibu Spika, ugawaji maeneo kwa kigezo cha aina ya madini. Mkoa wa Katavi maeneo mengi yana madini aina tofauti tofauti, ukanda wa Wilaya Tanganyika ndio umepangwa kwa ajili ya wachimbaji wadogo lakini ukanda huo zaidi ni madini ya shaba ndiyo yanapatikana kwa wingi lakini Wilaya ya Mpanda, Jimbo la Nsimbo ndiyo kuna dhahabu, hivyo eneo hilo linafaa kutengwa kwa ajili ya wachimbaji wadogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuboresha sheria, sera na kanuni ili kufikia malengo. Serikali iendelee kuboresha sheria, sera na kanuni kwa kuzingatia pande zote za kulinda maliasili na uwekezaji kuendelea kukua.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Serikali iongeze kasi katika kutekeleza uwekezaji wa mashine ya uchenjuaji (smelter) ili kuokoa upotevu wa maliasili na kuongeza ajira nchini. Waziri atoe taarifa uwekezaji wa smelter umefikia wapi.

Mheshimiwa Naibu Spika, shukrani kwa nafasi.