Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Madini

Hon. Doto Mashaka Biteko

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukombe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Madini

NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTO M. BITEKO): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili na mimi nitoe mchango wangu kwa ajili ya hoja ambayo imewekwa mbele yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijasema, naomba nichukue nafasi hii vilevile nimshukuru sana Mungu, mwingi wa rehema ambaye ametupa uzima na afya mpaka kuifikia siku ya leo na kwa kweli bila yeye tusingekuwa hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba vilevile nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa imani kubwa ambayo alinipatia na kuniteua kuwa Naibu Waziri wa Madini. Naomba niseme tu kwamba nafasi hii ambayo ameniteua nitafanya kazi hii kwa nguvu zangu zote, kwa weledi mkubwa na kwa kumtanguliza Mungu mbele ili ndoto ambayo yeye anaiona kwa ajili ya nchi hii niweze kumsaidia kuifikia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba vilevile nimshukuru Mheshimiwa Waziri wa Madini, mtoa hoja, dada yangu, Mheshimiwa Angellah Kairuki, ambaye kwa kweli pamoja na mambo mengine amekuwa mwalimu mzuri sana kwangu. Mtafahamu mimi nimeteuliwa mwishoni, nimeingia Wizarani nikiwa mgeni. Mheshimiwa Waziri huyu, pamoja na kwamba yeye ni Mbunge mwenzangu, amekuwa mwalimu mzuri sana kwangu. Mimi naweza kuwa shahidi na Wabunge wengine ambao wameshafanya kazi na Mheshimiwa Angellah Kairuki watakuwa mashahidi, ni mtu wa pekee ambaye anapenda kuona kila mmoja anatumia kila talanta aliyonayo kutekeleza majukumu yake na yeye anakusaidia kufanya kazi yako kwa urahisi. Kwa kweli ningekuwa na muda wa kusema ningesema sana kwa bahati kubwa ambayo Mungu amenipa ya kufanya kazi na Mheshimiwa Waziri huyu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nimshukuru sana Mheshimiwa Stanslaus Nyongo, Naibu Waziri wa Madini. Huyu tunaitana pacha; yeye alitangulia kuteuliwa pale Wizarani, amenipokea, ameni-orient vitu vingi, nimejifunza mambo mengi sana kutoka kwake kwa namna ya utendaji lakini kuifahamu Wizara kwa sababu nilikuwa mgeni na yeye alinitangulia kufika hapo. Kaka yangu nakushukuru sana, Mungu akubariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi hii kuishukuru sana familia yangu; mke wangu mpenzi Bernadetha Biteko kwa kuendelea kunivumilia, yeye pamoja na watoto wetu, wakati natekeleza maukumu haya. Naomba niwashukuru sana wananchi wa Bukombe ambao wao ndio walinichagua na kunituma kuwawakilisha kwenye nyumba hii. Naomba niwahakikishie kwamba kazi ambayo walinipa kuifanya kwa niaba yao ntaendelea kuifanya kwa nguvu zangu zote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maneno hayo ya utangulizi, naomba sasa nitangulie kusema naunga mkono hoja. Kwa kweli hoja hii imeletwa muda mwafaka kwa sababu Wizara hii ni mpya na Waziri tuliyenaye ni Waziri mpya na tangu Wizara hii imeundwa ndio Waziri wa kwanza mwanamke, kwa hiyo, ni Wizara ya kipekee sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme tu kwamba mambo mengi sana ambayo yamewasilishwa na Waheshimiwa Wabunge ni ya msingi sana. Mchangiaji wa kwanza hadi wa mwisho, kama atakavyokuja kueleza mtoa hoja, wote ukiwasikiliza utaona mambo mengi wanayozungumza ni ushauri mzuri ambao unatuelekeza namna bora ya kutekeleza majukumu yetu ili sekta hii iweze kukua na iwe na mchango mkubwa kwa pato la Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli champion wa kubadilisha sekta hii ya madini hapa Tanzania ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Yeye ndiyo ametoa uongozi na uelekeo wa namna gani tusimamie sekta hii ili madini ambayo Mungu ametupa yaweze kuwanufaisha Watanzania. Rais wetu ametamani kwa muda mrefu na hicho ndicho anachotaka sisi wasaidizi wake tufanye, kuwasaidia Watanzania waweze kunufaika na rasilimali hizi. Naomba niseme juhudi kubwa ambayo Mheshimiwa Rais ameifanya na sisi chini ya Waziri, Mheshimiwa Angellah Kairuki, tutaifanya kwa mioyo yetu na nguvu zetu zote.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba nijielekeze kwenye michango michache ambayo Waheshimiwa Wabunge wameeleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza ambalo limeelezwa hapa ni kuwasaidia wachimbaji wadogo. Nieleze kwamba, historia ya wachimbaji wadogo Tanzania na Afrika kwa ujumla, ni ndefu sana. Sisi Tanzania wachimbaji wadogo ni wengi sana lakini tunazo changamoto ambazo tumezikuta na hizo ndizo tutakazozishughulikia ili tuhakikishe kwamba wachimbaji wadogo hawa wanakua, wanatoka kwenye uchimbaji mdogo wanakwenda kwenye uchimbaji wa kati; wanatoka kwenye uchimbaji wa kati wanakwenda kwenye uchimbaji mkubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo mtoa hoja amesema kwenye hotuba yake, uchimbaji mdogo ni hadhi ya muda mfupi. Sisi kama Wizara tunatoa msukumo mkubwa kuwasaidia wachimbaji wadogo. Ndiyo maana utaona tunahama kwenye majina ambayo wachimbaji wadogo kwa miaka mingi wamekuwa wakiitwa; mara wanaitwa wavamizi, wasio halali, wachimbaji haramu na majina mengine mabaya. Tunatamani tuwaone wachimbaji wa Tanzania wale wadogo wanakuwa wachimbaji ambao wanarasimishwa, wanachimba kwa kufuata sheria, wanachimba katika mazingira ya kutunza mazingira ili madini wanayochimba yaweze kuwa na manufaa kwao wenyewe na watoto wao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mzuri tumeuona. Kuna watu wengine wanadhani wachimbaji wadogo ukiwasaidia hawana tija. Tulikwenda Mundarara, Jimbo la Longido kwa Mheshimiwa Dkt. Kiruswa, tumekuta Wamasai kule ni wachimbaji wadogo wa ruby na Mbunge wa Longido naye amesema hapa; wamefanya maendeleo makubwa, wamejenga nyumba za kisasa, wamehama kwenye matende, wanaishi maisha mazuri. Tulipofanya mkutano pale wote wanafurahia kuona kwamba Serikali ya Awamu ya Tano inawapa fursa ya kunufaika na rasilimali zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi hii si nguvu ya soda, tutaifanya kwa nguvu zetu zote. Ndiyo maana kila mahali mnapotuona tunakutana na wachimbaji wadogo; kazi kubwa tunayoifanya ni kuwatia moyo na kuwapa miongozo ya Kiserikali namna gani watende kazi zao kwa uadilifu na walipe kodi za Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia hoja hii, sisi kama Wizara, sisi kama Serikali ya Awamu ya Tano kazi yetu itakuwa hiyo; kuwalea, kuwasaidia na kuwahamisha wachimbaji wadogo kwenye uchimbaji wa kubahatisha na kuwapeleka kwenye uchimbaji wa uhakika ili waweze kujikwamua kimaisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine iliyozungumzwa hapa ni habari ya STAMICO na kwa sababu tuko wengi wenzangu watakuja kuzungumza hapa lakini mimi nieleze eneo moja la madeni ya STAMIGOLD.

STAMIGOLD ni kampuni iliyoanzishwa na Shirika la Taifa la STAMICO na ikarithi mgodi mmoja wa Tulawaka. Shida tuliyoipata pale ni suala la management. Watu wamekwenda pale bahati mbaya sana baada ya kufika pale wametengeneza utaratibu kana kwamba tayari wamekwisha ku-break even. Wamejilipa mishahara mikubwa, wameweka gharama kubwa za uendeshaji, wazabuni wamefanya tendering kwa bei kubwa sana, imetokea sasa mgodi ule hauwezi kutengeneza faida.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yetu pamoja na mambo mengine tumechukua hatua tisa za kwanza za kufanya. Moja, kuhakikisha kwamba tunabadilisha management yote ya STAMIGOLD na kuweka management ya watu ambao ni waadilifu. Pili, tunatafuta wazabuni ambao bei zao ni bei shindani, bei nafuu, bei za soko. Tunataka tuhame kwenye exaggerated prices twende kwenye bei ambazo ni halisi za soko na hili jambo tunalifanya kwa nguvu zote. Kwa mfano, kwenye mzabuni anayetupatia mafuta tumempata Puma ambaye bei yake anayotuuzia ina upungufu wa Sh.159, lakini zamani ungeweza kuona kwamba bei ya mafuta tuliyokuwa tunanunua ilikuwa kubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niwaombe Waheshimiwa Wabunge watuamini, Wizara hii ni mpya tunafanya kila tuwezalo kuhakikisha kwamba hatuliangushi Bunge hili na zaidi sana hatumuangushi Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Watanzania wote ambao wameiamini Serikali ya CCM iweze kuwaongoza. Naomba niwaombe mtupe muda, kuna kazi kubwa tunaifanya kwa STAMIGOLD, baada ya muda mtaona mabadiliko na matokeo makubwa kama ambavyo mmeshauri. Naomba niseme kwamba ushauri wa Waheshimiwa Wabunge juu ya STAMICO na STAMIGOLD tunauchukua na hatupuuzi ushauri wa aina hata mmoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine imezungumzwa juu ya kuwasaidia wachimbaji wadogo kwa kufanya utafiti. Hapa nataka nitoe mfano mmoja kwa hoja ya Mheshimiwa Kanyasu, Mbunge wa Geita ambaye alizungumzia habari ya utafiti wa GST kwenye Wilaya ya Bukombe ambako na yeye ana wananchi wake wanachimba kule.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge kwamba utafiti uliofanyika kule Bukombe ni wa awamu ya mwanzo, lakini kuna utafiti unaotakiwa kufuata ambao ni geochemistry, tulikuwa hatujawahi kuufanya; tumefanya geophysics, tukimaliza tunakwenda kwenye geochemistry ili tuweze kujua miamba iliyoko pale ina madini ya namna gani na yenye dhahabu kiasi gani. Namuomba Mheshimiwa Mbunge awe na subira baada ya muda tukipata fedha tutapeleka GST waende wakakamilishe utaratibu ule walionao.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Nachuma amezungumza mambo mengi juu ya Kamati, kwamba Kamati ya Tanzanite ya Mheshimiwa Spika iliyoundwa hapa ilikuwa na mapendekezo mengi haoni matokeo. Naomba nimhakikishie, kama ambavyo Mheshimiwa mtoa hoja alivyotoa kwenye hotuba yake, dira yetu pamoja na mambo mengine ni pamoja na hizo taarifa za Mheshimiwa Spika. Naomba nimhakikishie na kwa uhakika kabisa, mapendekezo yote ya Kamati zote zilizoundwa, kuanzia zile za Mheshimiwa Rais pamoja na za Mheshimiwa Spika, sisi kama Wizara tumezitengenezea matrix na time frame ya kuweza kuzitekeleza, hata hiyo One Stop Centre nayo tunaijenga ndani ya ukuta.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye suala la tanzanite hatuna mzaha, tunatamani kuona madini haya yanawafurahisha Watanzania. Tutoke kwenye aibu ya kuona madini haya yanapatikana kwenye nchi nyingine na hapa Tanzania sisi tunakuwa wageni. Naomba nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba kazi hii tunaifanya na tumeshaanza na tuko mbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata haya mabadiliko, mimi nilidhani wakati huu Mheshimiwa Mbunge angetupongeza na angempongeza Mheshimiwa Rais kwa sababu moja ya mapendekezo yaliyokuwepo ni kujenga ule ukuta, ameona tumeujenga. Tunakwenda kwenye hatua nyingine ya udhibiti, tunakwenda kwenye kuhakikisha kwamba tunakuwa na eneo moja la kuuzia madini hayo ili kila mtu anayechimba madini yale aseme nina madini ya namna hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ya kudhibiti madini, moja ambayo ni ya msingi sana ni kuondoa urasimu, hutakimbiza mwekezaji lakini la pili ni kupigana na rushwa, uondoe rushwa kwenye mfumo. Ndiyo kazi ambayo Mheshimiwa Angellah Kairuki anahangaika nayo kwenye hii Wizara. Bahati nzuri wafanyakazi wetu tunakubaliana kwamba tuna wajibu wa kujenga image ya Wizara yetu kwa kufanya kazi kwa nguvu lakini kuwaondolea urasimu watu wanaohitaji huduma ofisini kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama kuna jambo anahitaji mtu kulipata leo mpe leo kama amekidhi vigezo, hakuna sababu ya kumwambia njoo kesho wakati anastahili kupata ili utengeneze mazingira binafsi. Hili jambo tutapigana nalo kwa nguvu zote na kwa hili hatutaangalia mtu usoni. Tunataka Mtanzania yule mwenye haki apate haki yake, tunataka Mtanzania anayekuja Ofisi yetu ya Madini asiwe na mazingira ya aina yoyote ya kuomba rushwa au kiashiria, hata kukonyezwa tu kwamba mtu anataka rushwa, tunataka kuondoa hali hiyo. Tupeni muda, tumejipanga, Waziri wetu anatupa maelekezo kila siku. Sisi watendaji, Katibu Mkuu na Tume ya Madini tutafanya kazi hii kwa nguvu zetu zote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Alhaj Bulembo amezungumza habari ya wachimbaji wadogo kuwapatia leseni, hili ndilo jambo tunalolifanya. Kila mahali kunakotokea rush tukawakuta wachimbaji wadogo, tukiangalia tukakuta hakuna leseni ya mtu kazi ya kwanza tunayoifanya na tunawashirikisha Waheshimiwa Wabunge, tunawarasimisha wale wachimbaji wadogo waliogundua hayo madini ili wachimbe kihalali, watoke kwenye uchimbaji wa kubahatisha wawe na nyaraka ili mtu yeyote akija kuwaona akute ni watu halali. (Makofi)


Mheshimiwa Naibu Spika, tumefanya hayo mambo maeneo mengi na Mheshimiwa Alhaj Bulembo angekuwepo ni shahidi, kule alikokuwa anazungumzia Geita tumerasimisha, ukienda Nyakavangala kule Iringa tumerasimisha, hata Mundarara, kule alikozungumza Mheshimiwa Kalanga na kwenyewe tunawarasimisha. Lengo ni kuhakikisha kwamba wanafanya kazi katika hali ambayo ni rasmi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Joel ameeleza habari ya CSR kwenye jimbo lake na kwenye ule Mgodi wetu wa Itiso ambako wanachimba dimension stones. Nimekwenda mwenyewe Itiso, kampuni ile inafanya kazi kubwa, ina deposit kubwa ya mawe, tena yenye gharama kubwa na wao tuliwaambia na wanafanya vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda kule Itiso kampuni hii imewachimbia maji wananchi, wanapata maji ya kunywa, lakini imekuwa ikitoa michango mbalimbali kwenye jamii. Lengo ni kurudisha huduma kwa wananchi ili kupata kile kitu kinachoitwa license on operation, upate kukubalika kwa wanajamii ili wakati unafanya kazi yako iwe rahisi kwako.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo limezungumzwa hapa ni jambo ambalo Mheshimiwa Ndassa amelieleza. Naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Ndassa, yeye anawatetea wachimbaji wakubwa na wawekezaji. Mimi niseme, Serikali ya Awamu ya Tano nia yake ni kuhakikisha kwamba wawekezaji wote wenye nia njema ya kuja kuwekeza Tanzania kwa hali ya win-win situation wanakaribishwa milango iko wazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwatoe wasiwasi Waheshimiwa Wabunge, mimi toka nimeteuliwa ukikaa pale ofisini wawekezaji wanaokuja ofisini kuomba appointment waweze kuzungumza mambo ya uwekezaji ni wengi huwezi kuwamaliza. Ndiyo maana kuna Mbunge mmoja amesema tunakaa mpaka saa mbili usiku, si kwamba tunakaa tunaangaliana, hapana, tunakutana na wawekezaji wa kila namna. Tunachotamani kukiona kwenye Wizara yetu na wawekezaji wetu, wawe wawekezaji ambao ni genuine, si wawekezaji wajanja wajanja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwekezaji ambaye anakuja kwetu hana hata mtaji anataka kuja kutumia rasilimali za Tanzania kutafuta mtaji kisha awekeze hapa, hao hawana nafasi. Mwekezaji ambaye amejipanga kuja kufanya kazi Tanzania tunamkaribisha, tunatamani uwekezaji wa fedha za kigeni ndani ya nchi na hii ndiyo dira ya Mheshimiwa Rais wetu, tunataka tuwaone Watanzania wanafanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwenye Mgodi wa Magambazi nini kilichotokea? Pale kulikuwa na wachimbaji wadogo zaidi ya 5,000, wale wachimbaji wadogo wamechimba wametengeneza marudio lakini ile leseni ilikuwa ya mtu mwingine, tukawaondoa wachimbaji wadogo wampishe mchimbaji mkubwa mwekezaji. Bahati mbaya kumbe yule mchimbaji mkubwa yeye hakuwa na huo mtaji wa kuwekeza pale, yeye akaja kuchukua yale marudio ya wananchi anachenjua hayo anapata pesa. Sasa hatuwezi kutumia nguvu ya Watanzania kwa ajili ya mwekezaji wa kigeni kwa kigezo kwamba eti ni mwekezaji. Hawa ni Watanzania wametumia nguvu yao, wamesaga mawe, wametengeneza marudio, kama ni mchimbaji kweli akachimbe naye kama wao walivyochimba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumetuma timu ya kwenda kukagua kule, wametuletea mapendekezo, zaidi ya sheria 19 zimevunjwa, sasa tunampa maelekezo namna gani afanye ili aweze kutekeleza sheria yetu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Ndassa Wizara yetu iko tayari kumsaidia mwekezaji yeyote ambaye yuko tayari kufuata sheria. Kama kuna mwekezaji mwingine yeyote, sio wa Magambazi tu, wa pande kuu nne zote za Tanzania ambaye anadhani anaweza kuja Tanzania na briefcase bila mtaji akaupata hapa akarudi kwao akiwa tajiri, zama hizo zimepitwana wakati. Tunataka mtu aje awekeze mtaji, tumsaidie sisi apate leseni na yeye apate kitu cha kuacha hapa kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba nirudie tena kukushukuru sana kwa kunipa nafasi, lakini nirudie kusema namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa imani kubwa aliyonipa, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa namna anavyoendelea kutufundisha kufanya kazi. Ni bahati mbaya tu Mheshimiwa Waziri amekaa nyuma, nilitamani niseme maneno haya ninamuona ilia one sura yangu inachokisema ninakusudia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja, nakushukuru sana.